Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Sakata la Kadco laibuka bungeni

Bungeni 660x400 Sakata la Kadco laibuka bungeni

Wed, 3 Apr 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson amesema Uwanja wa Ndege wa Kilimanjaro uko chini ya Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) na kuwa hakuna namna ambavyo Serikali itaweza kudharau ama kwenda kinyume na Bunge.

Novemba mwaka juzi wakati wabunge wakipitia ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Bunge liliazimia uwanja huo, uliokuwa chini ya Kampuni ya Uendelezaji na Uendeshaji wa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Kilimanjaro (KADCO), ukabidhiwe kwa TAA.

Hata hivyo, Novemba 2023, Kamati ya Bunge ya Miundombinu ilirejea tena na jambo hilo bungeni na Serikali ilitoa ufafanuzi kuwa kulikuwa na mkataba mmoja bado wa upangaji.

New Content Item (1)

Novemba 10, 2023, Kamati ya Kudumu ya Miundombinu ikiongozwa na mwenyekiti wa kamati hiyo, Moshi Kakoso walikwenda kushuhudia makabidhiano ya uwanja huu kati ya Kampuni ya Kadco kwa TAA.

Hata hivyo, Machi 10, 2024, Kadco ilitoa siku 21 kwa wananchi 1,712 wa vijiji vinane waliovamia eneo la Uwanja wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) kuondoka ili kupisha shughuli za uendelezwa wa uwanja huo, ni miongoni mwa mambo yanayozua utata.

Akizungumza baada ya kipindi cha matangazo bungeni leo Jumanne Aprili 2, 2024, Dk Tulia amesema baada ya makabidhiano hayo, Bunge lilimaliza kazi yake na masuala ya kiutendaji yanabakia kwa Serikali.

“Bunge haliwezi kufuatilia huko kung’ang’ania nani amefanya nini, nani amesaini barua gani hiyo sasa tutakuwa tunaenda nje ya ule utaratibu ambao tumejiwekea wa mgawanyo wa majukumu na madaraka kwa mujibu wa Katiba,”amesema.

Dk Tulia amesema Machi 10 mwaka huu kulitokea changamoto, Kadco ilitoa notisi ya siku 21 kwa wananchi wahame kwenye eneo hilo.

Amesema changamoto ikajitokeza kwa kuwa barua hiyo iliandikwa na Kadco wakati Bunge na Serikali ilishakabidhi kwa TAA, hivyo wangetarajia kuwa barua hiyo iandikwe na TAA na sio Kadco.

Amesema kilichotokea ni suala kwa utendaji wa ndani ya Serikali na kwamba wao kama Bunge hawawezi kuingia huko kwenye utendaji wa Serikali labda itokee changamoto.

“Kwa mutadha huo ule mjadala uliokuwa unaashiria pengine Bunge limedharauliwa kwa Kadco kuandika barua huo ni mchanganyiko pengine wa upande wa Serikali na sisi hatuingii katika utendaji. Lakini kwa upande wa maamuzi Bunge lilishafanya,”amesema.

Amesema pia, Bunge lilishashughudia kuwa uwanja huo umehamia TAA, hivyo Bunge linafahamu lilishafanya uamuzi kuhusu jambo hilo na hakuna namna ambapo Serikali itadharau ama kwenda kinyume na maamuzi ya Bunge.

“Wabunge na wananchi wasiwe na wasiwasi kuhusu jambo hilo, Bunge lao linafanya kazi yake inayostahili na Serikali inafanya kwa sehemu yake yale ambayo kikatiba wanapaswa kufanya,”amesema.

Dk Tulia amesema kama kutatokea changamoto basi Bunge litashughulika nalo lakini kwa sasa Serikali imepewa muda ikalifanyie kazi jambo hilo na wanaamini watapata taarifa.

“Lakini kwa sasa hali iko hivyo Uwanja wa Kimataifa wa Kilimanjaro uko chini ya TAA,”amesema Dk Tulia.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live