Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

SIDO yatengeneza ajira 500,000

A01e14b566a950397ee4f2743b8fa85a SIDO yatengeneza ajira 500,000

Thu, 13 Aug 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

KATIKA miaka mitano iliyopita, Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO) limesimamia ujenzi wa viwanda 8,477 vilivyotengeneza fursa za ajira 500,000, hivyo kuchangia kukua kwa Pato la Taifa na kuifanya Tanzania kuwa taifa lenye uchumi wa kati.

Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Mkuu wa SIDO, Profesa Sylvester Mpanduji katika mahojiano maalumu jijini Dar es Salaam kuhusu uhusiano wa kufikiwa uchumi wa kati na mchango wa SIDO kuiwezesha nchi kupata mafanikio hayo

Alisema kuwa uchumi huo umefungamana na kuwepo viwanda na kwamba shirika hilo limetekeleza kwa vitendo sera ya kuanzishwa kwa viwanda. “Tumepata viwanda vikubwa 201, viwanda vya kati 460, viwanda vidogo 3,406 na viwanda vidogo sana 4,410 vimeanzishwa katika kipindi cha Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais John Magufuli na kuliwezesha shirika kufikia asilimia 98 ya malengo yetu,” alisema Profesa Mpanduji.

Alisema kuwa SIDO inawahamasisha wazalishaji wa ndani, kuzalisha bidhaa zenye ubora ili Watanzania wapende kuzinunua. “Mteja anapenda kupata bidhaa bora kulingana na fedha yake.

Hivyo ili viwanda viendelee kuwepo lazima ubora wa bidhaa uimarishwe ili kujenga imani ya wateja katika soko la ndani na hatua ya pili ni kuibua fursa ya kupata masoko ya nje ya nchi,” alisema Profesa Mpanduji.

Alisema kuwa ajira nyingi zimezalishwa na viwanda vidogo sana na viwanda vidogo na kufafanua kuwa mwaka jana sekta ya viwanda ilichangia asilimia 8.5 katika Pato la Taifa.

“Uwekezaji katika sekta ya viwanda hususani viwanda vidogo nchini, umeongeza uzalishaji wa bidhaa mbalimbali ikiwemo bidhaa za nguo na mavazi, ngozi na bidhaa za ngozi, kusindika nyama, chakula, mboga na matunda, maziwa, mafuta ya kula, sukari, vifungashio, mbolea na viwanda vya kubangua korosho,” alisema Profesa Mpanduji.

Alieleza kuwa katika kipindi cha mlipuko wa ugonjwa wa Covid-19, SIDO ilihakikisha viwanda vinazalisha vifaa vya kujikinga na ugonjwa huo ikiwemo utengenezaji wa barakoa na vifaa vya kujikinga.

“Vita dhidi ya corona imekuwa rahisi kutokana na kuwepo kwa viwanda vyenye uwezo ndani ya nchi na upatikanaji wa bidhaa mbali mbali.

Hali hii imepunguza utegemezi wa bidhaa kutoka nje ya nchi,” alisema

Chanzo: habarileo.co.tz