Shirika la Reli Tanzania (TRC) limesema utekelezaji wa mradi wa mkakati wa ujenzi mtandao mpya wa reli ya kisasa (SGR) utakuwa na manufaa ya kiuchumi kwa Tanzania kwa kuiwezesha kukuza biashara na nchi jirani.
Kwa kutumia SGR Tanzania itakuwa kitovu cha sekta ya usafirishaji na kufungua milango ya biashara na nchi jirani za Rwanda, Burundi, DRC, Uganda na Kenya.
Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika kipindi cha miaka mitano, imeelekeza serikali iendelee kuwekeza katika miundombinu ya kimkakati ya reli.
Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa miaka mitano (2021/2022-2025/2026) unaelekeza uboreshaji na uendelezaji wa miundombinu ya reli kwa lengo la kurahisisha shughuli za kiuchumi zikiwemo za kukuza biashara ndani na nje ya nchi kwa kuunganisha mikoa ya Dar es Salaam, Mwanza, Kigoma, Katavi na nchi zinazokuwa na bandari za Rwanda, Burundi, DRC na Uganda.
Pia unaelekeza ukamilishaji wa ujenzi mtandao wa SGR yenye urefu wa kilomita 1,219 kwa lengo la kuongeza kiwango cha usafirishaji wa shehena za mizigo hadi kufikia tani milioni 2.2 na usafirishaji wa abiria hadi kufikia watu milioni 2.3.
Ushiriki wa Watanzania
Mkurugenzi Mkuu wa TRC, Masanja Kadogosa alisema kwa kazi ambazo hazihitaji utaalamu wa hali ya juu, mkataba ulitaka asilimia 80 wawe Watanzania na asilimia 20 wageni, lakini mpaka sasa zaidi ya asilimia 90 ni Watanzania na wageni wako kati ya asilimia 6 hadi 8.
Kadogosa alisema kwa wataalamu wabobezi (wahandisi na mafundi) mkataba ulitaka asilimia 80 watoke nje na asilimia 20 wawe Watanzania na katika utekelezaji kati ya asilimia 48 hadi 50 ya wataalamu walikuwa ni Watanzania.
"Hiki ni kitu kizuri hususani katika suala zima la kuhamisha ujuzi, vijana wengi wahandisi wa Kitanzania wameshiriki kwenye miradi hii. Hili limewastaajabisha sana, baada ya kukuta kuna vijana wenye ujuzi na ambao ni rahisi kufundishika, walikuwa na uhakika hata hiyo asilimia 20 isingeweza kufikiwa," alisema.
Kadogosa alisema katika ajira Watanzania zaidi ya 16,000 wameajiriwa katika utekelezaji wa mradi wa vipande viwili na ukichanganya na kwa kipande cha Mwanza kinafanya jumla ya walioajiriwa kufikia jumla ya Watanzania 20,000.
Alisema kwa upande wa fursa, kampuni takribani 1,600 za Kitanzania zinashiriki kufanya kazi zikiwemo za kutoa huduma na ujenzi.
Awamu ya kwanza
Kadogosa alisema awamu ya kwanza ya mtandao wa reli ukanda wa kati kuanzia Dar es Salaam hadi Mwanza (km 1,219) unatekelezwa kwa vipande vitano kwa gharama ya Sh trilioni 16.6 ikijumuisha kodi ya ongezeko la thamani (VAT) huku wakandarasi wakiwa eneo la mradi wakiwa wamelipwa Sh trilioni 6.4.
Alisema hadi Juni mwaka huu, kipande cha Dar es Salaam- Morogoro (km 300) ujenzi wake umefikia asilimia 97.19 wakati kipande cha Morogoro-Makutupora (km 422) ujenzi umefikia asilimia 87.05.
Kadogosa alisema kipande cha Makutupora-Tabora (km 368) kazi za awali na usanifu wa kina wa njia unaendelea huku Shirika likisaini mkataba wa ujenzi wa kipande cha Tabora- Isaka (km 165). Vipande vyote vinajengwa na mkandarasi Yapi Merkezi kutoka Uturuki.
Pia kipande cha Isaka- Mwanza chenye urefu wa kilomita 341 ujenzi wake umefikia zaidi ya asilimia 9 na kinajengwa na mkandarasa, kampuni ya China Civil Engineering Construction (CCEC) na China Railway Construction Corporation (CRCC).
"Mradi huu umelenga kuhudumia kanda ya kati na soko kubwa la Uganda. Kwa Kampala pekee mizigo inayoenda ni zaidi ya tani milioni 7 lakini sisi tunapata chini ya asilimia 2 kutokana na kutokuwa na miundombinu ya uhakika ya kusafirisha," alisema Kadogosa na kuongeza:
"Na hii ndio maana ya azma ya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan ya kufungua nchi, hivyo ni lazima tujipange kibiashara."
Awamu ya pili
Kadogosa alisema awamu ya pili inahusu ujenzi wa mtandao wa reli ya Tabora-Kigoma wenye urefu wa kilomita 1,505 zitajengwa katika vipande vinne.
Alisema kipande cha Tabora-Kigoma (km 411) na kile cha Uvinza-Musongati-Gitega (km 282) viko katika hatua ya manunuzi ya msimamizi na mkandarasi.
Kwa mujibu wa Kadogosa, kipande cha Kaliua-Mpanda-Karema (km 317) na kile cha Isaka-Rusumo-Kigali (km 495) viko katika hatua ya utafutaji wa fedha za ujenzi.
"Huku tumelenga biashara, tunataka kufika Congo, tukifika Kigoma tunaweza kutumia Ziwa Tanganyika na kwenda Kiremeya DRC na hatimaye Lubumbashi na hii ndio kufungua nchini na kufungua ambako ni kuwezesha watu wafanye biashara," alisema Kadogosa.
Aliongeza: "Pia tukifika Kigoma unaweza fika bandari ya Uvila eneo la Bukavu lenye idadi kubwa ya watu na kuna madini. Na kipande cha Uvinza-Msongati –Kitege, hapa kuna machimbo makubwa ya Nikeli ambayo yatakuwepo kwa zaidi ya miaka 100."
“Sio kama tunajenga tu, bali tunajenga tukiwa na lengo la kupata kitu ndani ya miaka mitano au 10 na itakuwa ni kutekeleza maelekezo ya Rais Samia ya kuifanya Tanzania kuwa kivutio kwa usafirishaji," alisema Kadogosa.
Alisema ukanda wa Kusini unajumuisha ujenzi wa njia ya reli ya Mtwara-Mbambabay na matawi ya Liganga na Mchuchuma (km 1,000) huku Kanda ya Kaskazini ambayo ni muhimu kwa sababu ya bomba la mafuta linalotoka Uganda kwenda Tanga, itajumuisha ujenzi wa njia ya reli ya Tanga-Arusha-Musoma (km 1,028).
Kadogosa alisema utekelezaji wa miradi hii utafanywa kwa ubia na kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa awali imekamilika.
Mapato yatakayoongezeko
Kadogosa alisema mradi huo unatarajiwa kuanza kutoa faida baada ya miaka mitano ya utekelezaji wake.
Alisema pia utawezesha ongezeko la usafirishaji wa mizigo ambapo reli itabeba mzigo wa mpaka tani 10,000 kwa mkupuo sawa na uwezo wa malori 500 ya mizigo.
Alisema pia itachochea maendeleo katika sekta ya kilimo, biashara, madini na viwanda hususani katika maeneo ambapo reli hiyo inapita pamoja na kwa nchi jirani na kupunguza gharama za mara kwa mara za matengenezo ya barabara.