Benki ya Standard Chartered Tanzania imetoa ripoti yake ya kwanza inayoonesha mchango wa Benki hiyo katika kuchochea maendeleo endelevu kwa mwaka 2022 iitwayo 'Here for good: a sustainable future for Tanzania’ ripoti ambayo inaangazia juhudi za Benki na mafanikio yaliyopatikana katika kuleta maendeleo ya kijamii na kiuchumi nchini Tanzania.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, Kampuni imechangia maendeleo kwa Watanzania kupitia nguzo tatu za maendeleo za benki, uwekezaji wa fedha katika miradi endelevu, kampuni inayowajibika na ujumuishaji ambapo akizungumza wakati wa hafla ya uzinduzi, Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki hiyo Herman Kasekende alisema, “Ripoti hii inaonesha namna ambavyo mbinu za maendeleo endelevu huchochea ukuaji wa uchumi, kuboresha ustawi wa jamii na kulinda mazingira kwa ajili ya vizazi vijavyo"
Naye Naibu Katibu katika Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira) Dr. Switbert Mkama ambaye alikuwa Mgeni rasmi katika hafla hiyo alisema "nimefurahishwa sana na maendeleo ambayo yamepatikana kutoka katika uwekezaji wa fedha katika miradi endelevu na jinsi benki inavyounga mkono juhudi za Serikali katika kuifanya Tanzania kuelekea kwenye uchumi wa viwanda.”
Utafiti na data ndani ya ripoti hiyo vinaonesha juhudi za kimaendeleo zinazofanywa na Benki hiyo ikiwemo katika uwekezaji wa fedha katika miradi endelevu ambapo imefadhili TZS 3.7 quadrillioni katika ujenzi wa mradi wa Reli mpya ya Standard Gauge (SGR) kutoka Dar es salaam hadi Dodoma (Makutupora) ambayo ikikamilika itapunguza gharama za usafirishaji wa mizigo kati ya DSM na Kongo kutoka kima cha chini cha dola 6,000 kwa tani hadi dola 4,000.