Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Sababu za China kufanya uwekezaji mkubwa nchini

Uwekezaji Mkubwa China.jpeg Sababu za China kufanya uwekezaji mkubwa nchini

Sun, 30 Oct 2022 Chanzo: Mwananchi

Wakati Rais Samia Suluhu Hassan akitarajiwa kuzuru nchini China kwa ziara ya kitaifa ya siku tatu kuanzia Novemba 2, Kiongozi wa Taifa hilo anayesimamia masuala ya Afrika ameeleza sababu ya nchi yake kuwa mwekezaji namba moja Tanzania, huku akisema yajayo yanafurahisha. Kwa mujibu wa taarifa za Kituo cha Taifa cha Uwekezaji (TIC), China, ambayo ilikuwa ikishikilia nafasi ya pili tangu mwaka 2012 nyuma ya Uingereza, miaka mitatu iliyopita ilipindua meza na kuwa mwekezaji namba moja. Tangu kuingia madarakani kama Rais, Machi mwaka jana baada ya kifo cha Rais wa awamu ya tano, Rais Samia amekuwa akisisitiza juu ya hatua zake za kuifungua nchi kwa lengo la kuvutia uwekezaji kutoka nje ya nchi na kukuza biashara za ndani na kimataifa.

Mkurugenzi wa Idara inayoshughulikia masuala ya Afrika wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China, Wu Peng alisema siri ya mafanikio ni kuwa wananchi, wafanyabiashara na Serikali ya China wana imani na uchumi wa Tanzania na Afrika kwa siku zijazo.

“Hatuitazami Tanzania au mataifa ya Afrika kama nchi zinazoendelea au zinazohitaji kusaidiwa, hapana, tunalitazama bara la Afrika kama ukanda unaoweza kufanya biashara, hivyo tunaamini kesho ya Afrika ni ang’avu sana,” alisema.

Alisema siku zijazo Afrika inatarajiwa kuwa na mchango mkubwa na muhimu katika uchumi wa Dunia kutokana na wingi wake wa watu, rasilimali za asili, nguvu kazi inayojitoa na bunifu pamoja na soko kubwa.

“Hiyo ndiyo sababu China na wafanyabiashara wa China wanaamua kufanya uamuzi wa kuwekeza fedha zao Tanzania na Afrika kwa ujumla, licha ya kuwa wakati mwingine hata katika mazingira hatarishi kwa mitaji yao,” alisema Peng.

Hata hivyo, Peng alisema bado kuna changamoto ya nchi husika (Afrika kwa ujumla) kutengeneza mazingira ya biashara yanayovutia zaidi uwekezaji wa nje na hilo si kwa China tu, bali mataifa yote, wawekezaji wakubwa duniani waone Afrika ndiko sehemu sahihi ya kwenda kuwekeza.

“Ni muhimu kuzingatia hilo, mfano halisi ni China miaka ya 1990 pato la mtu mmoja mmoja lilikuwa chini ya dola 800 za Marekani na hapo ndipo tulichukua hatua ya kufungua nchi na kufanya mageuzi mengi katika sera zetu za uwekezaji,” alisema.

Ili kuvutia wawekezaji, alisema Serikali ilitoa vitu vingi na mahususi, ikiwemo ardhi ya bure na misamaha ya baadhi ya kodi na huduma mbalimbali.

“Mtu anaweza kudhani kuwa haikuwa hatua nzuri hiyo ama haiwezi kuleta matokeo chanya, lakini sasa uhalisia unatuambia namna hiyo inafanya kazi matokeo tumeyaona. Mfano ukimshawishi Toyota akaja nchini kwako na biashara yake ikaenda vizuri wenzake watakuja kama Honda na Volkswagen,” alisema Peng.

Alisema ukiwa na kampuni kubwa zinazotambulika duniani na biashara zake zikawa zinakwenda vizuri, huna haja ya kufanya matangazo ya kuwaita wawekezaji, wawekezaji wengine wakubwa watakuja wenyewe, watavutiwa na mafanikio ya mwenzao.

Alisema kampuni zote ama wawekezaji wote duniani lengo lao ni kutengeneza faida na mwisho wa siku sasa wote tunahimizana juu ya uwajibikaji kwa jamii. “Mara kwa mara tunawaeleza wawekezaji wa China wasifikirie tu kutunisha mifuko kupitia faida, bali kuwajibika kwa jamii ya nchi wanazofanyia shughuli zao.

“Tunaamini katika kuheshimiana na manufaa ya pande zote mbili na kama mazingira hayo yanaruhusu tunafanya biashara endelevu kwa manufaa ya wawekezaji nchi husika na watu wake, uhusiano wa China na Tanzania na kiuwekezaji kwa siku zijazo nauona ukiendelea kukuwa zaidi,” alisema Peng.

Alisema hatarajii kuwa uwekezaji wenyewe utakuwa ni mdogo wa kufungua tu mgahawa, bali uwekezaji mkubwa ambao unaleta matokeo chanya kwa watu kama viwanda na kilimo, ili wazawa katika nchi husika wapate ujuzi, kazi na kukidhi mahitaji yao.

Alisema anajua kuwa tayari kuna uwekezaji wa namna hiyo, akitolea mfano wa viwanda vya simu akisema licha ya kuwa yeye si mfanyabiashara, angependelea kuona uwekezaji wa namna hiyo, hivyo ana imani hata wafanyabiashara wa China watazingatia hilo.

Akizungumza uhusiano wa kiuchumi kati ya China na Tanzania, Balozi wa Tanzania nchini China, Mbelwa Kairuki alisema hali inazidi kuimarika.

Alisema China inaongoza kwa idadi kubwa ya mitaji ya nje iliyowekezwa nchini Tanzania, huku Taifa hilo la pili kwa uchumi duniani likiongoza pia katika orodha ya nchi ambazo zinafanya biashara na Tanzania.

“Hadi Oktoba, jumla ya miradi 1,098 yenye thamani ya dola bilioni 9.6 za Marekani ilisajiliwa katika Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) na miradi 15 yenye thamani ya dola milioni 202.1 ilisajiliwa Mamlaka ya Kukuza Uwekezaji Zanzibar (ZIPA),” alisema Kairuki.

Alisema kwa upande wa biashara, China imeendelea kuwa mojawapo ya nchi zinazoongoza kwa biashara na Tanzania. Katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita ujazo wa biashara kati ya China na Tanzania umeongezeka kwa kiasi kikubwa.

“Takwimu zinaonyesha hadi mwisho wa mwaka 2021 ujazo wa biashara kati ya China na Tanzania ulifikia dola bilioni 6.74 za Marekani. Muuzo ya bidhaa za Tanzania katika soko la China yameendelea kuongezeka na katika mwaka 2021 yalifikia dola milioni 600,” alisema.

Aidha, Mei 2019, Balozi Kairuki alinukuliwa na gazeti dada la The Citizen akisema mafanikio yaliyopatikana yanatokana na juhudi za Serikali na taasisi zake za kutangaza fursa za uwekezaji zinazopatikana nchini.

Chanzo: Mwananchi