Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Sababu diaspora wa Tanzania kutuma fedha kidogo nyumbani

FEDHA Sababu diaspora wa Tanzania kutuma fedha kidogo nyumbani

Thu, 15 Feb 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Ripoti ya Benki ya Dunia (WB) inaitaja Tanzania kuwa nchi ya pili kutoka mwisho ndani ya Afrika Mashariki katika upokeaji wa fedha nyingi kutoka kwa raia wake wanaoshi nje (diaspora).

Ripoti hiyo inayoakisi mwaka 2023 inaonyesha Tanzania ilipokea takribani Sh829 bilioni kutoka kwa watu wake wanaoishi nje ikiwa imeitangulia Burundi iliyopokea wastani wa Sh12 bilioni.

Uwapo wa kiwango hicho kidogo kinatajwa kuchangiwa na kukosekana kutambuliwa rasmi kwa Watanzania wanaoishi nje.

Fedha zilizopokewa mwaka 2023 zilikuwa pungufu ikilinganishwa na Sh1.007 trilioni zilizokuwapo mwaka 2017.

Ndani ya nchi za Afrika Mashariki, Kenya inaongoza.

Kwa mwaka 2023 pekee watu wake walipokea zaidi ya Sh10.53 trilioni kutoka kwa diaspora, ikifuatiwa na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) iliyokuwa na Sh3.50 trilioni.

Akizungumza, Mkurugenzi wa Tanzania Diaspora, Kelvin Nyamori amesema mabalozi wengi wanaoiwakilisha Tanzania walikuwa hawajui ni watu wangapi kutoka nchini waliopo katika kituo chake cha kazi, jambo lililofanya hata uhamasishaji kuwa mgumu.

Kutokana na hilo, diaspora kwa kushirikiana na Wizara ya Mambo ya Nje walikuja na mfumo utakaowawezesha wao kujisajili katika sehemu walipo.

“Hii inasaidia kwa sababu wengi walikuwa wakienda nje hawasajiliwi katika ofisi za mabalozi na balozi hajui, kwa sasa wako kati ya 300,000 hadi 400,000 lakini tunaamini wanaweza kuwa zaidi ya hapo,” amesema.

Jambo lingine linalofanya kuwapo kwa kiwango kidogo cha fedha zinazorudi nchini ni kukosekana akaunti maalumu ya wao kutuma fedha nchini kwa ajili ya kuchangia uchumi wa nchi.

“Nchi kama Kenya, wao wana akaunti maalumu katika benki za nchi zao zinazopokea fedha kwa ajili ya kuchangia uchumi mbali na zile walizotuma kwa ndugu zao,” amesema Nyamori.

Kutokana na hilo, ametaka kuanzishwa akaunti maalumu kupitia Wizara ya Fedha na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ili Watanzania waishio nje waweze kuitumia kuchangia uchumi.

Hata hivyo, ripoti ya WB inakinzana na ile ya BoT inayoonyesha kiwango cha fedha kilichopokewa kutoka nje mwaka 2022 kilikuwa Sh1.344 trilioni tofauti na Sh815 bilioni zilizotajwa na WB kwa mwaka huo.

Mtanzania mwingine anayeishi nje, Masoud Hassan Maftah amesema wakati mwingine changamoto wanazokabiliana nazo katika benki zimekuwa zikiwakatisha tamaa ya kutuma fedha nchini.

Akitoa mfano wa kilichotokea kwake wakati akituma fedha kutoka Marekani siku chache nyuma, amesema hukosa nafasi ya kuandika neno ‘Limited’ badala yake akaandika ‘LTD’ mbele ya benki husika kunaifanya fedha hizo zisipokewe na benki, badala yake zilirudishwa nchi aliyokuwa.

“Ilinilazimu kumpigia mkurugenzi wa benki husika akanisaidia, huyo ni mimi namjua kiongozi, vipi kuhusu wengine, inakatisha tamaa,” amesema Maftah.

Akizungumzia uwepo wa akaunti maalumu, Gavana wa BoT, Emmanuel Tutuba amesema tayari jitihada zimefanyika, ikiwamo kulegeza masharti ya ufunguaji wa akaunti kwa Watanzania wanaoishi nje.

Amesema kwa sasa Watanzania hao wanahitajika kuwa na kitambulisho chochote au pasi ya kusafiria ili kuwa na akaunti inayowapa haki ya kufanya uwekezaji ikiwamo kununua hatifungani za Serikali.

“Lakini kwa nini kiwango cha fedha kinachotumwa ni kidogo, Watanzania wengi wanaoishi nje kiwango cha fedha wanachopata hakiwatoshi kutuma nyingine nyumbani kwa kiwango kikubwa,” amesema Tutuba.

Ametaja sababu nyingine kuwa ni idadi ndogo ya watu waishio nje ya nchi ikilinganishwa na mataifa mengine.

Diaspora mwingine, Ester Kroll ametaja njia nyingine inayoweza kutumiwa na nchi ili kuongeza ushiriki wa Watanzania katika uchumi ni kutumia ujuzi walionao kwa sababu wapo wanaofanya shughuli nje ambazo zinaweza kuleta manufaa kwa nchi ikiwemo kuvutia uwekezaji wa kigeni.

“Uongozi wa sasa ni mzuri umefungua mahusiano ya diplomasia ya uchumi itamfanya Mtanzania yeyote aliye nje ya nchi kusaidia kukua kwa uchumi ikiwamo kuleta wawekezaji,” amesema Kroll.

Suala la ujuzi liliungwa mkono na Nyamori, ambaye ameeleza watu wanaoishi nje wana uwanja mpana katika kuchangia uchumi bila kuangalia namna wanavyotuma fedha, bali kwa kutumia vitu walivyonavyo kama vile ujuzi.

“Watanzania walioko nje wana utaalamu wa aina mbalimbali, Serikali ikiweza kuwasiliana nao tunaweza kutumia walichonacho, kama ni wataalamu wa magonjwa mbalimbali, madaktari, wahandisi, watumike vizuri,” amesema Nyamori.

Namna nyingine ya kuongeza ushiriki wa Watanzania, amesema wanafikiria kuanzisha tuzo maalumu kuwatambua mabalozi wanaohamasisha zaidi Watanzania wanaoishi nje kurudi kuwekeza Tanzania.

“Tuwashindanishe mabalozi, kwa kile wanachokifanya ikiwemo kuhamasisha Watanzania kurudi kuwekeza nchini, tuwatambue na michango yao katika uchumi wa nchi ionekane,” amesema.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live