Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Sabasaba imedhihirisha ubunifu wa kiteknolojia unaolenga kukuza uchumi

9314 Saba7+pic TanzaniaWeb

Wed, 1 Aug 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Kama ulipata nafasi ya kutembelea maonyesho ya Sabasaba yaliyomalizika Julai 15 basi utakuwa na jambo la kusimulia.

Miongoni mwa mambo hayo ni ubunifu wa kiteknolojia aina tofauti ambao uliokonga nyoyo za watazamaji wengi waliojitokeza kushuhudia mambo mapya yaliyokuwapo kwenye maonyeshonya mwaka huu.

Ni ukweli kwamba ubunifu uliokuwa ukionyeshwa katika maonyesho hayo uliwaacha watu na simulizi za kusismua hata wengine kubaki wakishangaa kama Tanzania inaweza kubuni vitu vya aina hiyo.

Wapo wanaamnini endapo ubunifu huo utatumiwa na kuendelezwa basi utasaidia kwa kiwango kikubwa kuinua na kukuza sekta ya viwanda na kukuza uchumi wa Taifa huku ukipunguza umasikini wa wananchi.

Taa ya Veta

Miongoni mwa mambo yaliyovuta hisia za wengi na kuona ubunifu wa kipekee ni taa ya kuzima na kuwasha kwa kupiga makofi ambayo ilibuniwa na wanafunzi wa Chuo cha Mafunzo na Ufundi Stadi (Veta).

Mfumo huo wa kuwasha na kuizima taa hiyo kwa kupiga makofi unaitwa Smart House System na unaweza kutumika kwenye nyumba yoyote yenye umeme.

Mbali na kutumia makofi kuwasha na kuizima, unaweza kutumia simu ya mkononi hata ukiwa nje ya nyumba yako kufanya utakacho. Vilevile, unaweza kuzima vifaa mbalimbali vya nyumbani vinavyotumia umeme hata ukiwa mbali na nyumbani. Kwa kubonyeza simu yako ya mkononi, mfumo unakuruhusu kuendesha vifaa vyako vya nyumbani hata ukiwa nje ya nchi.

Mfumo huo unalenga kuboresha matumizi ya nishati hasa kupunguza gharama za nyumbani na kuwasaidia watu wasioona vizuri au walemavu wa macho kutumia vifaa vya kielektroniki walivyonavyo au wanavyotaka kuwa navyo nyumbani.

Mashine inayotumia chumvi

Mashine hii pia imebuniwa na Veta kwa mara ya kwanza ambayo inatumia maji na chumvi kupata umeme unaoweza kuchomelea vyuma kama vile mageti, milango na madirisha.

Mvumbuzi wa mashine hiyo kutoka mkoani Mara, Heri Maduhu anasema aliitengeneza kwa kutumia vifaa alivyoviokota baada ya kutupwa jalalani na kuchangia manufaa yake katika sekta ya viwanda .

“Badala ya kutumia umeme mwingi kufanya kazi mbalimbai za viwandani hasa vya kuunga na kutengeneza vyuma unaweza kutumia chumvi na maji tu na ukapunguza gharama za umeme,” anasema.

Mkono wa roboti

Katika maonyesho hayo pia kulikuwa na mhitimu wa kidato cha sita kutoka Sekondari ya Ilboru iliyopo Arusha, Gracious Fanuel ambaye alikuja na ubunifu wa mkono wa roboti unaotumia ishara, sauti na simu kujiendesha.

Mkono huo wa roboti una uwezo wa kuendeshwa kwa kutumia simu ya mkononi, ishara na sauti na unaweza kutembea kwenda mahala popote kuchukua kitu utakachoagizwa.

“Hii roboti imetengenezwa kwa kutumia mfumo ambao unaiwezesha kujiendesha yenyewe bila kutumia simu wala sauti au ishara. Ni suala la kuseti tu kulingana na mahitaji husika,” anasema mbunifu huyo.

Fanuel anasema mkono huo umebuniwa kwa ajili ya kuwasaidia watu wenye ulemavu na kufanikisha baadhi ya kazi za viwandani.

Kufukuza ndege

Katika maonyesho hayo kulikuwa na mtambo wa kufukuza wanyama na ndege wahalibifu wa mazao shambani. Mtambo huo una kengele inayotoa sauti ya tai na wanyama wengine hatari ili kuwatisha ndege na wanyama waharibifu pindi wanapoingia shambani.

Mtambo huo unatumia umemejua na unaweza kufungwa shambani na kutegesha aina ya mlio unaotakiwa kulingana na aina ya wanyama na ndege ambao wanashambulia mazao yaliyopo.

Mkufunzi wa Chuo cha Veta wilayani Mikumi ulikobuniwa mtambo huo, Ludovick Saronga anasema umetengenezwa kwa muundo wa ndege aina ya tai na una sauti za wanyama na ndege ambazo zinaogwa na nyani au kolekole ambao wanashambulia zaidi mazao.

“Tumebuni mtambo huu ili kuwasaidia wakulima kuvuna mazao mengi kwa sababu wengi hupata hasara kutokana na mazao yao kuliwa na ndege au wanyama waharibifu,” anasema.

Kw akutumia mtambo huo, mkulima anaokoa muda wa kulinda shamba hivyo kupata wasaa wa kufanya shughuli nyingine za uazalishaji.

“Tunawekeza zaidi kwenye viwanda ambavyo ili viweze kufanyakazi vinategemea sekta ya kilimo hivyo mtambo huu unalenga kuinua uchumi wa viwanda kwa kumsaidia mkulima kuzalisha kwa wingi,” anasema.

Mita ya maji

Ubunifu mwingine uliwavutia wananchi wengi ni mtambo wa kuchemsha chai na kuchota maji ya bomba kwa kutumia sarafu

Mashine hizi mbili zimebuniwa na Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT) ambazo zimelenga kuboresha teknolojia katika kutoa huduma mighahawani na wale wauzao maji.

Mhadhiri wa DIT idara ya komputa, Dk Daudi Simbeye anasema mashine ya kuchemsha chai inatumia umeme na mfumo wake wa kufanya kazi unategemea sarafu itakayowekwa.

“Hii ni maalumu kwa ajili ya hotelini au kwenye sherehe na mikutano. Inamwezesha mtu kujihudumia chai bila kushika kijiko, majani wala sukari. Ni suala la kuseti tu na chai inajichemsha yenyewe baada ya kudumbukiza sarafu ambayo ni sehemu ya malipo ya chai hiyo,” anasema.

Anafafanua kuwa mashine hiyo haiwezi kuchemsha wala kumimina chai kwenye kikombe bila kuweka sarafu sehemu husika.

Akizungumzia mashine inayochota maji maarufu kama mashine pesa anasema ina mfumo unaofanana na mashine y akuchemsha chai isipokuwa hii inatumika kwa wanaofanyabiashara ya maji.

“Kwa mfano, ukiwa na tanki na akatokea mteja anahitaji kuchota maji itamlazimu kudumbukiza sarafu kulingana na kiasi cha maji anayotaka kuchota. Mashine ina muziki pia hupigwa kila yatokapo maji kumburudisha mchotaji,” anasema.

Anasema mfumo huo walioutumia unalenga kubana matumizi lakini pia kudhibiti wizi hasa kwa wajasiriamali wanaouza maji na chakula hotelini hata kwa mama lishe.

Hatari

Chuo cha Veta pia kimekuja na ubunifu mwingine wa kifaa chenye uwezo kutoa taarifa za hatari zinazoweza kutokea nyumbabni mfano moto, mafuriko au uvamizi wa majambazi.

Mvumbuzi wa kifaa hicho, Best Eliabu anasema kinaweza kutoa taarifa pindi panapotokea viashiria vya hatari wa janga lolote.

Kifaa kinatoa taarifa kwa kupiga kelele pindi panapokuwa na kiashiria cha hatari au kupiga kwenye simu ya mkononi.

Anasema kifaa hicho kina simu mbili ambazo zimeunganishwa na simu ya nyumbani huku ya pili ikiunganishwa na ya mkononi.

“Ikitokea janga lolote muhusika atajulishwa kwa simu hizo mbili,” anasema.

Anasema kifaa hicho kinaweza kuunganishwa moja kwa moja na kitengo cha zimamoto ili likitokea janga kikajulishwa na kutoa maelekezo ilipo nyumba husika.

Eliabu anasema amebuni kifaa hicho kusaidia kukabiliana na majanga yanayoweza kuleta uharibifu nyumbani na viwandani.

Ingawa maonyesho yameisha, ni wakati muafaka wa wananchi kutumia ubunifu huu rahisi kufanikisha shughuli zao kulingana na mahitaji yaliyopo.

Kutoendeleza ubunifu ulioonyeshwa kwenye maonyesho hayo ni kuua vipaji vya wabunifu hivyo wadau na mamlaka husika zinapaswa kuweka mikakati ya kuhakikisha wananchi wananufaika kwa kuwekeza na kufikisha bidhaa husika kwa wananchi kwa ajili ya matumizi.

Chanzo: mwananchi.co.tz