Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Sababu za Bank M kuwekwa chini ya usimamizi wa BoT hizi hapa

9848 Pic+benk TanzaniaWeb

Fri, 3 Aug 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Taarifa za fedha za Benki M Tanzania Plc zinabainisha upungufu wa ukwasi uliosababisha Benki Kuu (BoT) kuiweka chini ya usimamizi wake.

Bank M ambayo ilikuwa ikitoa huduma kwa kampuni (corporate and investment bank) ilijikuta ikitoa kiwango kikubwa cha mikopo kuliko fedha zinazoingia kama amana au marejesho ya mikopo.

Taarifa za fedha za Bank M kwa kipindi cha Januari hadi Juni, zimebainisha jumla ya fedha zilitolewa kama mikopo zilikuwa zaidi ya amana na marejesho kwa asilimia 32.7.

Bank M katika taarifa hiyo iliyotolewa hivi karibuni inaonyesha jumla ya amana na marejesho ya mikopo hadi Juni ilikuwa Sh422.7 bilioni wakati fedha zilizotolewa kama mikopo zikiwa Sh628.4 bilioni.

Hesabu hizo zinaakisi sababu ya benki hiyo kuwekwa chini ya uangalizi wa BoT.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, gavana wa BoT, Florens Luoga alisema uamuzi huo umefikiwa kutokana na benki hiyo kuwa na ukwasi mdogo chini ya matakwa ya sheria ya benki na taasisi za kifedha ya mwaka 2006.

“Upungufu wa ukwasi ulioshuhudiwa katika benki hiyo unahatarisha usalama wa sekta ya fedha. Kuendelea kutoa huduma za kibenki kwa Benki M kunahatarisha amana za wateja wake, hivyo siku 90 kuanzia sasa benki hiyo itakuwa haitoi huduma,” alisema Profesa Luoga.

Alisema BoT imeisimamisha bodi ya wakurugenzi na uongozi wa Benki M, hivyo mamlaka hiyo ya juu ya usimamizi wa sekta ya fedha itakuwa ikifanya tathimini kusaidia kupata ufumbuzi wa suala hilo. Profesa Luoga alisema benki iliyo chini ya uangalizi wa BoT inaweza kujinasua iwapo wanahisa wataongeza mtaji kama ilivyofanya Kilimanjaro Community Bank Limited (KCBL).

Alisema benki iliyo chini ya uangalizi pia inaweza kuruhusiwa kuendelea na shughuli endapo wanahisa wataunganisha nguvu.

Gavana alisema hilo limefanyika kwa kuunganishwa Benki ya Wanawake (TWB) na Benki ya Posta (TPB).

Profesa Luoga alisema kwa kuwa chini ya BoT, inaendelea kuifanyia tathmini Benki M na kuangalia mwenendo wake ambao ukiridhisha inaweza kuruhusiwa kuendelea na shughuli zake.

Alisema hatua zinazochukuliwa na BoT hukusudia kulinda amana za wateja na ustawi wa sekta ya benki.

Gavana huyo alisema katika hatua za kurekebisha mwenendo wa benki zinaposhindikana, BoT hurudisha amana za wateja na kulipa madeni. Baada ya BoT kutoa taarifa ya kuiweka chini ya usimamizi wake Bank M, tawi lililopo Kisutu mlangoni liliwekwa tangazo likieleza kuwa imefungwa.

Mtumishi wa benki hiyo ambaye hakutaka jina lake litajwe gazetini alilieleza Mwananchi kuwa yupo njiapanda kuhusu ajira yake.

Benki zaunganishwa

Profesa Luoga pia alizungumzia kuunganishwa benki za TWB na TPB, huku ya KCBL na Benki ya Wananchi ya Tandahimba (Tacoba) zikiruhusiwa kuendelea na shughuli zake baada ya kuimarisha mtaji. Benki hizo zilikuwa chini ya uangalizi wa BoT kwa miezi zaidi ya sita kutokana na kuwa na kiwango kidogo cha ukwasi ambacho hakikukidhi matakwa ya sheria.

TWB imefuata njia ya Twiga Bancorp ambayo Mei 16 iliunganishwa na TPB. “Sambamba na mikakati ya Serikali ya kuboresha muundo wa benki za umma, wanahisa wenyewe ndio walioamua kuziunganisha benki hizo ili kuboresha utendaji. Baada ya muungano huo kutakuwa na benki moja ambayo itaendelea kuitwa TPB Bank Plc,” alisema.

Aliwaomba wateja wa TWB kuwa watulivu katika kipindi cha mpito cha uunganishwaji wa benki hizo na waendelee kupata huduma kulingana na utaratibu utakaotolewa na menejimenti ya TPB.

Kuhusu kurejea kwa huduma za Tacoba na KCBL, alisema benki hizo zimefikia kiwango kizuri kwa kuwa zimeweza kuongeza mtaji na kukidhi kiwango kinachohitajika kisheria.

Alisema Tacoba ilifanya juhudi za kujiimarisha kwa kufanya ushirika na CRDB na KCBL wanahisa wake waliongeza mtaji.

Chanzo: mwananchi.co.tz