Dar es Salaam. Rais wa Tanzania, John Magufuli leo Jumamosi Oktoba 12, 2019 amezindua safari za Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) kutoka Dar es Salaam kwenda mkoani Katavi.
Mbali na uzinduzi huo, Magufuli ameipongeza ATCL kwa kuanzisha safari hizo kwa kuwa zitachochea biashara na utalii katika mikoa ya karibu na Katavi na nchi za DRC Congo na Zambia.
Katika uzinduzi huo uliofanyika mkoani Katavi, Magufuli amesema, “ATCL liendelee kutoa huduma nzuri kwa Watanzania na muendelee kuzingatia muda.”
“Mkisema mtafika muda fulani uwe muda huo. Mnapokosa mtoe taarifa mapema. Muangalie vizuri gharama zenu ili Watanzania wafaidike na ndege hizi.”
Awali akitoa taarifa kuhusu safari hizo, mkurugenzi wa ATCL, Ladislaus Matindi amesema kutakuwa na safari moja ya Dar es Salaam kwenda Mpanda.
“Hiyo safari itakuwa Jumatano na ndege ndege itatoka Dar es Salaam kwenda Mpanda ikipitia Tabora itakayochukua saa mbili wakati wa kwenda.”
Habari zinazohusiana na hii
- Magufuli: Watu 138 wameomba msamaha kwa DPP
- Magufuli kuwashukia viongozi watakaoshindwa kuhamasisha uandikishaji Serikali za mitaa
Matindi amesema ikifika Novemba, 2019 wataongeza safari kufikia tatu kwa kuzingatia ongezeko la abiria.
Katika hatua nyingine, Rais Magufuli amesema kuna ndege nyingine moja inayoendelea kutengenezwa nchini Marekani na itawasili nchini mwishoni mwa mwaka 2019 itakayokuwa na uwezo wa kubeba abiria 262.
Mbali na ndege hiyo amesema kuna ndege nyingine tatu zinaendelea kutengenezwa.
“Tunataka Tanzania mpya ya kisasa watu wafanye biashara wazunguke wanavyotaka watengeneze pesa,” amesisitiza Magufuli.