Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Rais Samia azindua upanuzi bandari Kigoma

Bandari Pichjhjh Rais Samia azindua upanuzi bandari Kigoma

Tue, 18 Oct 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Rais Samia Suluhu Hassan ameweka jiwe la msingi kwa ajili ya upanuzi wa bandari ndogo ya Ujiji na Kibirizi mkoani Kigoma.

Mbali na kuweka jiwe hilo la msingi ametaka uongozi wa mkoa huo kushirikiana na wataalamu kuandaa ramani itakayopendezesha eneo la kuingia bandarini ikiwemo kujenga miundombinu mipya ya wafanyabiashara.

Samia ameweka jiwe hilo la msingi leo Jumanne ya Oktoba 18, 2022 ikiwa ni muendelezo wa ziara yake katika mkoani humo ambapo tayari amefanya shughuli mbalimbali ikiwemo uzimaji wa majenereta baada ya Kigoma kuunganishwa na gridi ya Taifa.

Samia amesema wakati akiingia bandari ya Kibirizi hakufurahishwa na sura aliyoiona nje ikiwemo barabara na wafanyabiashara wanaofanya shughuli zao katika eneo hilo.

Amesema tayari ameteta na Waziri wa Ujenzi ili waisaidie Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (Tarura) kujenga barabara inayoingia bandarini hapo.

“Lakini pia sikupendezwa na vibanda nilivyoviona, kwa maana hiyo kuna haja ya mwongozo wa mkoa na wilaya hii, kuliangalia hilo eneo, kushirikiana na wataalamu kupata ramani itakayopendezesha eneo hili la biashara ya kuingia bandarini.

“Ombi langu kwenu wafanyabiashara wa eneo hili, tukubaliane na yale yakayokuja kufanyika, kwa sababu maendeleo ni kuharibu kwanza, lazima tubomoe vibanda vilivyopo, tufanye ramani mpya halafu soko litakalokubaliwa lijengwe, halafu wale walioondoshwa warudishwe,” amesema Samia.

Amesema wakati akienda kutafuta fedha ya kujenga eneo hilo pia wao wakae na umoja wao wa wafanyabiashara wakubaliane jinsi eneo hilo litavyotengenezwa ili mtu atakapotoka bandarini akute wafanyabiashara wakiwa katika maeneo mazuri na wanafanya biashara nzuri.

Kwa mujibu wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), upanuzi wa bandari ya Kibirizi na Ujiji ni sehemu ya mradi mkubwa unaohusisha bandari tatu ikiwemo hiyo ya Kibirizi, Ujiji na bandari kuu ya Kigoma ambako jengo jipya litajengwa.

Katika bandari ya Kibirizi yanajengwa majengo ya kupokea mizigo, abiria na ofisi pamoja na ujenzi wa gati.

Kwa upande wa Ujiji litajengwa jengo la kupokea abiria, kantini huku mradi mzima ukigharimu Sh32 bilioni ambao ulianza mwaka 2019.

Hadi sasa mradi wa Kibirizi umefikia asilimia 69.5 na upande wa Ujiji mradi umefika asilimia 61 huku majengo yakiwa yameshakamilika katika maeneo yote na yanatumika.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live