Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

SCCULT yapongeza vyama kufutwa

Thu, 7 May 2020 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

SIKU moja baada ya serikali kuvifuta rasmi vyama hewa vya ushirika 3,348, Chama Kikuu cha Ushirika wa Akiba na Mikopo Tanzania (SCCULT Ltd-1992), kimesema vyama hivyo vilianzishwa kwa malengo ya kisiasa na havikuwa na uhakika wa uhai wake.

Jana, Mkurugenzi Mtendaji wa SCCULT Ltd, Hassani Mnyone, akizungumzia uamuzi huo alisema chama hicho kinaunga mkono uamuzi huo wa serikali, kwa vile kulikuwa na makosa yalifanyika wakati wa uandikishaji wa vyama hivyo.

Kwa mujibu wa Mnyone, miongoni mwa makosa hayo ni pamoja na kutozingatiwa kwa hali ya kiuchumi ya muda mrefu ya vyama, jambo ambalo ni muhimu kupima uhai wa chama cha ushirika kuendelea kutoa huduma zake.

“Kimsingi ilikuwa ni muhimu kufanyika, kwa sababu kulikuwa na vyama vingi ambavyo vilikuwa havifanyi kazi yoyote na havijulikani vilipo. Kwa upande wa Saccos ilikuwa ni lazima ifanyike hivyo ili kuhakikisha utekelezaji wa matakwa ya Sheria ya Huduma Ndogo za Fedha ya mwaka 2018 na kanuni zake za mwaka 2019.

“Tunakuwa na Sacco’s ambazo tayari zina nguvu na zinahudumia wanachama wake vizuri, sasa hivi tunavyo vyama ambavyo ni hai, vina nguvu na vina hudumia watu wake. Jukumu letu kama wadau ni kuhakikisha vyama hivi vinaendelea kuwa imara kwa kutoa usaidizi mkubwa wa kitaalamu, kuvipatia nafasi ya kujifunza kuanzia wanachama, viongozi na watendaji.”

Juzi, Waziri wa Kilimo, Josephat Hasunga, akiwa jijini Dodoma alitangaza kufutwa kwa vyama hivyo vya ushirika, pia alivitaka vyama vilivyosalia kuimarisha mwenendo wao.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live