Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ripoti Maalum -3 Hii ndiyo hatima ya korosho msimu huu

KOROSHO Ripoti Maalum -3 Hii ndiyo hatima ya korosho msimu huu

Wed, 6 May 2020 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

*Waziri afuatilia Sh. bilioni 124 'zilizopigwa' Ushirika

TOLEO la jana lilikuwa na ufafanuzi wa kina kuhusu hali ya akiba ya chakula nchini na zao la biashara la pamba. Waziri Japhet Hasunga, leo hii ana ufafanuzi wa kina kuhusu hatima ya korosho, zao lililopata msukosuko msimu uliopita.

Vilevile, ana maelezo ya kina kuhusu Sh. bilioni 124 zilizotoweka kiutatanishi kwenye vyama vya ushirika. ....... MWAKA wa fedha uliopita, serikali ilipanga bei elekezi ya Sh. 3,300 kwa kilo ya korosho na kuwataka wanunuzi wote kununua korosho za daraja la kwanza kwa bei hiyo.

Hatua hiyo ilisababisha wanunuzi wengi kugomea kununua zao hilo kwa maelezo kwamba bei elekezi hiyo ilikuwa kubwa na wasingepata faida wakati wa kuuza.

Baada ya mgomo huo, serikali iliamua kununua korosho zote zaidi za tani 200,000 kutoka kwa wakulima. Endelea na ufafanuzi wa maswali na majibu:

SWALI: Wakati unateuliwa kuwa Waziri wa Kilimo, kulikuwa na tatizo katika soko la korosho inayozalishwa nchini. Uhai wa soko la korosho msimu huu ukoje na corona hii?

HASUNGA: Ni kweli kabisa wakati ninateuliwa kulikuwa na tatizo la soko la korosho na limetusumbua sana mpaka sasa hatujamaliza kuwalipa wakulima. Mpaka sasa, wakulima bado wanatudai zaidi ya Sh. bilioni 20. Bado hatujamaliza kuwalipa.

Hii inatokana na udanganyifu uliojitokeza katika baadhi ya maeneo ambayo bado tunafanya uhakiki. Tukikamilisha, wakulima wote watalipwa hizo hela zao.

Tulichokifanya katika msimu uliofuata, ambao tumeusimamia mwaka huu na umeleta mafanikio makubwa, tuliwaruhusu soko binafsi wanunue moja kwa moja, lakini soko liwe la wazi.

Tuliamua sasa sanduku (la zabuni) litawekwa saa mbili kamili asubuhi na litafungwa saa 10 jioni, litafunguliwa katika eneo la wazi na watu wote watashuhudia katika kufungua na tutamwona nani ameahidi nini na amefanya nini na hicho alichoahidi. Kama ameshinda, huyo ndiye atatangazwa mshindi na kupatiwa zile korosho.

Hii itasaidia sana kuondokana na dosari zilizokuwapo miaka ya nyuma na udanganyifu na rushwa zilizokuwapo zitafutwa. Kwa hiyo, kwa kiwango hiki tunaweza kufanikiwa sana.

Lakini, sasa hivi katika kipindi hiki cha corona, tuna imani hii minada ambayo bado tunaiendesha vizuri sana kwa mwaka huu, huenda isifanikiwe kwa sababu watu wengi watashindwa kusafirisha na kuja nchini kushiriki minada.

Tunachokusudia kufanya, ni kuuza kwa TMX (kwa mtandao). Tunauza kwa njia ya mtandao, wanunuzi watakaa huko huko waliko, lakini watakuwa na uwezo wa kutoa ofa zao na kupata korosho zao kwa kadri watakavyoona inafaa. Tuna imani katika hili, itatusaidia.

La pili, nimeagiza Bodi ya Korosho iende na vyombo vya ushirika wakatembelee masoko, wawasiliane na wanunuzi wakubwa, waingie katika mikataba ya moja kwa moja ya kuuziana bidhaa.

Yaani kwa sasa mtu akileta bei ambayo tunaiona kwamba ni nzuri na 'reasonable' (inayokubalika) na iko kwenye kiwango cha soko la dunia, basi tunaingia naye mkataba wa moja kwa moja. Kinachobaki sasa ni kwenda kusafirisha tu mzigo na kumpelekea.

Lazima tuingie mikataba ya moja kwa moja, badala ya kutegemea kuja kuanzisha minada maana isipofanikiwa, inakuja kuwa dosari. Kwa hiyo, tunafikiri utaratibu huu unaweza kutusaidia sana.

Na tumeagiza pia balozi zetu zote zitafute wanunuzi huko ili tuzungumze nao, tuingie mikataba ya mauziano ya korosho. Hii itakuwa ni njia ambayo inaweza ikasaidia.

Jambo la mwisho, tumezungumza pia na wawekezaji mbalimbali kutoka Marekani na maeneo mengine, nchi za Scandinavia (Denmark, Norway na Sweden), wanataka waje wajenge viwanda vya kuongeza thamani.

Tukiongeza thamani, tukabangua korosho hapa nchini, soko la korosho nchini litakuwa vizuri. Kwa mwaka huu, hatuwezi kusema tutabangua zote kwa sababu hata viwanda vyenyewe ambavyo vipo, viko 30, vingine havijajengwa, lakini lazima tutafanya hicho kitu kizuri.

SWALI: Uhai mpya wa ushirika ulioibuliwa na Rais John Magufuli na viwanda vyake, unakusaidiaje?

HASUNGA: Kwa kweli umetusaidia sana. Maelekezo ya Mheshimiwa Rais kwamba 'tunataka ushirika ambapo serikali itaweka mkono, ushirika ambao utasimamiwa ipasavyo, ambao utakuwa ni tumaini la wakulima wengi' na Watanzania kwa ujumla', yamefanikiwa kwa kiwango kikubwa na yameleta ari mpya.

Wakulima hawana chombo chochote cha kuwaunganisha. Ni kupitia ushirika ndiyo unaweza ukawaunganisha wakawa kitu kimoja, wakazungumza kwa sauti moja, wakajadiliana bei ya mazao yao kwa sauti moja. Ndiyo ushirika ambao tunautaka.

Ushirika ambao unaweza ukamhudumia mkulima, ushirika ambao utajua mkulima wake anahitaji pembejeo gani, anahitaji mbegu gani na atapataje kipindi ambacho hana hela, ushirika ambao utaweza kuwakopesha wanachama wake. Ndiyo ushirika ambao tunautaka.

Kikubwa ambacho kilikuwa kinafanyika kwenye uendeshaji wa ushirika, ni ubadhirifu mkubwa kwenye mali za ushirika na fedha za ushirika.

Hatua gani ambazo tumezichukua? Utaona wizara tumeanza kuchukua hatua kutokana na maagizo ya Mheshimiwa Rais. Tumesimamia ukaguzi wa vyama vya ushirika na ripoti ikatolewa. Yale yaliyoonekana ni upungufu, tumeanza kuwachukulia hatua.

Na kwa kujua kuna mamlaka zile za kuwafikisha watu mahakamani, nilichukua zile ripoti, nikaikabidhi Takukuru (Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa) ili wawakamate wale na kuwapeleka mahakamani na wewe umeona jinsi Takukuru walivyopambana katika hilo na sisi tunawashukuru sana.

Katika maelekezo yangu, ilionekana kuna karibu Sh. bilioni 124 zilikuwa zimeibwa kipindi kile na vyama vya ushirika. Kwa hiyo, bado ninalifanyia kazi.

Mpaka sasa, wamehakiki Sh. bilioni 68, wanaendelea na uhakiki ili tubaini hasa ni kiasi gani cha fedha ambacho kimeibwa na vyama vya ushirika na wale walioiba, wachukuliwe hatua na wazirejeshe hizo fedha.

Tuna imani kwa kufanya hivyo, kwanza itakuwa ni fundisho kwa vyana vya ushirika, wataacha kujishirikisha na wizi. La pili, wananchi watakuwa sasa na imani na vyama vya ushirika na kila kiongozi atakayekuwapo pale, atakuwa anawahudumia wananchi moja kwa moja.

Tatu, watu hawatataka tena kudhalilika kama walivyodhalilika mwaka huu. Maana wale watu tukiwakuta ni wezi, tunakamata mali zao, tunakamata nyumba zao, tunawafikisha mahakamani, wanashtakiwa kwa Sheria ya Uhujumu Uchumi. Hiyo sasa imetuletea ari mpya na mambo yanakwenda vizuri.

Pia, tunapitia upya Sheria ya Ushirika ili kurekebisha dosari mbalimbali zilizojitokeza zilizotokana na mfumo wa sheria, na kuangalia sifa za viongozi, ili kiongozi anayesimamia ushirika awe somo au taaluma fulani. Tunataka hao ndiyo wasimamie ushirika, ili ushirika uwe na manufaa makubwa kwa wananchi wote.

*JE, MABWANA SHAMBA NA WATAALUMA WA FANI HIYO NA SUALA LA MABORESHO LINA NAFASI GANI KATIKA KUINUA KILIMO? FUATILIA KESHO.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live