Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Samia, Ndayishimiye wapongezwa diplomasia ya uchumi

4608e2dbb48842b8dfcdc8499ca364fb.jpeg Samia, Ndayishimiye wapongezwa diplomasia ya uchumi

Tue, 12 Jul 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Katibu wa Chama Tawala Nchini Burundi cha CNDD-FDD, Reverien Ndikuriyo amepongeza hatua ya Rais Samia Suluhu Hassan na Rais wa Burundi, Evariste Ndayishimiye kwa kuendelea kuimarisha diplomasia ya uchumi.

Ndikuriyo alisema hayo jana jijini Dodoma alipotembelea kiwanda cha mbolea cha Intracom kinachojengwa na mwekezaji kutoka Burundi kwa gharama ya dola za Marekani milioni 180 na kitakuwa na uwezo wa kutoa ajira 3,000.

Alisema juhudi za viongozi hao zimechangia kuwapo kwa wawekezaji wa Burundi waliokuja kuwekeza Tanzania.

“Niwapongeze marais wetu kwa kudumisha diplomasia ya uchumi.

Hatua hii imefanya kujengwa kiwanda cha mbolea ambacho ni kikubwa zaidi ya kilichoko Burundi ambacho kwa sasa kuna mpango wa kukipanua zaidi,” alisema Ndikuriyo na kuongeza kwamba kiwanda hicho ni fursa nzuri ya kutoa ajira kwa vijana wa Kitanzania.

Alisema hatua ya kuja kuwekeza Tanzania ni kusaidia upatikanaji wa mbolea na kushirikiana na ubunifu wa Burundi wa kuzalisha mbolea rafiki wa mazingira.

Ndikuriyo pia alitembelea Chuo Kikuu cha Dodoma, ujenzi wa stendi ya kisasa na kiwanda cha mvinyo na kusema katika miaka 60 ya Uhuru Tanzania imezidi kupiga hatua katika maendeleo na imeendelea kuwa salama.

“Burundi na sisi tumeanza kuwa salama. Uongozi wa Chama cha CNDD-FDD kinachoongoza nchi kwa miaka 17 kimeendelea kudumisha amani na usalama wa nchi na kuwabana wahalifu,” alisema.

Akiwa kwenye soko la Wamachinga, Ndikuriyo amepongeza serikali kwa kujali kundi la wafanyabiashara wadogo kwa kuwawekea miundombinu mizuri.

“Nilipofika hapa nilikuwa nahoji mamantilie wamewekwa wapi? Hakika mmewajali wafanyabiashara wadogo.

Tulikuwa tunasikia wamachinga wanapewa vitambulisho kwa shilingi 20,000 na sasa mnawawekea miundombinu, hii mmefanya jambo jema nasi tutajifunza kupitia ubunifu huu.”

Naibu Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Bara, Christina Mndeme alisema Rais Samia Suluhu Hassan amekuwa akisimamia diplomasia ya uchumi na ndio maana Serikali ya CCM imeendelea kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji.

“Niwasihi wafugaji kwa uwekezaji huu kinyesi cha mifugo ni mali hivyo ni vyema kuanza kujipanga kufuga zaidi ili kuzalisha bidhaa hiyo kwa wingi na ambayo itakuwa ni asilimia kubwa ya malighafi kwenye kiwanda hicho,” alisema Mndeme.

Mhandisi wa Intracom, Emmanuel Ngowi alisema awamu ya kwanza ya uzalishaji inaanza muda wowote ndani ya mwezi huu na kwamba kiwanda kitakuwa na uwezo wa kuzalisha tani 600,000 za mbolea na tani 300,000 za chokaa kwa mwaka.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live