Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

SHIRECU yatenga bil 9.6/- kununua mazao, kufufua kiwanda

483ec80b08e185093bb443e6e818f7c9 SHIRECU yatenga bil 9.6/- kununua mazao, kufufua kiwanda

Mon, 4 Apr 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Chama kikuu cha Ushirika Shinyanga (SHIRECU 1984 LTD) kimetenga Sh bilioni 9.6 kwa ajili ya kununua zao la pamba kutoka kwa wakili na mazao mchanganyiko katika msimu ujao wa mavuno ili kuwainua wakulima kiuchumi.

Sambamba na hilo, sehemu ya pesa hizo itatumika kufufua kiwanda kimoja cha kuchambua zao la pamba cha Mhunze.

Kaimu Meneja wa Shirecu, Sebastian Max alisema juzi wakati wa mkutano mkuu wa 27 wa chama hicho kuwa lengo kuu la kutenga kiasi hicho cha fedha ni kunyanyua ushirika ambao ni mkombozi wa mkulima na kuhakikisha mkulima anapata malipo stahiki.

Alifafanua kwamba Sh billioni 6.1 ni kwa ajili ya kufufua kiwanda na Sh bilioni 3.5 kununua mazao, hatua itakayorudisha heshima ya mkoa kwa upande wa kilimo.

Kwa mujibu wa Max, toka soko huria la ununuzi wa mazao lilipoanza wakulima wengi walikimbilia kwa wanunuzi binafsi ambapo baadhi wamekuwa wakipunjwa, hivyo maboresho kwenye chama yataondoa changamoto hiyo.

Ili kufanikisha hilo, Kaimu Meneja huyo alisema semina kwa viongozi wa AMCOS itafanyika kabla ya msimu kuanza ili wawaelimishe wakulima jinsi ya kunufaika na mazao yao hususani pamba.

Kwa upande wake, Meneja wa Bodi ya Pamba Kanda ya Magharibi, Joanes Bwahama, alisema msimu huu bodi imeshagawa mbegu zaidi ya kilo 16,000 na chupa za dawa ya kuua wadudu wa zao hilo milioni nane ili kukuhakikisha pembejeo zinapatikana kwa wakati.

"Tayari asilimia 80 ya wakulima tumeifikia katika kanda ambapo tayari chupa zaidi ya milioni 6.7 zimesambazwa," alisema.

Aliwataka wanufaika na wasambazaji wa dawa hizo kutumia pembejeo hizo kwa makusudi yaliyopangwa, kwani serikali inafuatilia kwa karibu na kumchukulia hatua za kisheria yeyote atakayebainika kwenda kinyume na taratibu zilizowekwa.

Mmoja wa wanachama wa chama cha msingi cha ushirika Mwalukwa (Amcos), Mhoja Musa, alisema chama kinataka zao la pamba lirudishe heshima kama zamani na wapo viongozi wenye ubunifu, wanaotoa elimu ya mara kwa mara kwa wakulima ili uzalishaji uwe wa tija.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live