Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Sakata la uwekezaji wa Bandari bado halijatulia

Bandari Chachamaa Sakata la uwekezaji wa Bandari bado halijatulia

Wed, 4 Oct 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Zikiwa zimepita wiki mbili tangu Shirika la Bandari Zanzibar (ZPC) lilipokabidhi bandari hiyo kuendeshwa na mwekezaji kampuni ya Africa Global Logistics (AGL) ya Ufaransa, Septemba 18, 2023, bado wadau wa bandari wanazidi kulalamikia utaratibu unaotumika.

Wakizungumza na Mwananchi Digital kwa nyakati tofauti, wadau wa bandari walisema licha ya kuelezwa kwamba ametafutwa mwekezaji kumaliza changamoto za bandari, hali imekuwa tofauti na iwapo itaendelea hivyo itavuruga uchumi wa nchi.

Mwenyekiti wa Chama cha Mawakala wa Forodha Zanzibar (ZFB), Omar Mussa alisema wanaendelea na kazi, lakini hali bado haijakaa sawa kwa sababu bado kuna changamoto nyingi zinaendelea kujitokeza.

“Hawa (AGL) walikuja kama wawekezaji na kazi ya mwekezaji ni kuwa na vitendea kazi, lakini uwekezaji wao bado hatujaona ufanisi wake kwa sababu vifaa hawana, nguvu kazi nazo ni shida, mfumo shida,” alisema Omar.

Alisema walitarajia kuwa kampuni hiyo ingefanya kazi kimataifa zaidi, lakini kwa namna wanavyofanya kazi inaonekana hawana uwezo mkubwa

Alisema kwa siku walikuwa wanatoa kontena 150, lakini kulingana na utaratibu uliopo kwa sasa zinaweza kutoka kontena 15 au 30 .

Alisema kontena zilizofika zaidi ya wiki mbili zilizopita zinaanza kutozwa fedha za uhifadhi wakati kilichochelewesha ni utaratibu uliopo unaoongeza gharama badala ya kupunguza.

“Bado mpaka sasa hatujaona mabadiliko, maana awali sisi wenyewe kwa wenyewe tulikuwa tunajuana kwamba unaweza ukashughulikia kontena fulani unapata fursa hiyo, lakini kwa sasa hakuna ruhusa hiyo.”

Alisema mbali na kuwa eneo dogo, hata vifaa vya kufanyia kazi havipo, hivyo hakuna muujiza utakaoweza kubadilisha ufanisi.

Mmiliki wa meli, Mansour Said alisema bado wanaendelea kupiga kelele, lakini changamoto zipo pale pale.

“Unalipia risiti za ushuru wa bandari (walphage) lakini unashindwa kupatiwa huduma, unatumia siku nzima kushughulikia masula ya ushuru.

Alisema siku ya Jumamosi wanafanya kazi kuanzia saa 6:00 mchana hadi saa tatu usiku lakini siku hizi hawafanyi kazi usiku.

Nao uongozi wa kampuni tanzu ya AGL, Zanzibar Multipurpose Terminal (ZMT) inayosimamia bandari ilisema changamoto nyingine zinaanza kushughulikiwa.

Mkurugenzi Mtendaji wa ZMT, Nicolas Escalin alisema wanajipanga kujenga bohari ya makontena nje ya bandari ili kupunguza msongamano katika bandari hiyo.

Alisema kwa sasa changamoto nyingine zinaendelea kupatiwa ufumbuzi kwa sababu wanalenga kuwa na miundombinu yenye uwezo wa kushughulikia uagizaji na uuzaji wa nje kwa kufuata viwango vya kimataifa.

Alisema watajenga miundombinu ya kisasa yenye uwezo kuhakikisha mtiririko mzuri wa kupandisha na kushusha makontena.

Alisema mpaka sasa wameshusha makontena 300 tangu wakabidhiwe bandari hiyo na imechukua wafanyakazi 400 waliokuwa ZPC.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa ZPC, Nahat Mahfoudh alisema changamoto zinaendelea kufanyiwa kazi, maana lengo la Serikali ni kuwa kituo cha usafirishaji bora cha kanda.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live