Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

SMZ yapata gawio bil 27/- kuratibu uchumi

37cf7b1c427fe767b9e49be3881218fe SMZ yapata gawio bil 27/- kuratibu uchumi

Thu, 28 Apr 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Serikali ya Zanzibar imepelekewa mgawo wa Sh 27,038,498,469.01 kwa ajili ya kuratibu masuala ya kiuchumi na kijamii.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Dk Selemani Jafo alisema hayo jana bungeni Dodoma wakati akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya wizara yake kwa mwaka wa fedha 2022/2023.

Akielezea kazi zilizofanyika kwa mwaka wa fedha 2021/22 kwa upande wa Muungano, Dk Jafo alisema ofisi hiyo imeratibu gawio la Serikali ya Zanzibar, ambapo hadi Machi, 2022, Sh 27,038,498,469.01 zimepelekwa Serikali ya Zanzibar.

Alisema katika fedha hizo, Sh bilioni 1.4 ni fedha za Mfuko wa Kuchochea Maendeleo ya Jimbo Zanzibar na zaidi ya Sh bilioni 13.319 ni fedha za mapato ya Paye.

Jafo alisema pia Sh bilioni 2.348 ni fedha za misaada kutoka nje (GBS), Sh bilioni 9 ni gawio la faida ya Benki Kuu na Sh milioni 971.469 ni gawio la miamala ya simu.

Kuhusu Fedha za Mfuko wa Kuchochea Maendeleo ya Jimbo, Zanzibar, Jafo alisema zimeendelea kutolewa katika majimbo yote Tanzania Bara na Zanzibar kila mwaka kwa ajili ya kuchochea maendeleo.

"Ofisi ya Makamu wa Rais ilifanya ufuatiliaji wa utekelezaji wa miradi inayotekelezwa kwa kutumia fedha hizo mwezi Machi, 2022 kwa lengo la kubaini mafanikio na changamoto za utekelezaji na kushauri namna ya kukabiliana nazo," alisema Dk Jafo na kuongeza:

"Katika ufuatiliaji huo imebainika kuwa fedha hizo zimesaidia kuibua na kutekelezwa kwa miradi ya kijamii ikiwamo maji, afya, elimu na umeme ambayo imewanufaisha wananchi wa majimbo husika.”

Dk Jafo alisema pia serikali imeendelea kuwawezesha wananchi wa pande zote mbili za Muungano kushiriki katika shughuli za kiuchumi na kijamii kupitia utekelezaji wa miradi na programu za maendeleo.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live