Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Safari za anga Songea zitakavyofungua anga la wawekezaji na watalii

975c11ed45cf7dfc2f6b87bd8c7350d4 Safari za anga Songea zitakavyofungua anga la wawekezaji na watalii

Sun, 28 Feb 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

KAMPUNI ya Ndege Tanzania (ATCL) imerejesha safari za usafiri wa anga mkoani Ruvuma baada ya kukamilika kwa ukarabati wa kiwanja cha ndege cha Ruhuwiko mjini Songea.

Serikali ilitoa zaidi ya shilingi bilioni 37 kukarabati kiwanja cha ndege Songea na kuwezesha ndege aina ya Bombardier Q400 kuanza tena safari zake Songea kuanzia Februari 17 mwaka huu.

Akizungumza mara baada ya kushuka katika safari ya kwanza ya Bombadier kwenye uwanja wa Songea, Waziri wa Maliasili na Utalii ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Songea mjini, Dk Damas Ndumbaro, amesema kuanzishwa kwa safari ya anga mkoani Ruvuma ni utekelezaji wa Ilani ya CCM.

Anasema ibara ya 58 ya Ilani ya CCM imetamka kwamba uwanja wa ndege wa Songea utajengwa na pia imetamka kwamba zitanunuliwa ndege 11 mpya.

Anasema pia ilani imetamka kuwa ATCL itaongeza safari za ndege kutoka viwanja vinne mwaka 2015 hadi viwanja 13, mwaka 2021, Songea ikiwa moja ya viwanja hivyo.

Anasisitiza kuwa kiwanja cha Ndege Songea kitafungua anga la mkoa wa Ruvuma na kuruhusu wawekezaji na watalii kufika Ruvuma kujionea fursa mbalimbali za uwekezaji na utalii hivyo kuchangia pato la taifa na kuinua uchumi wa wananchi wa Mkoa wa Ruvuma na Taifa kwa ujumla.

Kwa upande wake, Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Pololet Mgema, anampongeza Rais John Magufuli kwa kutoa fedha kiasi cha shilingi bilioni 37 ambazo zimekamilisha ujenzi na ukarabati wa kiwanja cha ndege cha Songea ambacho kimeanza kutumika rasmi kutua ndege kubwa.

Anasema kabla ya ukarabati wa kiwanja hicho, Mkoa wa Ruvuma ulikuwa na kiwanja cha ndege ambacho kilijengwa katika utawala wa Serikali ya Awamu ya kwanza ya Mwalimu Julius Nyerere hivyo ulikuwa umechakaa na kuhitaji ukarabati.

Amesema Kiwanja cha ndege cha Songea kilifungwa mwaka 2018 kwa ajili ya kupisha ukarabati, hali ambayo ilisababisha kero kubwa kwa wananchi kwa sababu walilazimika kulipa kati ya shilingi 600,000 hadi 700,000 kiwa ajili ya nauli kwa kutumia ndege ndogo toka Songea hadi Dar es Salaam.

Tunamshukuru sana Rais wetu sasa tuna kiwanja kipya, zinatua ndege kubwa hata nauli ni nafuu zaidi ukilinganisha na ndege za kampuni binafsi anasema Mgema.

Kwa upande wake, Meneja Kiwanja cha Ndege Songea, Jordan Mchami anasema safari za ndege za ATCL zimerejeshwa mkoani Ruvuma kwa kuanzia safari toka Dar es Salaam hadi Songea zitakuwa siku ya Jumatano na Jumapili.

“Ndege itakuwa inaondoka Dar es Salaam saa 1:00 asubuhi, itafika Songea saa 2:25 asubuhi, itaondoka Songea 2:50 asubuhi itafika Dar es Salaam saa 4:10 asubuhi, kwa kuanzia nauli ni shilingi 252,000, kwenda na kurudi ni 372,000. Natoa wito kwa wakazi wa Mkoa wa Ruvuma na mikoa jirani kutumia ndege hii,” anasema Mchami.

Kwa upande wake Meneja wa ATCL Songea, Godfrey James, anasema ndege inayotua Songea ni aina ya Bombadier Q400 yenye uwezo wa kubeba abiria 76 na kwamba kwa kuanzia itafanya safari mara mbili kwa wiki na abiria wakiongezeka safari zitaongezeka.

Naye Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Ruvuma, Odo Mwisho, anasema usafiri wa anga ni sekta muhimu katika kuchochea maendeleo na ndiyo maana serikali iliamua kupanua na kuongeza hadhi katika kiwanja cha ndege cha Songea ili kuwezesha kutua ndege kubwa.

Abdalah Mabodi, Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar akizungumza kwenye mapokezi hayo ya ndege, ameipongeza serikali kwa kuwatumia marubani wa ndege watanzania ambapo ametoa rai kuhakikisha kiwanja cha ndege kinatunzwa pamoja na rasimali zote za usafiri wa anga ili ziwe endelevu.

Mmoja wa abiria kutoka nchi Kongo (DRC), Veve Makonga, akizungumza mara baada ya kushuka na ATCL kwenye kiwanja cha Songea ametoa rai kwa watanzania kutembelea Mkoa wa Ruvuma ili kuona maendeleo makubwa yaliyofanywa na serikali ikiwemo kujenga kiwanja cha ndege cha kisasa.

Meneja wa Wakala wa Barabara (Tanroads), Mkoa wa Ruvuma, Lazeck Alinanuswe anasema Kiwanja cha Ndege cha Songea kimeboresha barabara ya kutua na kuruka ndege yenye urefu wa mita 1740, eneo la maegesho ya ndege na taa za kuongozea ndege hali ambayo inawezesha ndege kubwa kutua usiku na mchana.

Anasema Mkandarasi amekamilisha kujenga mita 1,200 za barabara ya kuruka na kutua ndege ambayo inaruhusu ndege kubwa aina ya Bombardier kutua kwa usalama.

Kwanja cha ndege wa Songea ni rasilimali adimu inayoweza kusaidia kukuza uchumi wa mji wa Songea na mkoa mzima wa Ruvuma hasa kutokana na uwanja huo kuwa ni miongoni mwa viwanja bora Tanzania.

Kiwanja cha ndege wa Songea kilijengwa kati ya mwaka 1974 hadi 1980 na kiliwekewa lami hivyo kuwa na uwezo wa kutua ndege majira yote masika na kiangazi.

Safari za anga kwa kutumia ndege za ATCL zitasaidia wadau mbalimbali kutumia muda mfupi kusafiri kwa ndege kutoka Songea na kwenda Dar es Salaam badala ya kupoteza zaidi ya saa 15 kwa kutumia usafiri wa barabarani na kuzorotesha uchumi wa Mkoa wa Ruvuma.

Mwandishi wa makala haya ni Afisa Habari Mkoa wa Ruvuma

Chanzo: habarileo.co.tz