Mchambuzi wa masuala ya kiuchumi, Gabriel Mwang'onda amesema kupaa kwa bei za vyakula nchini kumesababishwa na kufunguliwa kwa masoko nje ya nchi, jambo ambalo limeongeza ushindani sokoni.
Mwang'onda ameyasema hayo leo Jumatano, Desemba 28, 2022 wakati akiuchambua mwaka 2022 ulivyokuwa hasa kwenye sekta za kiuchumi kupitia Mwananchi Twitter Space.
Amesema kwa mara ya kwanza Taifa limeshubudia wakulima kuruhusiwa kuuza mazao yao nje ya nchi, jambo ambalo amesema limesababisha mfumuko wa bei kwenye vyakula.
"Leo hii ukienda kuuliza bei ya mchele ni gharama, lakini mchele umetuingizia fedha nyingi za kigeni. Kwa hiyo kufunguka huku kwa masoko kumeongeza ushindani sokoni," amesema Mwang'onda.
Amesisitiza sekta ya kilimo imekwenda vizuri na kwa mara ya kwanza Serikali imetenga zaidi ya Sh940 bilioni kwa ajili ya Wizara ya Kilimo.
Amesema sehemu ya fedha hizo zimeelekezwa kwenye kilimo cha umwagiliaji ambapo vitalu vimetengwa kwa ajili ya kuwezesha kilimo hicho.
"Tumeshuhudia utoaji wa ruzuku kwenye mbolea. Mbolea zilizokuwa zinanunuliwa Sh100,000 sasa zinauzwa Sh50,000. Pia, tumeshuhudia ujenzi wa vihenge," amesema Mwang'onda.