Mbunge wa Sikonge (CCM), Joseph Kakunda amehoji kwanini Serikali isitoe ruzuku ya Sh432 bilioni kwa ajili ya kuondoa nyumba za nyasi nchini Tanzania.
Akiuliza swali la nyongeza bungeni leo Ijumaa Juni 3, 2022, Kakunda amesema kwa mujibu wa sensa ya watu na makazi ya mwaka 2012 Tanzania ina nyumba zaidi ya milioni 11.8.
Amesema nyumba bora ni milioni 3.4 sawa na asilimia 37.1 maana yake kuna nyumba zaidi ya milioni nane zisizo bora huku nyumba milioni 2.3 sawa na asilimia 25.4 ni zilizoezekwa na nyasi.
“Nyumba ya vyumba viwili inahitaji Sh 400,000 za kununulia bando mbili za bati. Kwanini mtu asitoe Sh200,000 na Serikali ikachangia Sh200,000 ili hatimaye itoe Sh432 bilioni kuondoa kabisa nyumba za nyasi katika nchi hii?”alihoji.
Katika swali lake la pili, Kakunda alihoji ni kwanini Serikali isiweke viwango vya nyumba bora ili kila mwananchi azingatie viwango hivyo.
Akijibu swali hilo Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Makazi, Ridhiwani Kikwete alisema watakapokamilisha Sera ya Nyumba na Makazi jibu la swali lake litakuwa ndani ya sera hiyo.
Alisema wizara imeendelea kuandaa rasimu ya Taifa ya Nyumba ambayo pamoja na mambo mengine itatoa mwongozo wa viwango vya nyumba bora vinavyotakiwa kuzingatiwa na watu wanaojenga.
“Sera hiyo pia itaweka uratibu wa upatikanaji wa vifaa vya gharama nafuu, upatikanaji wa mikopo ya nyumba, mfumo wa uratibu wa wadau wa nyumba na hivyo upatikanaji wa nyumba bora kuwa nafuu,”alisema.
Kwa upande wake Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Lucy Mayenga amesema sababu kubwa inayofanya wananchi washindwe kujenga nyumba bora ni gharama kubwa za vifaa vya ujenzi.
“Kwa kuwa suala hili liko pia katika Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara, sasa wizara hii ipo tayari kukaa na wizara hiyo ili kuangalia sababu zote zinazofanya vifaa vya ujenzi kuwa na gharama kubwa?”alihoji.
Alitaja sababu hizo ni matamko ya viongozi, gharama kubwa za kodi na changamoto nyingine.
Akijibu swali hilo, Ridhiwani alisema yapo maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan ya wizara zote zinazohusika na jambo hilo kukaa kwa pamoja ili kuhakikisha gharama za ujenzi wa nyumba bora unakuwa nafuu, vifaa na mazingira yanakuwa mazuri katika upatikanaji wa nyumba bora na salama.