Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Sakata la korosho lapunguza mapato ya mauzo ya mazao nje

36960 Pic+korosho Sakata la korosho lapunguza mapato ya mauzo ya mazao nje

Thu, 17 Jan 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Uamuzi wa Serikali kuzuia korosho kuuzwa nje umesababisha upungufu wa takribani dola 500 milioni za Marekani katika urari wa malipo kwa mwaka ulioishia Novemba 2018.

Ripoti ya mwezi ya Benki Kuu (BoT) ya Desemba 2018 imeonyesha urari wa jumla wa malipo (BoPs) ukiwa na upungufu wa dola 753.0 milioni kwa mwaka ulioishia Novemba 2018 ikilinganishwa na upungufu wa dola 171.6 milioni iliyorekodiwa Oktoba ya mwaka huo.

Ripoti hiyo inasema mapato ya mauzo ya korosho, ambalo ni zao linaloongoza kwa mauzo ya nje ya nchi, yameshuka kutokana na uamuzi wa Serikali kununua zao hilo kutoka kwa wakulima na kuzibangulia katika viwanda vya ndani.

Mauzo ya korosho nje ya nchi yamekuwa yakifikia dola 575 milioni, mauzo ambayo ni sawa na mazao mengine matano ya biashara; pamba, tumbaku, chai, kahawa na katani.

Hivi karibuni, Serikali ilitangaza kuwa itanunua zaidi ya tani 200,000 za korosho kutoka kwa wakulima katika mikoa inayozalisha kwa wingi zao hilo, ili iziuze nje ya nchi baada ya kuzibangua kwa kutumia viwanda vya ndani.

Serikali ilifikia uamuzi huo baada ya wafanyabiashara kuweka bei ya chini ya Sh3,000 kwa kilo ya korosho ghafi tofauti na msimu uliopita wakati wakulima walipouza zao hilo kwa hadi Sh4,000.

Pamoja na Serikali kuwaita wafanyabiashara hao Ikulu na kutoa muda kwa wanaotaka kununua kujitokeza, ni wachache waliojitokeza na hivyo Rais John Magufuli akatangaza kuwa Serikali itanunua korosho yote na itazikusanya kwa kutumia magari ya jeshi.

Hata hivyo, hadi sasa Serikali imemudu kununua korosho za takriban Sh200 bilioni kwa bei ya Sh3,300 kwa kilo, hiyo ikiwa ni takriban theluthi moja ya shehena inayotarajiwa kununulia.

Ripoti hiyo inasema pamoja na korosho, mauzo ya mazao ya biashara nje ya nchi yalipungua kwa asilimia 1.0 hadi kufikia dola 885 milioni kwa mwaka huo unaoishia Novemba 2018 kutokana na kuanguka kwa mapato ya chai na karafuu.

“Wakati huohuo, kushuka kwa thamani ya mauzo ya chai nje kulitokana na kupungua kwa kiwango cha zao hilo kilichouzwa pamoja na bei,” inasema ripoti hiyo.

Hata hivyo, inasema zao la pamba lilikuwa na ongezeko kubwa la mapato ya nje kutokana na kusafirisha kwa wingi baada ya msimu wa mwaka 2017/18 kuwa wa neema pamona bei katika soko la dunia kuwa juu.

Ripoti ya BoT pia inaonyesha akaunti ya malipo ilikuwa na dola 11,749.8 milioni kwa mwaka ulioishia Novemba 30,2017.

Inasema kuongezeka kwa nakisi katika urari wa malipo kwa kiasi fulani kunaelezewa kuwa kulitokana na kupanuka kwa nakisi ya akaunti ya malipo.

Kwa hali hiyo, salio katika akaunti ya malipo kulikua hadi kufikia nakisi ya dola 2.5 bilioni, kutoka dola 1.4 bilioni. Hiyo ni kutokana na kushuka kwa mauzo nje ya nchi huku kukiwa na ongezeko la bidhaa kutoka nje.

Thamani ya bidhaa na huduma zinazouzwa nje ya nchi zilishuka kwa dola 8.5 bilioni kwa mwaka ulioishia Novemba 2018 ikiwa chini kidogo kulinganisha na Novemba 2017. Hiyo ilikuwa ni anguko kwa mauzo ya bidhaa za nje.

Mapato kutokana na bidhaa zinazouzwa nje ya nchi kwa mwaka unaoishia Novemba 30, 2018 yalishuka ikilinganishwa na mapato ya mwaka ulioishia kipindi kama hicho mwaka 2017. nchi zikiwa sawa na asilimia 38.0 ya mauzo ya nje na huduma na asilimia 71.4 ya bidhaa.

Mauzo ya nje ya bidhaa zisizo za kitamaduni yameshuka kwa asilimia 9.7 hadi Dola3.2 bilioni ikiwa ni anguko kubwa lililoonyeshwa , isipokuwa bidhaa za mbogamboga.

Mapato kutokana na mauzo ya dhahabu ambayo ndiyo bidhaa kubwa isiyo ya kitamaduni nayo yameshuka katika mauzo ya nje.



Chanzo: mwananchi.co.tz