Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ripoti Maalum -2 Waziri: Hii ndiyo hali ya chakula nchini

Tue, 5 May 2020 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

*Pamba, aendeleza alipoachia Majaliwa

BAADA ya jana kupata ufafanuzi wa Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga, kuhusu kishindo cha corona kwenye mazao makuu manne ya biashara nchini, mjadala wa Nipashe na waziri huyo leo unaangalia mustakabali wa akiba ya chakula nchini ilikosimama katika zama hizi za corona, pia harakati za kuliinua zao kongwe la pamba nchini.

SWALI: Hali ya chakula ikoje kwa sasa nchini na kwenye Ghala la Taifa? NFRA watanunua tani ngapi mwaka huu?

HASUNGA: Bado tuko kwenye mchakato wa kuangalia kiasi gani watanunua, lakini kwa upande wa chakula, kwanza kama nchi, sisi mfumo wetu uko tofauti kidogo na nchi nyingi.

Chakula kingi mwananchi ananunua mwenyewe. Chakula ambacho kinahifadhiwa na Hifadhi ya Taifa ni chakula ambacho ni cha dharura. Hicho ndicho tunatunza. Mpaka sasa tuna tani 47,000 kwenye ghala.

Na nimezunguka nchi nzima, chakula ni kingi. Mwaka huu watu wamehamasika sana, wamezalisha sana, chakula ni kingi na sasa hivi mavuno yameanza. Maeneo mengi zaidi mahindi yameanza kukauka, mpunga uko tayari unavunwa na vyakula vingine vingi.

Kwa hiyo, sasa chakula ni kingi na nina imani hali ikiendelea kama hivi, Watanzania kwa upande wa chakula hatutakuwa na upungufu. Lakini sasa kama NFRA tunataka tufanyeje?

Kwanza, tumeimarisha uwezo wetu wa kuhifadhi. Uwezo wetu ulikuwa ni kuhifadhi tani 251,000. Baada ya kuanza kujenga haya maghala ya kisasa, tunaongeza uwezo wa kuhifadhi kwa tani 250,000.

Ina maana kwamba NFRA itakuwa na uwezo wa kununua na kuhifadhi kwa wakati mmoja tani 501,000. Ina maana uwezo umeongezeka mara mbili.

Na tayari tumeagiza NFRA wanunue mazao hayo kwa njia mbili; ya kwanza watanunua yale ambayo ni kwa ajili ya kutunza kwenye Hifadhi ya Taifa. Tutawapa fedha ambayo tutaitenga kwenye bajeti pamoja na hiyo akiba ambayo wanayo. Tutahakikisha tunahifadhi kwenye Hifadhi Taifa tani zisizopungua 120,000. Huo ndiyo utaratibu tunaoutaka.

Halafu tunataka sasa karibu tani 400,000 wawe na uwezo wa kununua na kuuza, waingie kwenye mikataba ya kununua na kuuza.

Kwa mfano, WFP wanahitaji, watanunua, yaani hata shirika lolote litakalokuwa linahitaji, nchi za nje watakapokuwa wanahitaji, wanunue kutoka NFRA.

Tunataka wafanye hivyo na ndiyo maana tumewapa mamlaka sasa waweze kukopa hela kama hawana fedha za kutosha au wawe na mikataba mizuri na wale wanunuzi, wawanunulie kusudi hilo lifanyike.

Kwa hiyo, tuna imani tutakuwa tumetengeneza soko kwa wakulima, lakini pia tutakuwa tumewezesha shirika letu uwezo wa kufanya kazi kwa mwaka mzima.

SWALI: Vita inayoongozwa na Waziri Mkuu kuibua tena zao la pamba, unaielezeaje ilikofika?

HASUNGA: Kwanza, ninampongeza sana Mheshimiwa Waziri Mkuu, ninampongeza sana Mheshimiwa Rais John Magufuli kwa jitihada walizokuwa wamezifanya, kwa sababu wakati mimi ninaingia, nilikuta tayari wameshaanza kuzifanya hizo jitihada za kufufua hili zao la pamba.

Kwa kushirikiana na Wizara ya Kilimo na wadau wengine, tumehamasisha sana uzalishaji uongezeke na ndiyo maana utaona kwa mwaka huu tumepata tani 348,850 za pamba, lakini tunataka uzalishaji huu uongezeke.

Kufanikisha hilo, tumeamua kutafuta maeneo yanayofaa kwa uzalishaji wa mbegu za pamba. Pia, tunataka kuhamasisha wakulima waongeze tija badala ya kulima wanapata labda wastani wa kilo 200 kwa ekari, tunataka wapate kilo 1,000 mpaka 1,500 (ongezeko la kati ya asilimia 500 na 750).

Kwa hiyo, tunataka waongeze tija, waongeze matumizi sahihi ya viuatilifu, lakini mbolea zinazohitajika kwenye pamba, wengi wao watumie mbolea. Tunataka tuwe na mbolea ambazo wanaweza kuzitumia, lakini wanaweza kupanda kwa kilimo kile cha mstari, kitaalamu kabisa cha kamba iliyonyooka, kilimo kinapendekeza.

Kama yote hayo wakizingatia, tuna imani kwamba wanaweza kuongeza uzalishaji zaidi. Lengo letu sisi ni kufikia tani 600,000 kwa mwaka na hivyo kama tukifikia hicho kiwango, kiasi fulani, angalau hata nusu ya pamba hiyo iwe inatumika kwenye viwanda vya ndani na ile nyingine tuwe tunauza kama malighafi katika maeneo mbalimbali. Hilo ni jambo la kwanza.

La pili, Mheshimiwa Waziri Mkuu amesimama kidete kuhakikisha viwanda vyote vile vya pamba, vile vilivyokuwa vinachambua pamba vinafufuliwa. Na sasa tumefikia viwanda vingi sana vilivyokuwa chini ya ushirika, tumeagiza vyote vifufuliwe, na vya watu binafsi navyo tunataka vifufuliwe.

Zaidi ya hapo, tunataka tuongeze zaidi viwanda vya kutengeneza nyuzi na tukitoka hapo, tunakwenda kwenye viwanda vya kutengeneza majola ili badala ya soko la pamba kutegemea twende kuuza nje ikiwa ni malighafi, tutengeneze nguo hapahapa nchini, watu wetu wapate nguo hapahapa zinazotokana na pamba yetu, na sisi wenyewe tuvae nguo za kwetu.

Hiyo tunaamini kwamba tutakuwa tumetengeneza ajira nyingi sana kwa Watanzania, lakini pia tutakuwa tumeongeza thamani na uchumi wetu utakuwa umekua vizuri sana kuliko kwenda kuuza nje ya nchi.

Pia, tumeamua Bodi ya Pamba kuiongezea uwezo, tumewapa mamlaka waajiri maofisa ugani wa kwao kwa ajili ya kusaidia utaalamu. Hii nayo ni sehemu ya jitihada ambazo tumeamua kuzifanya na tunafikiri itachangia sana kuongeza uzalishaji.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live