Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

STAMICO yasaini mkataba mradi mkubwa wa shaba Kilimanjaro

WhatsApp Image 2021 12 04 At 14.50.36 660x400.jpeg STAMICO yasaini mkataba mradi mkubwa wa shaba Kilimanjaro

Sat, 4 Dec 2021 Chanzo: millardayo.com

Shirika la Taifa la Madini (STAMICO) limesaini mkataba wa makubaliano ya awali na Kampuni ya Suness Limited ya Italia kwa ajili ya kuendeleza mradi mkubwa wa Shaba katika Mkoa Kilimanjaro. Suness Limited ni kampuni ya Kiitaliano inayojishughulisha na uchimbaji madini na Kampuni hiyo imeonesha utayari wa kushirikiana na STAMICO katika kuendeleza kwa pamoja mradi wa shaba.

Akiongea mara baada ya kusaini mkataba huo leo jijini Roma Italia, Mkurugenzi Mtendaji wa STAMICO Dkt. Venance Mwasse amesema kuwa mkataba umesainiwa kupitia jukwaa la biashara na uwekezaji lililofanyika Jijini Roma Italia tarehe 02 – 03 Disemba 2021.

Pamoja na mambo mengine, STAMICO wameweza kuelezea juu ya mradi wa mkubwa wa shaba unaopatikana katika Mkoa wa Kilimanjaro ambapo pia mwekezaji ameonesha nia ya kuingia ubia na STAMICO.

“Shirika lina mradi wake mkubwa wa Shaba mkoani Kilimanjaro wenye kiasi kikubwa cha mashapu ya Shaba na kupitia jukwa la wafanyabiashara na uwekezaji lililofanyika Roma Italia, tumewaeleza juu ya mradi huo na wenzetu wameonesha kuvutiwa na mradi huo na tukakubaliana kusaini makubaliano ya awali na baadae watakuja Tanzania ili kwa pamoja twende kwenye eneo la mradi husika na mwishowe tuingie katika makubaliano ya pamoja ya kuendeleza mradi huo,” Dkt. Mwasse

Naye Rais wa Kampuni ya Sunless Bw. Sandro Calo amesema kuwa amefurahishwa na utiaji saini wa awali wa mkataba wa makubaliano kwa ajili ya kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika kuendeleza kwa pamoja mradi wa Shaba

“Nimefurahia kuanza kwa makubaliano haya mapya ambayo yataleja matokeo chanya kati ya nchi ya Tanzania na Italia na naahidi kuendeleza ushirikiano huu kwa maslahi mapana ya pande zote mbili katika sekta hii ya madini,” Calo.

Utiaji saini wa makubaliano hayo umeshuhudiwa na Naibu Waziri, Wizara ya Madini Prof. Shukrani Manya, Balozi wa Tanzania Nchini Italia, Mhe. Mahmoud Thabiti Kombo, Mkurugenzi Idara ya Diplomasia ya Uchumi katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Edwin Rutageruka pamoja na Mkurugenzi wa Kampuni ya Utalii ya Zanzibar Classic Safaris, Bw. Yussuf Salim Njama.

RAIS SAMIA AWAVAA WASALITI, AWAONDOA WENYE VITI WA BODI “WATU WA HOVYO, ETI UFISADI AWAMU YANGU”

Chanzo: millardayo.com