Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ripoti Maalum Waziri: Corona imesababisha majanga mazao manne nchini

HASUNGA IPPMEDIA.webp Ripoti Maalum Waziri: Corona imesababisha majanga mazao manne nchini

Mon, 4 May 2020 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

*Chai hali mbaya, mengine yanafuata *Adokeza umakini hifadhi ya chakula

WIZARA ya Kilimo imesema mlipuko wa virusi vya corona, umesababisha madhara makubwa kwa chai nchini, zao lililoiingizia nchi fedha za kigeni wastani wa Sh. bilioni 100 kwa msimu uliopita wa kilimo.

Akizungumza na Nipashe jijini Dodoma wiki iliyopita, Waziri mwenye dhamana na kilimo, Japhet Hasunga, alisema mbali na chai inayoongoza kwa hali mbaya, mengine yaliyo katika mkumbo wenye mwelekeo huo ni kahawa, tumbaku na pamba.

Hasunga alifafanua kuwa eneo kuu la athari linahusu kushuka kwa bei ya mazao ya biashara yanayosafirishwa nje, huku chai ikiwa katika hali mbaya zaidi.

Kwa mujibu wa waziri huyo, sababu kuu ya athari hiyo inatokana na taifa jirani la Kenya ambako ndiko kwenye soko jijini Nairobi, kufunga mipaka yake kutokana na janga la corona, huku Tanzania ikipategemea zaidi.

"Chai ndiyo tumeathirika kabisa kwa sababu minada ya Kenya imefungwa. Tanzania tulikuwa hatuna mnada wa chai, sasa ndiyo tunapambana kuanzisha mnada wa chai," Hasunga alibainisha.

Pia, alisema athari katika mazao mengine yaliyobaki, kwamba licha ya kutofikia athari zilizojitokeza kwa chai, nayo yameshuka bei na kuziingiza katika hatihati ya ufanisi wa kimasoko kwa kiwango kikubwa.

"Kwenye upande wa 'exports' (mauzo ya nje ya nchi), mazao yetu karibu yote tuliyokuwa tunayauza nje yanaonekana kushuka bei. Kwa mfano, pamba imeshuka bei kwa kiwango kikubwa.

"Kahawa pia tunatarajia itashuka kidogo. Itashuka bei kwa sababu walaji wakubwa, zile 'movements' zao zitakuwa 'restricted' (zitazuiwa). Utakuta baadhi ya maeneo wamefunga kabisa vile vioski vya kahawa, hiyo ina maana kwamba bei ya kahawa inaweza ikaathirika kwa kiwango fulani," alisema, huku akidokeza dalili ya athari hizo kwa tumbaku.

Mbali na athari za mauzo ya nje ya nchi, Hasunga pia alitaja sura ya pili iko katika kupanda kwa bei ya mbolea na viuatilifu, inayoendana na dalili za tishio la njaa, hivyo akawataka wananchi kujihami kwa kuhifadhi chakula.

Baadhi ya maeneo maarufu yanakozalishwa mazao yaliyotajwa na Waziri Hasunga ni Tukuyu, Mufindi, Lushoto, Amani - Muheza (Chai); Tabora, Shinyanga, Kigoma (tumbaku); Mwanza, Simiyu, Shinyanga, Tabora, Mara (pamba), Bukoba, Moshi, Tukuyu, Mbozi, Mbinga, Lushoto (kahawa).

Ripoti ya Ukaguzi kwa Mwaka wa Fedha 2018/19 ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), inabainisha kuwa, chai iliyozalishwa na kuuzwa nje ilikuwa tani 29,243.841 kwa mwaka 2018/2019, na kuiingizia nchi Dola za Marekani 43,890,138 (Sh. bilioni 100.906).

Kwa mujibu wa CAG, Charles Kichere, mwaka mmoja kabla, nchi iliuza tani 29,160.642 zilizoingiza Dola za Marekani 62,167,167 (Sh. bilioni 142.925).

Ifuatayo ni sehemu ya ufafanuzi wa Waziri Hasunga, alipohojiwa na Nipashe:

SWALI: Mlipuko wa virusi vya corona umeathiri vipi sekta ya kilimo hasa katika ‘import na export’?

HASUNGA: Kwanza kabisa, mlipuko wa hii homa ya mapafu ijulikanayo kama COVID-19, umeathiri kwa kiwango kikubwa kwenye upande wa 'imports' (bidhaa zinazoingizwa kutoka nje ya nchi).

Sisi tunategemea sana kuagiza mbolea kutoka nje, tunaagiza pia dawa kutoka nje, yaani viuatilifu, lakini tumekuwa tunaagiza mbegu. Sisi imetuathiri sana kwenye upande wetu kwa sababu bei zimepanda, na uzalishaji kule kwenye soko la dunia umeshuka.

Kwa hiyo, tunataraji kwamba baadhi ya mbolea bei zikapanda zaidi kuliko ilivyo sasa hivi. Ndiyo maana tumetumia hii nafasi katika mkakati ambao tunaufanya, tumeagiza kampuni kuhakikisha zinaagiza mbolea za kutosha kipindi hiki.

La sivyo, itafikia kipindi kama hatujaagiza, tukawa na upungufu. Kwa hiyo, hili tunataka tukabiliane nalo kwa kuagiza mapema. Na nina uhakika tayari mfumo wetu wa BPS watakuwa wanaufungua hivi karibuni. Kwa hiyo, hili eneo tumeathirika kwa kiwango fulani.

Pia kuna vifungashio ambavyo tulikuwa tunaagiza kutoka nje, tunatarajia bei yake huenda isiwe nzuri sana.

Kwenye upande wa 'exports' (bidhaa zinazosafirishwa kwenda nje ya nchi), mazao yetu karibu yote tuliyokuwa tunayauza nje yanaonekana kushuka bei. Kwa mfano, pamba imeshuka bei kwa kiwango kikubwa.

Kahawa pia tunatarajia itashuka kidogo, itashuka bei kwa sababu walaji wakubwa, zile 'movements' zitakuwa 'restricted' (zitazuiwa), utakuta baadhi ya maeneo wamefunga kabisa vile vioski vya kahawa, hiyo ina maana kwamba bei ya kahawa inaweza ikaathirika kwa kiwango fulani.

Tumbaku pia tumepata hiyo shida. Kwenye chai ndiyo tumeathirika kabisa kwa sababu minada ya Kenya imefungwa. Tanzania tulikuwa hatuna mnada wa chai, sasa ndiyo tunapambana kuanzisha mnada wa chai.

Kwa hiyo, ina maana moja kwa moja unakuta tumeathirika kwa kiwango kikubwa sana. Minada ya mazao kama mbogamboga, matunda, maua imeathirika kwa kiwango fulani.

Kwa njia nyingine, baadhi ya mazao imekuwa kama fursa, kama mazao ya chakula. Imekuwa ni fursa kwa sababu nchi nyingi zimefunga mipaka, lakini wanahitaji chakula. Imekuwa ni fursa kwa sababu usafiri ukipatikana, tunaweza kwenda kuuza na kuuza kwa bei nzuri.

Ni fursa pia kwa Watanzania kuongeza uzalishaji, ni fursa ya kuuza baadhi ya vyakula, lakini yale ya kibiashara yataathirika kidogo na kushuka kwa bei, machache sana ambayo bei inaweza ikabaki palepale au kuongezeka.

SWALI: Serikali imejipangaje kuhakikisha wananchi wana uhakika wa kupata chakula katika kipindi hiki ambacho dunia inakabiliwa na baa la corona?

HASUNGA: Kwanza, tunawahamasisha wananchi wenyewe watunze chakula ili kwamba wanapovuna, wahifadhi vizuri. Na sasa hivi sisi tatizo la chakula si kubwa kama nilivyosema awali.

Tunachojipanga sisi ni kuhakikisha kwamba, kama tutafikia mahali tutazuia watu kutoka majumbani, tutawezaje kusafirisha chakula kutoka sehemu moja kwenda nyingine. Hiyo ndiyo itakuwa changamoto yetu kubwa.

Kwa hiyo, sasa hivi tumeagiza maeneo yote; sisi kama nchi tumeigawa katika kanda nane na kila kanda tunahakikisha kunakuwa na akiba na maghala ya chakula. Maghala yapo ya kutosha, ya mpunga yapo ya kutosha, ya mahindi nayo yapo ya kutosha, vijijini huko yapo yamejaa.

Tunataka vyakula vyote vihifadhiwe katika maeneo yale, lakini pia sehemu zinazohitajika, zitumike. Kikubwa zaidi tunachokitaka sisi ni kwamba, sasa tuko kwenye mkakati wa kuagiza dawa kwa ajili ya kuhifadhi mahindi ili yasiharibike, lazima yapate dawa, yaani viuatilifu vilivyo sahihi kwa ajili ya kutunza yasibunguliwe na wadudu. Hili nalo tumejipanga.

Kubwa zaidi ambalo tunataka lifanyike kwenye upande wa chakula ni kwamba, chakula ambacho tunakitegemea kama taifa, tathmini inaonesha tunaweza kupata zaidi ya tani milioni 20 za nafaka na mazao mengine.

Kwa hiyo, tuna imani uzalishaji ni mkubwa ambao haujawahi kutokea katika historia ya nchi yetu. Chakula tunacho kingi, hatuna shida.

Mwishoni mwa mwaka jana, virusi vya corona vilitambuliwa kwa mara ya kwanza mjini Wuhan, China. Hadi jana saa sita mchana, zaidi ya watu milioni 2.97 walikuwa wameripotiwa kuambukizwa virusi hivyo katika nchi 185, huku zaidi ya watu 206,000 wakipoteza maisha kutokana na ugonjwa huo na zaidi ya 868,000 wamepona.

Mlipuko wa virusi hivyo tayari umeonekana kuwa na madhara karibu kwa sekta zote, uchukuzi (usafiri wa anga) na utalii zikiwa zimeathirika zaidi katika maeneo yote duniani kutokana na uamuzi wa nchi nyingi kufunga mipaka.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live