Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ruksa kuagiza chuma chakavu nje

Image 68865 2 Ruksa kuagiza chuma chakavu nje

Mon, 28 Feb 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Serikali imeruhusu wenye viwanda kuagiza vyuma chakavu kutoka nje ya nchi ili kupata malighafi za kuzalisha bidhaa za chuma, jambo litakalochochea ukuaji wa viwanda nchini.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Dk Selemani Jafo alisema hayo juzi, katika mahojiano na Mwananchi alipotembelea Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL), jijini Dar es Salaam.

Alisema lengo la Rais Samia Suluhu Hassan ni kuhakikisha viwanda vinakwenda mbele zaidi, hivyo kwa kutambua changamoto ya uhaba wa malighafi za viwanda hivyo, Serikali iliruhusu vyuma chakavu kuingizwa kutoka nje.

“Mwaka jana ilitulazimu turekebishe kanuni ya watu kuagiza vyuma kutoka nje kwa ajili ya uwekezaji, uendelee kuimarika hapa nchini, kwa hiyo jambo hili tumelifanya,” alisema Waziri Jafo.

Dk Jafo alisema huko nyuma kulikuwa hakuna viwanda vingi vya bidhaa za chuma na nondo nyingi zilikuwa zinatoka nje ya nchi, lakini sasa kuna viwanda vingi vinavyozalisha nondo, hasa kiwanda cha Lodhia na Kamal Steel.

Alisema viwanda hivyo vimesaidia kwenye miradi mikubwa inayotumia nondo zinazozalishwa hapa nchini, jambo ambalo ni fursa kwa ukuaji wa viwanda hivyo kwa sababu soko la uhakika lipo.

“Serikali ya mama Samia, lengo lake ni viwanda viweze kwenda mbele zaidi, uwekezaji uwe mbele zaidi,” alisema Jafo na kusisitiza kwamba nchi imepiga hatua kwa kuzalisha nondo nyingi hapa nchini.

Kabla ya Serikali kubadilisha kanuni hizo, wenye viwanda hawakuruhusiwa kuagiza nje vyuma chakavu, jambo lililodaiwa kuchochea uharibifu wa miundombinu kwa sababu ya biashara hiyo.

Aprili 2020, Mkurugenzi Mkuu wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), Dk Samuel Gwamaka aliwaelekeza wenye viwanda kununua chuma chakavu kutoka kwa wafanyabiashara waliosajiliwa na kutambulika na baraza hilo. “Utafiti wetu unaonyesha uhujumu mkubwa wa miundombinu hapa nchini, hali iliyochangia kufunga usafirishaji wa chuma chakavu nje ya nchi.

“Kuanzia sasa wenye viwanda wote watalazimika kununua chuma chakavu kutoka kwa wafanyabiashara ambao wamesajiliwa na NEMC ili kulinda miundombinu,” alisema Dk Gwamaka.

Wenye viwanda wamefurahishwa na hatua hiyo ya Serikali kwa kile walichosema itawasaidia kupunguza gharama za uzalishaji kwa kuchanganya chuma chakavu na chuma asilia katika utengenezaji wa bidhaa zao.

Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Ando Roofing Products Ltd, Ado Maimu alisema bei ya chuma asilia iko juu ukilinganisha na chuma chakavu, hivyo wakichanganya vyote itawasaidia kupunguza gharama za uzalishaji na kuwafanya waweze kushindana na mataifa mengine.

“Hapa Tanzania hatuna vyuma chakavu vya kutosha kutokana na kule tulikotokea, hatukuwa na base ya viwanda vinavyotumia vyuma vikubwa vikubwa bali tumekuwa na viwanda vile vya kati.

“Kwa hiyo ile nafasi waliyotupa ya kuagiza kutoka nje inatusaidia kwa maana ya kubalance, ili tuweze kuagiza chuma material na chuma chakavu na kuchanganya pamoja kupata chuma na bei yetu ya ndani ikawa nzuri na tukaweza kushindana na vile vya wenzetu,” alisema Maimu.

Hata hivyo, mdau huyo wa chuma aliishauri Serikali kuwekeza kwenye mradi wa chuma wa Liganga ili Tanzania iweze kuzalisha chuma kwa wingi kwa ajili ya viwanda vya ndani na ziada kuuzwa nje ya nchi.

“Serikali iamue sasa kuwekeza kwenye mradi huo kwa namna yoyote, hata kama ni kwa kuuza share, kama itakuja na kitu cha namna hiyo, nina uhakika ile ingetutoa sana na ingetufanya tukaenda vizuri kuliko hata hii waliyoruhusu ya kuagiza vyuma kutoka nje,” alisema Maimu.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live