Licha ya juhudi kubwa zinazofanywa na Serikali katika kukabiliana na tatizo sugu la utakatishaji fedha unaotokana na biashara haramu, Tanzania bado inapoteza mapato ya kikodi yenye wastani wa dola za Marekani 1.5 bilioni (sawa na Sh3.3 trilioni) kila mwaka, hali inayoeleza kukwaza shughuli za maendeleo.
Kwa mujibu wa chapisho la kisera lililotolewa wiki iliyopita na taasisi ya Global Financial Integrity (GFI) na washirika wake, aina hii ya utakatishaji fedha ina athari mbaya kwa uchumi na jamii kwa jumla.
Vitendo hivyo vya kihalifu ni kama vile ambavyo mara kadhaa vimekuwa vikiibuliwa katika Bandari ya Dar es Salaam , hali iliyomlazimu Rais Samia Suluh Hassana kutangaza kuvunja bodi za wakurugenzi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) na ile ya Shirika la Meli kwa kutoridhika na utendaji kazi wake.
Uamuzi huo wa Rais kuzivunja bodi ulitangazwa Desemba 4, mwaka 2021.
Rais Samia alichukua uamuzi huo akisema kuna madudu mengi yanayofanywa ndani ya mamlaka hizo, kwani licha ya baadhi yake kuonyeshwa kwenye ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), bado hakukuwa na hatua zilizochukuliwa kwa wahusika.
Rais Samia alisema bado kuna mianya ya uvujaji wa mapato katika mamlaka kutokana na mifumo ya malipo kuchezewa na wafanyakazi.
“…mifumo imekuwa ikichezewa, inaonyesha kuwa mizigo imelipiwa kutoka getini, lakini sio kweli haijalipiwa hivyo bandari kukosa mapato.
Haya mapato yanayoonekana leo hayakupaswa kuwa hivyo yalivyo. Kama tungechukua hatua kudhibiti wizi huu, tungekuwa mbali sana kwenye kukusanya mapato,” alisema Rais Samia.
Ukubwa wa fedha
Iwapo kiasi hicho cha fedha Sh3.3 trilioni kingetumika katika ujenzi wa vituo vya afya, takriban vituo 7,000 vyenye thamani ya Sh500 milioni kila kimoja vingejengwa.
Kadhalika, fedha hiyo ingewezesha ujenzi wa miradi ya madaraja manne yanayofanana na lile lililopo Busisi mkoani Mwanza linalogharimu Sh716 bilioni.
Si hivyo tu, kama Sh1.3 trilioni za mkopo kutoka Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) ziliwezesha ujenzi wa madarasa 15,000, kiasi hicho cha fedha kingejenga takriban vyumba 45,000 vya madarasa.
Aidha, fedha hiyo ina uwezo wa kununua mashine 1,605 za CT-Scan na mashine 2058 za MRI na iwapo zingeingizwa katika Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa elimu ya Juu (HESLB), bajeti hiyo ingeongezeka mara tano ya Sh654 bilioni ya sasa.
Ongezeko hilo lingefanya wanufaika wafikie 140,000 kutoka 28,000 waliopo sasa.
Kama hiyo haitoshi, Sh3.5 trilioni zingewezesha ununuzi wa magari 43,750 ya kubebea wagonjwa yenye thamani ya Sh80 milioni kila moja na hivyo kila halmashauri ingekuwa na gari 230.
Ikiwa zingegawanya na idadi ya watu nchini ambao kwa sensa ya mwaka huu wanafikia, 61,741,120, kila Mtanzania angepata Sh56,688.3 ambayo ingemwezesha kununua kilo 16 za mchele kwa gharama ya Sh3,500 kwa kilo.
Pia kwa fedha hiyo kila Mtanzania angepata simu ya mkononi inayogharimu kiasi cha Sh50,000 na kiasi kubaki.
Baadhi ya matukio
Desemba 2015, TPA kwa kushirikiana na TRA, walikamata makontena tisa yanayodhaniwa kukwepa kulipa kodi.
Makontena hayo yalikamatwa, ikiwa ni mwendelezo wa watumishi tisa wa Bandari na TRA waliosimamishwa na Rais wa wakati huo, John Magufuli na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kupisha uchunguzi wa upotevu wa makontena 349 na ukwepaji wa kulipa kodi.
Katika mwendelezo huo, TPA ilitangaza kuwasimamisha kazi maofisa wake watatu katika sakata hilo. Hatua hiyo ilitokana na ziara aliyokuwa ameifanya bandarini, Waziri Mkuu.
Juni 13, 2021, watu 15 walikamatwa kwa mahojiano wakidaiwa kujiunganishia mabomba kutoka mtambo wa mita za upimaji wa mafuta wa Bandari ya Dar es Salaam na kuiba mafuta.
Hayo yalibainika wakati wa ziara ya kushtukiza katika mtambo huo iliyofanywa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Amos Makalla.
Gazeti hili lililokuwapo siku hiyo, lilijionea namna watuhumiwa hao walivyochimba kisima na kuunganisha bomba linalopita chini ya ardhi na kwenye makazi ya watu hadi katika bomba kuu la kupitishia mafuta kutoka bandarini hadi katika mtambo huo.
Ilichokisema TRA
Akizungumzia ripoti hiyo alipoulizwa na gazeti dada la The Citizen, Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipakodi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Richard Kayombo alisema: “Japo sijasoma hiyo ripoti, lakini utafiti wa namna hiyo unatupatia uchambuzi wa kina wa hali halisi juu ya tatizo hilo.”
Kwa mujibu wa Kayombo, biashara haramu huhusisha mambo mengi kama vile kuwa na biashara halali lakini yenye ukwepaji wa kodi, lakini pia kufanya biashara isiyo halali kwa mujibu wa sheria.
Kayombo alisisitiza: “Tumebuni mbinu mbalimbali katika kukabiliana na biashara haramu hasa hizi zenye misingi ya ukwepaji wa kodi, maana ndiyo zinaangukia kwenye uangalizi wetu. Tunashirikiana na vyombo vya dola kukabiliana na hili tatizo.”
Kwa mujibu wa Kayombo, TRA inafanya kazi kwa karibu na mamlaka zingine za forodha kutoka nchi jirani za Tanzania, ili kukabiliana na mtandao huo wa wafanyabiarasha haramu.
Hata hivyo, Kayombo alikiri kutokana na jiografia ya Tanzania, siyo kazi rahisi kupambana na mtandao huo japo kazi kubwa imefanyika.
“Changamoto kubwa ni kwamba biashara hii inavuka mipaka ya nchi, na kwa kuwa tuna ukanda mkubwa wa bahari karibu kilometa 1400, lakini pia tuna Ziwa Victoria, Tanganyika, na Nyasa ambayo kimsingi yako mipakani, tena na bandari zisizo rasmi, inakuwa ngumu kuzitambua,” alisema.
Aliongeza kusema: “Pia hata njia wanazotumia hawa wafanyabiashara haramu ni ngumu kujua japo katika bandari rasmi kazi kubwa inafanyika na tumekuwa tuna udhibiti mkubwa katika eneo hilo.”
Kayombo alisema kuwa mamlaka yake imeanzisha kikosi kazi maalum kinachopambana na biashara haramu na magendo, lakini pia TRA imekuwa ikifanya doria za mara mara kwa mara kwenye maeneo yanayosadikika kuwa njia za wafanya biashara hao pamoja na kutoa elimu ya kodi.
Undani wa GFI
Kwa mujibu wa GFI, wahusika katika biashara haramu pia hutoa stakabadhi za malipo zaidi ya moja, ambazo huonyesha tofauti ya ujazo au wingi wa bidhaa husika kinyume na uhalisia wa mzigo.
Ripoti pia inabainisha namba wafanyabiashara haramu hutumia mfumo usio rasmi (informal value transfer system - IVTS), ambao hutumika kutuma miamala katika mamlaka/nchi tofauti bila kusafirisha fedha halisi kama inavyotumika katika miamala ya simu.
Inasemakana mara nyingi mbinu hizi chafu zenye lengo la kutoa taarifa za uongo kwa mamlaka husika, hutumiwa kwenye utakatishaji fedha, ugaidi na ukwepaji wa kodi, ambapo asilimia tisa za kesi zilizohusiana na ugaidi zilipokea ufadhili kwa njia hii.
Hivyo basi, GFI inadhani ni wakati mwafaka kwa Serikali kuchukua hatua stahiki kukabilia na hali hii.
Hii ni pamoja na uanzishwaji wa kikosi kazi maalumu ambacho ni shirikishi hasa ukizingatia kuwa idara mbalimbali ndani ya Serikali zinahitaji kushirikiana ili kupambana na biashara haramu.
Jambo jingine ambalo GFI wameshauri ni utekelezaji wa mkakati wa kusajili wa taarifa za umiliki wa kimanufaa (national beneficial ownership registries), kwani kumekuwa na kampuni Za ‘mfukoni’ ambaZo hutumika katika uharibifu huu wa kifedha.
Kwa upande mwingine, imeshauriwa kuwa, taarifa za miamala ya kibiashara ziwasilishwe katika muda halisi zilipofanyika, lakini pia kuwa na matumizi ya teknolojia katika utambuzi wa gharama za miamala na kuweka mipango mahususi kwa lengo la kupambana na ufisadi.
Mtaalamu wa uchumi
Mshauri binafsi wa mambo ya uchumi na fedha Dk Hamis Juma, alisema: “Tanzania ni moja ya nchi tano Afrika ambazo zinafanya vizuri kiuchumi na hivyo ukuaji wake unakadiriwa kufikia asilimia 5.5 mwaka 2023/23.”
Ukuaji huu kwa mujibu wa Dk Juma, unaifanya Tanzania kuwa moja kati ya nchi kumi Afrika ambazo uchumi wake unakuwa kwa kasi.
“Hata hivyo ukuaji huo utakuwa hauna tija ikiwa kiasi kikubwa cha pesa kinapotea kutokana na ukwepaji kodi mkubwa unaotokana na biashara hizi haramu. Matokeo yake, Serikali inakuwa na wakati mgumu sana kufikisha huduma za kijamii vijijini, ambako watu wake wanategemea kilimo cha mvua, upungufu wa walimu, madawa, maji,” alisema Dk Juma.