Waziri Wa Nishati, January Makamba anatarajia kuzungumza na wadau na wafanyabiashara wa nguzo nchini ili kuweza kutoa ufafanuzi juu ya tamko la Serikali la kuagiza nguzo kutoka nje ya nchi.
Hivi karibu Serikali ilitoa tamko la kutaka kuagiza nguzo hizo nje ya nchi kwa kile kinachodaiwa kuwa nguzo za umeme zinazozalishwa nchini hazina ubora hii ni baada ripoti ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kukutwa kwa shehena za nguzo ambazo hazina ubora zikiwa mkoani Mtwara kwa ajili ya usambazaji wa umeme vijijini (REA).
Waziri huyo anatarajiwa kufika wilayani Mufindi mkoani Iringa kesho Jumamosi Aprili 30, 2022 kwa ajili ya kukutana na wadau na wafanyabiashara hao wa nguzo ili kuweza kutoa ufafanuzi juu ya suala hilo.
Akizungumza na mwananchi leo Mwenyekiti wa Chama Cha Wafanyabiasha wa Nguzo nchini (Wanguta) Negro Sanga amesema ujio huo wa Waziri wa Nishati utasaidia kutoa ufafanuzi wa maswali magumu ambayo walikuwa wanajiuliza hususani katika biashara hiyo ya nguzo.
"Kwa siku hizi karibu tulisikia kwamba Serikali inampango wa kuagiza nguzo nje ya nchi taarifa hiyo ilileta taharuki kwa wadau wa mikoa ambayo inafanya shughuli hizi ikiwamo Iringa pamoja na Njombe na kwa kila mwananchi ambaye anafanya biashara hii." amesema Sanga
Sanga amesema kuwa kikao hicho cha Waziri na wadau hao kitasaidia kupata majibu na msimamo wa Serikali kuhusu jambo hilo.
Kwa upande wake Katibu wa Umoja wa Wavunaji wa Sao Hill, Dk Bazil Tweve amesema uagizaji wa nguzo nje ya nchi utasababisha kupoteza ajira kwa vijana wengi.
"Ukiangalia katika mnyororo wa thamani tangu mti kupandwa hadi kuvunwa kuagiza kwa nguzo hizo nje ya nchi kutasababisha kunapoteza ajira kwa vijana wengi wa kitanzania." amesema Tweve
Ameiomba Serikali kuachana na uamuzi huo kwa sababu viwanda vilivyopo vinauwezo mkubwa wa uzalishaji kiasi cha nguzo milioni 300 kwa mwaka wakati mahitaji ya nguzo milioni moja kwa mwaka.
"Tunaomba Serikali itafakari upya kuhusu uamuzi huo wa kuchukua nguzo nje ya nchi wakati hapa nchini zipo kwa kufanya hivyo watawavunja moyo wananchi kupanda miti katika maeneo yao." Amesema Tweve.