Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Sababu gharama kubwa za mbegu nchini zaanikwa

Mbeguuu Mbeguuu.png Sababu gharama kubwa za mbegu nchini zaanikwa

Tue, 15 Aug 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Taasisi ya Kudhibiti Ubora wa mbegu nchini (TOSCI) imesema gharama kubwa za bei ya mbegu zinatokana na kutokuwepo kwa sheria ya kudhibiti ubora.

Kauli hiyo imetolewa leo Jumanne Agosti 15, 2023 na Mkurugenzi Mkuu wa TOSCI Patrick Ngwediagi wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu utekelezaji wa utendaji katika shughuli za taasisi hiyo jijini hapa.

Amesema hakuna chombo chochote kilichopewa mamlaka ya kusimamia suala la mbegu lakini kwa sasa wanasheria wanakuna vichwa kuona namna gani wataliingiza hilo ili kuwasaidia wakulima.

“Serikali inaendelea kutafakari ili waingize vipengele ambavyo vitamfanya mkulima anufaike hususani kwenye bei za mbegu kwani Tanzania inadaiwa kuwa na aina 647 za mbegu,” amesema Ngwediagi.

Akizungumzia ubora wa mbegu amesema wamejitahidi kudhibiti madukani kwenye uingizwaji mbegu bandia licha ya ukweli bado kuna wachache wanaofanya hivyo na siku za hivi karibuni waliwakamata watu watano na kuwapeleka mahakamani ambao TOSCI ilishinda kesi.

Mwenyekiti wa Jukwaa la wakulima wanawake wilaya ya Chamwino, Janeth Nyamayahasi amesema bado kuna kilio kikubwa kuhusu gharama kubwa za kununua mbegu.

Nyamayahasi ametaja changamoto hizo ni mbegu kupatikana maduka ya mijini pekee ambako wakulima wadogo hawawezi kufika kwa urahisi lakini gharama zake ni kubwa.

“Kingine ni umbali wa kufikiwa, kumbuka mkulima mwenye shamba linalohitaji kilo tatu anaweza kuzifikia mbegu hizo mjini kwa kutumia nauli kubwa wakati wangeweza kuweka mawakala wao hadi vijijini wakatuuzia,” amesema Nyamayahasi.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live