Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ramadhan yawaachia kicheko wafanyabiashara

8808 Pic+ramadhani TZW

Tue, 12 Jun 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Wakati waumini wa dini ya Kiislamu wakijiandaa kwa sherehe ya Eid el Fitri wiki hii, wauzaji wa kanzu, baibui na madera wanaeleza kufanya biashara nzuri katika kipindi cha Ramadhani.

Katika soko la Kariakoo jana kulikuwa na msongamano wa watu waliokwenda kujipatia mahitaji. “Sikukuu hiyoo! Na bado zikibaki siku mbili au moja tutakosa pa kusogeza mguu, wenye watoto watakuwa hawawezi kuingia,” alipaza sauti mchuuzi wa nguo zilizokuwa zimetandazwa mezani katika Mtaa wa Congo.

Wanawake wengi walikuwa kwenye maduka yanayouza baibui, madera na hijabu huku wanaume wakiwa maeneo zinakouzwa kanzu.

Mchuuzi wa nguo, Aisha Rajabu alisema tangu kuanza kwa mfungo wa Ramadhani biashara ya nguo imefanyika vizuri tofauti na siku za kawaida. “Kila mtu anataka kujisitiri katika mfungo wa Ramadhani, funga ya mtu inatakiwa iendane na mavazi anayoyavaa ndiyo maana watu wengi hasa wanawake wamekuwa wakinunua madera,” alisema Aisha.

Mchuuzi wa kanzu, Rajabu Kakole alisema huu ni mwezi wenye baraka kwa kuwa biashara yake imekuwa nzuri.

“Huwa nauza kanzu msimu wa Ramadhan na kuelekea sikukuu ya Eid, safari hii biashara imekuwa na wateja wengi,” alisema Kakole.

Alisema huuza kanzu kati ya Sh5,000 na Sh15,000 zikiwamo za watoto.

Chanzo: mwananchi.co.tz