Rais Samia Suluhu Hassan amewataka wakulima mkoani Mtwara kuwekeza fedha wanazopata baada ya kuuza mazao yao ili kuzitumia katika msimu unaofuata akisema kuwa utaratibu wa kutoa pembejeo na ruzuku hautadumu siku zote.
Ameyasema hayo leo wakati wa kuhitimisha ziara yake ya kikazi kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika Uwanja wa Bomani Masasi, mkoani Mtwara.
“Tupunguze matumizi yasiyo na tija, fedha zile tuziweke. Pembejeo za bure hizi hazitatoka miaka yote. Nia ya kuleta pembejeo za bure ni kuwajengea uwezo wa kiuchumi, mjijenge sasa hivi ili baadaye pembejeo hii haitatoka bure mtanunua tukitambua kwamba mmelima vizuri, mmeuza kwa bei nzuri na mnaweza kununua pembejeo,” amesema.
Aidha, amewaahidi wananchi wa Mtwara kuwa Serikali imedhamiria kufanikisha maendeleo kwenye mkoa huo kwa kuleta miradi mingi ya maendeleo itakayotoa neema kubwa kwa wanachi wa Mtwara.
Hata hivyo, ametoa wito kwa wazazi mkoani humo kuacha kuwacheza watoto wa kike katika umri mdogo kwa kuwa imekuwa chanzo cha mimba za utotoni na badala yake amewataka kutimiza mila hiyo kwa kuwacheza wakiwa kwenye umri wanaojitambua.
Pamoja na hayo, Rais Samia amewataka viongozi anaowateuwa kumwakilisha vizuri kwenye maeneo yao kwa kusikiliza na kutatua kero na changamoto za wananchi.