Shirika la Madini la Taifa (Stamico) limetangaza mradi wa mkaa mbadala unaotarajiwa kutoa suluhisho la kitaifa na kimataifa katika utunzaji wa mazingira.
Pia, limebainisha baadhi ya mafanikio lililopata ndani ya miaka hiyo 50 ikiwamo kuanza kujiendesha kibiashara kwa kuwa sehemu ya kuanzishwa kwa kiwanda cha kwanza cha uchenjuaji wa dhahabu.
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Stamico, Dk Venance Mwasse alisema hayo Dar es Salaam alipozungumza na waandishi wa habari kuhusu maandalizi ya maadhimisho ya miaka 50 tangu kuanzishwa kwa shirika hilo yatakayofanyika Agosti 12, mwaka huu jijini Dodoma.
Dk Mwasse alisema Stamico lilibuni mkaa huo unaoitwa Rafiki Briquettes baada ya kubaini Watanzania wengi wanatumia mkaa na kuni kupikia, hali inayosababisha uharibifu mkubwa wa mazingira kwa kukata miti.
Alisema kwa kushirikiana na Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (Costech), Shirika la Utafiti wa Maendeleo ya Viwanda (TIRDO) na vyuo vikuu nchini, waliufanyia utafiti mkaa huo tangu mwaka 2018 na kujiridhisha kuwa unafaa kwa matumizi baada ya kuidhinishwa na Shirika la Viwango Tanzania (TBS).
“Yote haya tumelenga kuunga mkono juhudi za Rais Samia Suluhu Hassan na juhudi za kimataifa katika kutunza mazingira na kupambana na uharibifu wa mabadiliko ya tabianchi,” alisema Dk Mwasse.
Alisema shirika hilo limeagiza mitambo minne ya kuzalishia mkaa huo itakayokuwa inazalisha kilogramu 20 kwa saa itakayosambazwa mkoani Pwani, Mgodi wa Makaa ya Mawe Kiwira, Mwanza na Dodoma. Dk Mwasse alisema mkaa huo utakaozalishwa kutokana na mabaki ya makaa ya mawe na Maranda utauzwa kwa bei nafuu ambayo Mtanzania wa kawaida ataimudu na tayari umeanza kuvutia soko la nje zikiwamo nchi za Oman na Umoja wa Falme za Kiarabu.
Alisema ndani ya miaka hiyo 50 shirika hilo sasa linajivumia mkaa huo kuwa utaingizia shirika hilo mapato na taifa fedha za kigeni.
Aidha, alitaja mafanikio mengine kuwa shirika hilo sasa linajivunia kujiendesha kibiashara na limejipanga kuwekeza zaidi kwenye sekta ya madini katika maeneo ya kuchimba, kuchenjua na kufanya biashara ili Watanzania wanufaike na madini yao kupitia Stamico.
Katika kuadhimisha miaka hiyo, wameandaa jarida kuelezea historia ya mafanikio, kushiriki kupanda miti takribani 10,000 Ipagala Dodoma itakayotunzwa na Stamico, kuzindua mkaa huo mbadala, kutoa vifaa vya uchimbaji kwa wachimbaji wadogo wenye usikivu hafifu na kutembelea wagonjwa katika Hospitali ya Ocean Road, Dar es Salaam.
Alisema siku ya upandaji miti itazinduliwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Dk Selemani Jafo.