Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Sababu TRC kuvunja mkataba na kampuni ya Eurowagon

Trc Pic Data Sababu TRC kuvunja mkataba na kampuni ya Eurowagon

Thu, 16 Jun 2022 Chanzo: www.mwananchi.co.tz

Shirika la Reli Tanzania (TRC) limevunja mkataba na kampuni ya Eurowagon ya nchini Uturuki baada ya kushindwa kukamilisha ujenzi wa vichwa viwili vya treni ya umeme na mabehewa 30 ya abiria.

Kwa mujibu wa mkataba huo, vifaa hivyo vilitakiwa kukamilika Novemba 2021 lakini kwa kuwa Eurowagon ilishindwa kutimiza matakwa ya mkataba na kipande cha kwanza Dar es Salaam mpaka Morogoro kikiwa hatua ya mwisho ya ujenzi, TRC ilisitisha mkataba huo Februari 25,2022.

Hayo yamesemwa leo Jumatano Juni 15, 2022 na mkuu wa kitengo cha uhusiano TRC, Jamila Mbarouk wakati akitoa taarifa ya vyombo vya habari kuhusu hatua mbalimbali zinazoendelea katika ujenzi wa reli ya kisasa SGR.

Amesema vifaa hivyo vya majaribio vilitakiwa kukamilika mapema katika kuhakikisha uendeshaji wa awali unaanza baada ya majaribio mara baada ya ujenzi kukamilika.

“TRC ilisaini mkataba wa  vifaa vichache wa muda mfupi wa ununuzi wa vichwa vya treni ya umeme viwili na behewa 30 za abiria vitakavyofanyiwa ukarabati kutoka kampuni ya Eurowagon ya nchini Uturuki."

“Vifaa vilitakiwa kukamilika Novemba mwaka jana, TRC iliamua kusitisha mkataba na kuwajulisha kwa barua Februari 25, 2025 na iliendelea na jukumu la kumalizia ukarabati bila gharama na vifaa vinatarajiwa kukamilika ifikapo Agosti mwaka huu,” amesema Jamila.

Advertisement Amesisitiza kuwa TRC haina mgogoro wa kimapato na kampuni ya Eurowagon kwani ilitimiza matakwa ya kimkataba ya kulipa asilimia 35 na kwa kutimiza masharti ya umiliki wa vichwa vya treni vya umeme viwili na behewa 30 vilishahamia kwa TRC.

“Mkataba unatoa haki kwa TRC kuchukua majukumu ya kumalizia ukarabati mara pale mzabuni anaposhindwa kutimiza masharti ya mkataba,” amesema Jamila.

Kaimu mkurugenzi miundombinu ya reli,  Machibya Masanja akizungumzia mkwamo uliopo sasa amesema uchelewaji wa mabehewa ya abiria pamoja na vichwa vya treni vipya umetokana na athari za Uviko19.

“Sisi si kisiwa tunahusiana na nchi nyingine mabehewa yanakozalishwa kumekuwa na changamoto na athari mojawapo ilienda kwenye uzalishaji wa mabehewa, juhudi mbalimbali zinafanyika kuwasiliana na mzabuni ili kufikia Agosti mabehewa hayo yawe yamewasili nchini,” amesema Masanja.

Wakati ujenzi ukiendelea TRC inafanya manunuzi ya behewa za mizigo, behewa za abiria, seti za treni za kisasa na vichwa vya treni ya umeme.

Shirika hilo lilisaini mikataba ya manunuzi ya behewa mpya 1430 ya mizigo kutoka kampuni ya CRRC ya nchini China, behewa mpya za abiria 59 kutoka kampuni ya Sung Shin Rolling Stock Technology Limited ya Korea Kusini, seti 10 mpya za treni za kisasa zenye  behewa 80 na vichwa 17 vya umeme vipya kutoka Hyundai Rotem ya Korea Kusini vyenye thamani ya Sh1.18 Trilioni.

Chanzo: www.mwananchi.co.tz