Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ruvuma yavuka lengo uzalishaji Mahindi

Pics Pg 9 Agosti 18 Ruvuma yavuka lengo uzalishaji Mahindi

Wed, 18 Aug 2021 Chanzo: ippmedia.com

MKOA wa Ruvuma kwa mwaka 2020/2021 umezalisha ziada ya mahindi tani 326,497 kati ya tani za mahindi 816,242 zilizozalishwa.

Akizungumza wakati anazindua soko la ununuzi wa mahindi Kanda ya Songea mkoani Ruvuma katika Kijiji cha Mgazini Halmashauri ya Songea, Mkuu wa Mkoa huo, Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge, alisema katika kipindi cha mwaka 2020/2021, wakulima wa mahindi wamelima hekta 276,488.

“Uzalishaji huu ni zaidi ya kiwango kilichozalishwa kwa ongezeko la asilimia nne, ikilinganishwa na kiwango cha uzalishaji katika msimu wa mwaka 2019/2020 ambapo tani 787,321 pekee zilizalishwa,’’ alisisitiza Ibuge.

Brigedia Jenerali Ibuge alisema mkoa una uwezo wa kuuza ziada hiyo ndani na nje ya nchi ambapo aliupongeza Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) kwa uamuzi wa kununua mahindi ambayo ni sehemu ya ziada.

Alisema katika awamu ya kwanza ya ununuzi kutakuwa na vituo tisa katika mkoa mzima, ambavyo vimepangwa, kwa lengo la kumrahisishia mkulima kuuza mahindi yake bila kutumia gharama kubwa.

Hata hivyo, alisema kiwango cha kununua tani 32,000 tu za mahindi kwa Mkoa wa Ruvuma ambacho kimewekwa na NFRA ni kidogo ikilinganishwa na uzalishaji mkubwa wa mahindi uliofanywa na wakulima msimu huu.

Alisema mgao huo ni kidogo, hivyo alitoa rai kwa Wizara ya Kilimo kupitia NFRA kuendelea kushirikiana kupanua wigo wa masoko ili wakulima wa Ruvuma waendelee kuzalisha ziada.

Meneja wa NFRA Kanda ya Songea, Ramadhani Nondo, alisema  kwa ujumla NFRA katika msimu wa mwaka 2020/2021, inatarajia kununua tani za mahindi 165,000 ambapo  Kanda ya Songea imetengewa kununua tani 32,000, na kwamba kwa awamu ya kwanza zinanunuliwa tani 6,000.

Amesema mahindi yatanunuliwa kwa shilingi 500 kwa kilo katika kituo cha NFRA Ruhuwiko na vituo vingine yatanunuliwa kwa shilingi 470, na kwamba ununuzi utafanyika kwenye vituo tisa vilivyopangwa ambavyo ni Namtumbo Mjini, Namabengo, Mgazini, Magagura, Mpitimbi, Mbinga Mjini, Kigonsera na Ofisi za Kanda za NFRA Ruhuwiko.

Chanzo: ippmedia.com