Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Amos Makalla, amesema chanzo cha matukio ya moto yaliyotokea hvi karibuni katika masoko, yamesababishwa kwa asilimia kubwa na uzembe wa baadhi ya wafanyabiashara.
Sababu hizo zimetajwa leo Ijumaa na Makalla, wakati akifungua mkutano wa wafanyabiashara wadogo maarufu kama wamachinga, jijini Dar es Salaam.
Akitaja baadhi ya sababu hizo, Makalla amesema matukio hayo yalisababishwa na baadhi ya kina mama lishe kuwasha moto usiku kwa ajili ya kupika maharage, kuunganisha umeme kwa kutumia vishoka.
“Kwa taarifa za matukio hayo yote ya masoko niliyotaja, Kariakoo, Cocacola, Karume, Mbagala na TFF, ukiangalia vyanzo vya moto asilimia kubwa ni uzembe, asilimia kubwa haya matukio ya moto ni uzembe, nasema uzembe kwa sababu unaambiwa ni uunganishaji wa umeme kwamba pale Cocacola kuna mtu anawaunganishia umeme na wanachaji siku, ukapiga shoti, huo ni uzembe,” amesema Makalla.
Makalla amepiga marufuku vitendo vya uwashaji moto katika masoko, wakati wa usiku, pamoja na kujiunganishia umeme katika vibanda kwa kutumia vishoka.
“Nimesema moto wa kujitakia nimeshachoka, moto wa mtu kujiunganishia umeme, moto wa mtu kuinjika maharage ayakute asubuhi, hapana, hiyo ni ya kujitakia. Sijui unachajisha simu hiyo siitaki,” amesema Makalla.