Serikali imetaja mafanikio yaliyotokana na filamu ya Royal Tour katika kupindi cha mwaka mmoja ambapo hadi Machi, 2023, jumla ya miradi mikubwa 26 ya uwekezaji katika utalii imesajiliwa, ikilinganishwa na miradi 16, Machi 2020.
Akitaja mafanikio hayo mbele ya waandishi wa Habari jana Aprili 28, 2023 jijini Dodoma, Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Dk Hassan Abas amesema tangu kuzinduliwa kwa filamu hiyo mwaka jana mafaniko kadhaa yameoneka kiuchumi.
Dk Abass amesema kwa mujibu wa ripoti ya kituo cha Biashara nchini (TIC), hamasa na mguso wa filamu ya Royal Tour umeongeza idadi ya wawekezaji nchini.
Amesema hadi Machi, 2023, jumla ya miradi mikubwa 26 ya uwekezaji katika utalii imesajiliwa, ikilinganishwa na miradi 16, Machi 2020 kabla ya Royal Tour.
Dk Abass ambaye ni Mwenyekiti wa kamati iliyoandaa filamu hiyo amesema TIC imeshuhudia ongezeko la miradi ya uwekezaji wa kitalii ikiwemo kusajiliwa mradi mkubwa wa Dola milioni 300 uitwao Tourism Adventure Park utakaokuwa na hoteli, maeneo ya utalii wa kitamaduni na michezo.
Katibu Mkuu huyo amesema akiwa Marekani mwaka jana Rais Samia Suluhu wakati wa uzinduzi wa Royal Tour pia alishuhudia mikataba ya awali 8 ikisainiwa.
Amesema katika mikataba hiyo ilihusisha sekta binafsi na sita ya kiserikali ilisainiwa ambapo uwekezaji wake utafikia thamani ya zaidi ya Sh11.7 trilioni.
“Baadhi ya wawekezaji hao wameshafika nchini na kupewa ardhi kama kampuni ya Camdemi HB, Kampuni ya Polo Properties imeshasajili mradi TIC na kampuni za Northern New Feed zimeshafika nchini na taratibu zinaendelea,”amesema Dk Abass.