Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Rais Samia awajengea soko la kisasa Peramiho

H 3 768x576 Rais Samia awajengea soko la kisasa Peramiho

Thu, 7 Jul 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama amesema, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) anajenga soko la kisasa katika Kijiji cha Peramiho ambalo litawahudumia wananchi, kuchangia mapato na ukuaji wa uchumi wa eneo hilo.

Mhe. Jenista amesema hayo, mara baada ya kukagua mradi wa ujenzi wa soko la kisasa la Peramiho linalojengwa na TASAF, akiwa kwenye ziara ya kikazi ya kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF mkoani Ruvuma.

Mhe. Jenista amewakumbusha wananchi wa Peramiho kuwa, wakati akiomba ridhaa ya kuwatumikia walimueleza kwamba kero yao kubwa ni kutokuwa na soko la kisasa hivyo aliwasilisha kero hiyo kwa Mhe. Rais, Samia Suluhu Hassan ambaye aliielekeza TASAF kujenga soko la kisasa Peramiho.

“Ujenzi wa soko hili la kisasa utakamilika kwa wakati na soko hili litachangia mapato na ukuaji wa uchumi hapa Peramiho, hivyo ninaomba tulitunze kwa manufaa na maendeleo yetu,” Mhe. Jenista amesisitiza.

Awali, akitoa taarifa ya ujenzi wa mradi huo wa soko la kisasa, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Songea, Bi. Neema Maghembe amesema kuwa ujenzi wa soko hilo ulianza rasmi tarehe 02 Machi, 2022 na mpaka sasa utekelezaji wake umefikia asilimia 70.

Akizungumzia mchango wa wananchi katika ujenzi wa mradi huo wa soko, Bi. Maghembe amesema kuwa wananchi wametoa mchango wenye thamani ya shilingi milioni 3,778,000/= ambao ni sawa na asilimia 2.2 ya gharama za mradi huo na kuongeza kuwa, kazi walizofanya wananchi wa Peramiho ni kuchimba msingi, kumwagilia maji ukuta, kuchota maji na kuchimba shimo la choo.

Bi. Maghembe amesema, ujenzi wa soko hilo la kisasa unaotekelezwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) kupitia utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini unatarajiwa kukamilika tarehe 15 agosti, 2022 kwa mujibu wa mkataba uliosaniwa.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama amehitimisha ziara ya kikazi ya siku 3 mkoani Ruvuma iliyokuwa na lengo la kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF mkoani humo.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live