Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Rostam kuingiza Sh470 bil akiuza hisa Vodacom

Tue, 3 Jul 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Kutokana na mauzo ya hisa anazomiliki ndani ya kampuni ya Vodacom, Rostam Aziz anatarajia kuingiza takriban Sh470 bilioni.

Hata hivyo, kiwango hicho kitategemea mazungumzo baina ya pande zinazohusika lakini taarifa za Soko la Hisa Dar es Salaam (DSE) zinaonyesha hisa moja ya Vodacom Tanzania ilikuwa inauzwa na kununuliwa kwa Sh800 jana.

Bei hiyo ikizidishwa na hisa anazomiliki Rostam ndani ya kampuni hiyo, iwapo zitauzwa kwa bei ya soko, basi mfanyabiashara huyo ataingiza kiasi hicho. Jarida la Forbes juzi limeripoti hisa za Rostam zina thamani ya Dola 200 milioni za Marekani (zaidi ya Sh55 bilioni).

Hii itakuwa ni mara ya pili kwa bilionea huyo kuingiza mabilioni baada ya kufanya hivyo mwaka 2014, alipouza asilimia 17.5 ya hisa zake kwa Dola 240 milioni za Marekani (zaidi ya Sh545 bilioni).

Wakati anauza hisa hizo mwaka 2014, Rostam alikuwa ni mmiliki wa kampuni ya Calvary Holdings iliyosajiliwa huko visiwa vya Jersey nchini Uingereza lakini awamu hii anafanya hivyo akimiliki hisa hizo chini ya kampuni ya Mirambo Limited.

Taarifa zinaonyesha Mirambo hiyo imesajiliwa Tanzania ikimilikiwa na kampuni ya East Africa Investment (Mauritius) Limited iliyosajiliwa Jamhuri ya Seychelles.

Vodacom Tanzania, kampuni pekee ya mawasiliano iliyotekeleza matakwa ya Sheria ya Elektroniki na Mawasiliano ya Posta (Epoca) ya mwaka 2010 kwa kuorodhesha asilimia 25 ya hisa zake Soko la Hisa Dar es Salaam (DSE) ilifanya hivyo Agosti ya mwaka jana.

Chanzo: mwananchi.co.tz