Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

SMZ yaagiza kasi kilimo cha viungo

4b23f2ed2fc5a4361b1dfdabddd0ecd9 SMZ yaagiza kasi kilimo cha viungo

Sat, 13 Mar 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar imewataka wakulima nchini kuongeza kasi ya kulima mazao ya viungo ambayo hivi sasa soko lake nje ya nchi ni kubwa na lenye uhakika litakaloingiza kipato na kuwakomboa wakulima kimaisha.

Hayo yalisemwa na Waziri wa Kilimo Umwagiliaji, Maji, Maliasili na Mifugo, Soud Nahoda Hassan wakati alipowatembelea wakulima wa mazao ya viungo Kizimbani.

Alisema lengo na mikakati ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ni kujitosheleza kwa chakula na kuwa mazao ya viungo yamepewa kipaumbele kwa ajili ya kuingiza pato kwa wakulima na kusafirisha nje ya nchi.

Aliyataja mazao ya viungo ambayo hivi sasa soko lake lipo la uhakika nje ya nchi kuwa ni vanila, pilipili manga, pilipili hoho, uzile na hiliki.

“Ujumbe wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa wakulima wetu wajikite katika uzalishaji wa mazao ya viungo ambayo soko lake nje ya nchi nje lipo la uhakika,” alisema.

Hassan alisema kituo cha utafiti wa mazao ya kilimo cha Kizimbani tayari kimepewa kazi ya kutoa elimu na mafunzo kwa mabibi shamba na mabwana shamba kwa ajili ya matayarisho ya mazao ya uzalishaji wa mazao ya viungo.

Katibu Mkuu Wizara ya Biashara na Maendeleo ya Viwanda Dk Islam Seif alisema soko la mazao ya viungo katika nchi za Ulaya, Asia na Bara Hindi ni la uhakika na kuwataka wakulima kuongeza bidii katika kilimo hicho.

Alisema mahitaji ya viungo katika nchi za nje hasa Bara Hindi na Asia ni makubwa na kuwa hadi sasa bado wakulima wa ndani hawajaonesha uwezo wa kukidhi mahitaji ya soko hilo.

“Wizara ya Biashara Viwanda wito wetu kwa wakulima wa ndani waongeze uzalishaji wa mazao ya viungo ambayo soko lake nje ya nchi ni kubwa na la uhakika,” alisema.

Meneja wa Mradi wa viungo ambao unafadhiliwa na Jumuiya ya Ulaya (EU) kutoka katika taasisi ya Jukwaa la (PDF) kutoka Tanzania Bara, Jorum Kizito aliwataka wakulima kuelekeza nguvu zao katika kilimo cha mazao ya viungo na mboga mboga ambacho soko lake lipo la uhakika.

Alisema mradi wa viungo umelenga kuwanufaisha jumla ya wakulima 21,000 wa Unguja na Pemba huku ukilenga kuwainua zaidi ya wanawake asilimia 55 kiuchumi.

“Huu ni mradi mkubwa ambao umelenga kuwakomboa wanawake kiuchumi na kupiga hatua kubwa ya maendeleo ya kiuchumi,” alisema.

Zanzibar katika miaka ya 1950 ilikuwa maarufu kwa uzalishaji wa mazao ya viungo na kusafirisha nje ya nchi ikiwemo pilipili manga, mbata pamoja na uzile na hiliki na inaongoza kwa usafirishaji wa zao la karafuu.

Chanzo: www.habarileo.co.tz