Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Redio yabadili maisha ya wakulima wa maharagwe

Tue, 4 Dec 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Arusha. Uzalishaji wa maharagwe kwa wakulima zaidi 1,000 katika mabonde ya Kapori, Kileo na Kivulini wilayani Mwanga, umeongezeka kwa asilimia 133 kutokana na elimu inayotolewa kwa njia ya radio.

Wakulima Bakari Mmbaga, Waziri Hassan, Ridhiwani Ismail, Juma Athman Mmbaga, Azizi Nyasi na Jovini Shirima wanaolima katika Bonde la Kileo walisema hayo walipozungumza na Gazetil la Mwananchi.

Walisema wao ni miongoni mwa wakulima 100,000 ambao wamefikiwa na mradi wa Farm Radio International (FRI) maarufu Redio kwa Wakulima, unaojulikana kwa jina la Uptake.

Mradi huo unafadhiliwa na Mfuko wa Kimataifa wa Maendeleo ya Kilimo (IFAD) chini ya mfuko wa New Alliance ICT Extension Fund Activity.

Meneja wa Programu ya FRI ukanda wa Kusini na Mashariki mwa Afrika, Rex Chapota alisema lengo la taasisi yake ni kuwajengea uwezo watangazaji ili watoe huduma za utangazaji zenye kukuza uelewa miongoni mwa wakulima wadogo, familia zao na jamii zinazowazunguka.

“Tunaamini elimu hii italeta maendeleo ya kiuchumi na uhakika wa chakula kwa wakulima wadogo. Kazi yetu ni kuhakikisha kila mkulima mdogo anapata huduma za vipindi vya radio zitakazomsaidia yeye kupata mafanikio,” alisema Chapota.

Mkoani Kilimanjaro, Uptake hufanya kazi kwa karibu na Redio ya Sauti ya Injili, ambayo hutoa elimu kwa ushirikiano na wataalamu wa zao la maharagwe kutoka Taasisi ya Utafiti wa Kilimo ya Selian ya Arusha.

“Kabla ya kujiunga na mpango huu, tuliweza kuvuna magunia matatu tu ya maharage kutoka katika shamba lenge lenye ukubwa wa ekari moja. Hivi sasa tunavuna mpaka magunia saba kwa shamba lenye ukubwa sawa na huo,” alisema Mmbaga.

Naye kiongozi wa kikundi cha wakulima cha Lilangwera kinachopatikana katika kijiji cha Nasholi Mkoani Arusha, Bi. Elishililia Mollely alisema mradi huo umewanufaisha sana kwa kuwawezesha kujua mbinu zote zakisasa za kulima zao la maharage.

“Kutokana na FRI, tunapata nafasi ya kuzungumza moja kwa moja na wataalaam kutoka Selian ambao hutusaidia kujua ni lini tuanze kuandaa mashamba; kupanda; mbegu zinazofaa katika maeneo yetu; jinsi ya kupalilia; jinsi ya kuvua na kupunguza upotevu wa baada ya mavuno,” alisema.

Mradi wa Uptake hufanya kazi kwa ushirikiano na radio nane nchini kote.

Vipindi vya radio zote huratibiwa na kituo cha kisasa cha Teknolojia ya Habari na Mawasiliano kinachopatikana katika ofisi za FRI zinazopatikana Arusha.

Kwa mujibu wa afisa wa ubunifu wa kidijitali (digital innovation officer) wa FRI, Bi. Caroline Kimaro, kituo hicho chakisasa kimejengwa kwa mahsusi ya kuwezesha wakulima kupata elimu kwa njia ya radio kutoka kwa wataalam wa kilimo bila wao (wakulima) kutumia gharama za mawasiliano.

“Tulianza na mfumo unaojulikana kwa jina la Telerivet ambao uliwawezesha wakulima kutuma ujumbe mfupi kupitia simu zao za mkononi lakini wao (wakulima) walilipia gharama za ujumbe hu. Ndipo tukaona tuboreshe ambapo tulianzisha mfumo uitwao, ‘Uliza’ ambao huwawezesha wakulima ‘kubipu’ na kusubiri kupigiwa simu kutoka radioni na upate nafasi ya kushauriwa na wataalam,” alisema.

Naye mshauri wa masuala ya teknolojia ya habari na mawasiliano wa FRI, Kassim Sheghembe, alisema mfumo huo (ICT System) hutuma maswali mbali mbali kwa wakulima yakiwepo yale yanayowakumbusha kuanza kwa msimu, magonjwa ya mazao yao, wadudu waharibifu wa mazao na hali ya hewa. “Hivi sasa tunaendela na maboresho ya mfumo ili kuhakikisha kila mkulima anayeuliza swali anapata kujibiwa na mtaalamu,” alisema.



Chanzo: mwananchi.co.tz