Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Rais Samia azungumza na wafanyabiashara Marekani, yupo boss wa EU

SAMIAAUS Rais Samia akizungumza na wafanyabiashara nchini Marekani

Fri, 24 Sep 2021 Chanzo: Nipashe

RAIS Samia Suluhu Hassan ameshiriki mkutano wa pamoja kati ya wafanyabiashara wa Tanzania na Marekani na kuhimiza kuimarishwa kwa biashara kati ya mataifa hayo mawili ili kuwa na faida kwa pande zote.

Katika mkutano huo uliofanyika jana, Rais aliwaeleza wafanyabiashara hao kuwa kwa sasa biashara zinazofanyika kati ya Tanzania na Marekani ni ndogo kulinganishwa na fursa zilizopo.

Alisema kwa mujibu wa takwimu za mwaka 2019, Tanzania iliagiza bidhaa zenye thamani ya Dola za Marekani milioni 241 na kuuza bidhaa zenye thamani ya dola za kimarekani milioni 46.

Kwa upande mwingine, Marekani imewekeza Tanzania Dola za Kimarekani bilioni 5.55 na kuajiri watu 44,118 wakati Tanzania imewekeza kiasi cha Dola za Kimarekani milioni moja tu ambacho ni kidogo kulinganishwa na ukubwa wa uchumi wa Marekani duniani na fursa zilizopo nchini.

Rais Samia aliwaeleza wafanyabiashara hao kuwa angependa kuona biashara inaongezeka kwa kuwa Tanzania ni mwanachama katika Jumuiya ya Afrika Mashariki(EAC) na pia Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) ambazo zinatoa fursa za wawekezaji na wafanyabiashara wa Marekani kwa soko la watu milioni 450, hivyo kuwa na mazingira mazuri ya uwekezaji.

Vilevile, aliwaeleza wafanyabiashara hao kuwa Tanzania imetia saini mkataba wa Biashara Huru Barani Afrika (AfCFTA) ambao umelegeza masharti ya biashara na kuunganisha soko la watu bilioni 1.3.

Rais Samia pia alikutana na kufanya mazungumzo na Rais wa Baraza la Umoja wa Ulaya (EU), Charles Michel, ambaye alimshukuru mkuu wa nchi huyo kwa kukutana naye na kueleza kuwa lengo lake ni kutaka kupata maoni ya Rais Samia kuhusu mambo manne ya kipaumbele kwa Umoja wa Ulaya kwenye uhusiano wake na Afrika na utayari wa Umoja wa Ulaya kushirikiana na Tanzania kwenye maeneo hayo.

Mambo hayo ni UVIKO-19, Mabadiliko ya Tabia Nchi, Hali ya Usalama Msumbiji na Mapinduzi ya Kidijitali.

Rais Samia aliushukuru Umoja wa Ulaya kwa ushirikiano wake na kuelezea hatua ambazo Tanzania inachukua katika kukabiliana na UVIKO-19, hasa ikizingatiwa kuwa ugonjwa huo umeathiri sekta nyingi ikiwamo ya utalii.

Pamoja na mambo mengine, Rais Samia alieleza hatua mbalimbali ambazo serikali inachukua katika kusambaza miundombinu ya afya ingawa bado kuna vikwazo katika upatikanaji wa vifaa tiba na rasilimali watu na hivyo kuukaribisha Umoja wa Ulaya kuangalia namna ya kushirikiana na Tanzania katika maeneo hayo.

Kuhusu mabadiliko ya tabia nchi, Rais Samia alisema Tanzania ni miongoni mwa nchi zilizoathirika na mabadiliko hayo na inalipa kipaumbele suala hilo katika kukabiliana nalo.

Rais Samia pia alihudhuria mkutano wa kuadhimisha miaka 20 ya tamko la Durban kuhusu kupinga ubaguzi wa rangi na aina zote za unyanyasaji.

Leo Rais Samia anatarajiwa kuhutubia Mkutano wa 76 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa unaoendelea New York, Marekani.

Chanzo: Nipashe