Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Rostam Aziz kuuza hisa zake zote za Vodacom

10123 Rostam+pic TZW

Thu, 28 Jun 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Tume ya Ushindani Tanzania (FCC), imetangaza mpango wa kampuni ya Vodacom Group kununua hisa zote anazozimiliki mfanyabiashara maarufu nchini, Rostam Aziz.

Taarifa ya hivi karibuni iliyotolewa na tume hiyo inasema imepokea maombi ya kampuni hiyo ya Afrika Kusini kununua asilimia 26.25 ya hisa zinazomilikiwa na kampuni ya Mirambo ambayo ni mali ya Rostam inayosimamia hisa hizo ndani ya Vodacom Tanzania.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, kampuni ya uwekezaji ya Mirambo imesajiliwa Tanzania ikimilikiwa na kampuni ya East Africa Investment (Mauritius) iliyosajiliwa katika Jamhuri ya Shelisheli.

“FCC inalichunguza ombi hili. Mtu yeyote mwenye pingamizi awasilishe ushahidi unaojitosheleza utakaoisaidia tume kufanya uamuzi sahihi,” inasomeka sehemu ya taarifa hiyo ya Aprili 4.

Vodacom Group ni kampuni tanzu ya Vodaphone ya Uingereza inayotoa huduma katika Bara la Afrika.

Vodacom Group imeorodheshwa kwenye Soko la Hisa Johannesburg (JSE) na kwa sasa inamiliki asilimia 48.75 ya hisa za Vodacom Tanzania.

Hii si mara ya kwanza kwa Rostam aliyekuwa mbunge wa Igunga na mjumbe wa kamati na halmashauri kuu za CCM kuuza hisa za Vodacom anazomiliki.

Kwa mara ya kwanza, Rostam aliuza sehemu ya hisa zake Aprili 2014. Mwaka huo, aliuza asilimia 17.2 ya asilimia 35 alizokuwa anamiliki kwa Vodacom Group kwa Dola 240 milioni za Marekani.

Wakati huo, mfanyabiashara huyo alikuwa anamiliki hisa hizo kupitia kampuni yake ya Cavalry Holdings iliyosajiliwa katika visiwa vya Jersey vilivyopo nchini Uingereza.

Kutokana na mauzo hayo, umiliki wa Vodacom Group uliongezeka kutoka asilimia 65 mpaka 82.2 ndani ya Vodacom Tanzania.

Mwanzoni mwa Agosti mwaka jana, Vodacom Tanzania iliorodhesha asilimia 25 ya hisa zake kwenye Soko la Hisa Dar es Salaam (DSE) ili kuwapa nafasi Watanzania kuimiliki kampuni hiyo, hivyo kubadili umiliki wake.

Kwa mabadiliko hayo, Vodacom Group inaendelea kuwa mmiliki mkubwa zaidi wa Vodacom Tanzania ikiwa na asilimia 48.75 ikifuatiwa na Rostam mwenye asilimia 25.25 na zinazobaki zikienda kwa wawekezaji wengine wadogo.

Mpaka mwaka 2014, Jarida la Forbes lilimkadiria Rostam (53), kuwa na utajiri unaofikia Dola 1 bilioni kutokana na miradi aliyonayo kwenye sekta za madini, uendelezaji majengo, bandari na uwekezaji kwenye hisa za kampuni tofauti.

Chanzo: mwananchi.co.tz