Dar/Dodoma. Huku wavuvi na wauzaji wa sakama katika Soko la Kimataifa la Samaki la Feri wakiirushia lawama Serikali kutokana na kuadimika kwa kitoweo hicho, Serikali imeamua kuwafutia makosa wote walioshtakiwa kwa kutokuwa na leseni, ikitaka waachiwe.
Jana, wavuvi na wauza samaki walisema Serikali inahusika na kuadimika kwa samaki katika soko hilo baada ya kuanzisha operesheni ya ukaguzi wa leseni za uvuvi, ikiwa ni tofauti na maelezo yaliyotolewa kwa maandishi na Wizara ya Mifugo na Uvuvi.
Mwenyekiti wa Umoja wa Madalali wa Biashara ya Samaki, Abdallah Hamis alisema uvuvi umeshuka kwa asilimia 70 na kuathiri upatikanaji wa samaki aina ya vibua ambao wamepanda kutoka wastani wa Sh75,000 kwa kilo 25 hadi Sh150,000.
Alisema, ndoo moja ya kilo 20 ya dagaa, wanaojulikana zaidi kama dagaa mchele, imepanda kutoka wastani wa Sh30,000 hadi Sh80,000 huku kilo 10 za samaki aina ya tasi ikipanda kutoka Sh60,000 hadi Sh150,000 ilhali bei ya fungu la samaki 30 aina ya changu ikipanda kutoka Sh70,000 hadi Sh140,000.
Hata hivyo, wakati taarifa zikionyesha kupanda ghafla kwa bei ya samaki, Serikali imewafutia adhabu wavuvi wote waliokamatwa mwaka huu kwa makosa ya kutokuwa na leseni na kuwataka wanaowashikilia, wawaachie mara moja. Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega alisema jana mjini Dodoma kuwa licha ya uamuzi huo tangu juzi wavuvi hawajafanya kazi yao kutokana na baadhi yao kukamatwa.
Aliagiza wavuvi wote waendelee kukatiwa leseni hadi Januari 31, na kuwataka maofisa wa wizara na halmashauri waanze kuwafuata kwenye mialo ili kuwakatia leseni kwa mujibu wa sheria.
Mwenyekiti wa Umoja wa Wavuvi Wadogo, Ali Alawi alisema hakuna mvuvi aliyegoma kulipia leseni, lakini wanashangazwa na utaratibu wa kukamatwa na kutozwa faini za juu kinyume na sheria.
“Leseni ya Sh23,000 kwa sasa ukikamatwa unalipa faini Sh600,000, hii wameitoa wapi? Kwa sheria ipi? Mbona muda wa kulipia (leseni) bado uko sawa kikanuni,” alisema.
Amina Said, mfanyabiashara wa samaki sokoni hapo, alisema juzi hakupata dagaa mchele ambao amekuwa akinunua kwa Sh80,000 kwa ndoo
“Kama dagaa wamepanda bei inabidi na sisi tupunguze kipimo au kuongeza bei, bila hivyo itakuwa ni hasara tu,” alisema.
Mwenyekiti wa Wamiliki wa Boti za Uvuvi, Saleh Msean alisema boti saba zimekamatwa na kila moja italazimika kulipia faini ya Sh3.3milioni.
Awali, Ofisa Uvuvi wa soko hilo, Ahmed Mbarouk alisema wavuvi wameanza kuchukua fomu za leseni na hakuna anayeruhusiwa kuvua samaki bila leseni. Soko hilo linakadiriwa kuwa na wavuvi 7,000.