Mkulima wa zao la Tumbaku Wilayani Sikonge mkoani Tabora Masoud Kilyamanda amempongeza Rais wa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa jitihada anazozifanya kuhakikisha sekta ya kilimo nchini inanufaisha walengwa.
Miongoni mwa walengwa hao ni pamoja na wanaojihusisha na zao la tumbaku zikiwemo kampuni za ununuzi wa zao hilo yanazidi kuongezeka na kilimo hicho kuonekana chenye tija.
Akizungumza na waandishi wa habari waliomtembelea kwenye mashamba yake yaliyopo vijiji vya Lufwisi katika Kata ya Igigwa , Igagula, Mkulima Kilyamanda amesema anamshukuru Rais Dkt Samia kwa kuruhusu kampuni za nje kuja nchini kununua zao la tumbaku.
Amesema hiyo imewafanya wakulima waanze kuwa na maisha bora na kuendelea kuwa na imani zaidi na Serikali ya awamu ya sita huku akifafanua kama Serikali itaendelea kutoa ruzuku kwenye mbolea wakulima watafanya mabadiliko makubwa ya kimaendeleo hasa Tabora ambako tumbaku linalimwa kwa wingi.
"Hapa kwenye mashamba yangu kuna zaidi ya hekari 300 na nimeajiri vijana zaidi ya 20 na wanalipwa mshahara hapa karibu Sh.milioni 25, hivyo ni uwekezaji mkubwa na ndio maana nashukuru Rais Samia kwa kuweka mazingira mazuri kwenye kilimo.Pia nazishukuru taasisi za fedha kama Benki ya Azania ambao wameniamini na kunikopesha trekta."
Ametumia nafasi hiyo kuziomba taasisi zingine kuwa karibu na wakulima hasa mkulima mkubwa kama yeye wafike kumtembelea waone uwekezaji huo kwani ni imani yake wakiona kwa macho itakuwa rahisi kumkopesha mkulima.
Aidha amesema licha ya kufanya vizuri kwenye kilimo cha tumbaku anatamani pia kufanya shughuli za ufugaji wa samaki hivyo ameiomba Serikali kupitia Wizara ya Kilimo chini ya Waziri Hussein Bashe kumsaidia aweze kupata malambo ya kuhifadhi maji.
Pamoja na shughuli za kilimo anazofanya pia anajihusisha na ufugaji na huko kote amefanikiwa kutoa ajira kwa vijana huku akisisitiza ndoto yake ni kuwa mkulima mkubwa na ataendelea kuajiri kama sehemu ya kuisaidia serikali kutatua changamoto ya ajira.
Kwa upande wake Shija Madowo ambaye naye anajishughulisha na kilimo, ametaja baadhi ya changamoto zinazowakabili wakulima ikiwemo ya ukaushaji wa tumbaku kwani ili ikauke inahitaji kuni au miti ya kuni jambo ambalo wakati mwingine linaleta shida .
Amesema wakati wakukausha tumbaku wamekuwa wakilazimika kulipia fedha senikalini na fedha hizo zimekuwa zikiongezeka badala ya kupungua, hivyo wanapaza sauti zao angalau zipungue."Gharama imeongezeka hadi kufikia 50,000 , ndio maana tunaomba serikali itusaidie."
Aidha amefafanua kilimo cha tumbaku gharama yake ni kubwa hasa kwa upande wa mbolea ambapo mfuko mmoja wa mbolea ni dola 70 mbapo kwa mkulima wa kawaida hawezi kumudu gharama hizo.
"Tunaiomba Serikali iangalie kwenye changamoto za mbolea, tupate ruzuku ya pembejeo ya tumbaku NPK ,kwa kweli tunashukuru kwa upande wa mwaka jana tulipata ruzuku ya mbolea ya kutosha ndiyo maana kwa msimu huu tumevuna mazao ya kutosha,”amesema Madowo.
Ametoa ombi Wizara ya Kilimo kutatua changamoto ya mbolea ya ruzuku ya zao la tumbaku aina ya NPK, na kutumia nafasi hiyo kumwomba Waziri Bashe awasaidie wakulima hao wa zao la tumbaku ili waendelee kulima zao hilo kwa wingi waweze kunufaika.