Rais Samia Suluhu Hassan amesema imefika wakati kwa nchi za Afrika Mashariki kuendeleza viwanda vya ndani katika kuzalisha bidhaa ili kupunguza uagizaji wa bidhaa hizo ikiwemo nguo kutoka nje ya nchi.
Rais Samia aliyasema hayo katika sherehe ya ufunguzi wa kiwanda cha nguo cha Basra Textile Mills Limited huko Chumbuni Unguja ikiwa ni shamrashamra za maadhimisho ya miaka 58 ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Alisema matarajio ya Watanzania ni kuona siku zijazo hawalazimiki tena kuagiza nguo kutoka nje hasa nguo za watoto na bidhaa hizo zitaweza kusafirishwa katika soko la Afrika Mashariki, SADEC na masoko ya kimataifa kwani na fursa nzuri kwa Zanzibar kutumia masoko hayo.
Alisema takwimu zilizokuwepo zinaonesha kwamba Zanzibar inapokea kanga vikoi na vitenge zaidi ya bilioni 3,000 ambavyo viliingia katika soko la Zanzibar kwa mwaka 2021.
"Hizo ni pesa nyingi kuzipeleka nje kununua bidhaa hivyo wakiwezesha kuzalisha vizuri hapa ndani basi fedha hiyo itabaki na itatumika kwa mahitaji mengine ya wananchi," alisema. Rais Samia alipongeza uamuzi wa serikali kwa kukubali mradi huo ambao sahihi kwa maendeleo ya wananchi wa Zanzibar na taifa kwa ujumla kwani kampuni hiyo ni zoefu katika uzalishaji wa nguo. Akizungumzia awamu ya pili ya utekelezaji wa mradi huo wa ujenzi wa kiwanda cha ushonaji wa nguo alisema ni matarajio kwamba mradi huo utatekelezwa katika kipindi kilichopangwa.
Alitoa wito kwa vyuo vya mafunzo ya Amali na vyuo vyote vinavyofundisha ushoni nchini kuiona fursa hiyo na kufundisha kwa bidii ili kiwanda hicho kitakapokamilika basi vijana waweze kuwa na sifa zinazotakiwa na kuweza kuajirika katika kiwanda hicho.
Alisema uzoefu unaonesha kwamba nchi nyngi za Asia na hata nchi nyengine za Afrika, wengi wanaoajiriwa katika viwanda hivyo ni kinamama hivyo ni fursa ya ajira kwa wanawake wengi na kuwasisitiza kusimamia fani ya ushoni ili iweze kuwakomboa kimaendeleo.
“Hii ni fursa ambayo serikali imewaandalia vijana wa kike nawaomba nanyi mjitayarishe kuipokea ajira hiyo,” alisema. Alisema kiwanda hicho pia kinaweza kutumia fursa ya soko lilikuwepo Marekani na kuwataka watendaji wa wizara kukisimmamia kiwanda hicho ili kufikia masoko hayo kwa kuzalisha bidhaa zenye viwango.
Hata hivyo, Rais Samia alisema awamu ya tatu ya mradi huo ni upanuzi wa kiwanda kwa kuongeza majengo mengine kwa ajili ya kuchakata pamba ambayo itaweza kutumika ndani ya nchi na kutoa bidhaa tofauti tofauti.
Alisema hiyo ni fursa nzuri kwani hawasafirishi ajira na njia hiyo itasaidia kuuza ajira ndani ya nchi na pia kuwezesha pamba kupanda bei kwa mkulima.
“Tunafanya mapinduzi ya kisera sheria kwa mawazo kwa maendeleo ya watu na mambo haya ndio mapinduzi tunayozungumzia na mradi huu ni mkombozi kwa wakulima na hata kwa vijana katika kupata ajira,” alibainisha.
Aliwashauri wawekezaji kuharakisha mradi huo kwa maeneo yaliyobakia na kuweza kupata tija kwa haraka zaidi na kufika wakati kama nchi kuacha kuagiza vitambaa, nguo vitenge na vitu vyengine.
Mbali na hayo aliwasisitiza vijana waliobahatika kuajiriwa katika kiwanda hicho kubadilika na kujua ajira ndio nguzo ya maisha kwa kufuata maadili ya kazi,uadilifu, heshima na weledi mkubwa ili kuwapa nguvu wawekezaji kuendelea kuwaamini.
Sambamba na hayo, aliwataka waajiri kutimiza masharti ya mikataba wanayoingia na wafanyakazi ili wanafanya wajibu wao kuhakikisha kila mmoja anapata maslahi yake.
Mbali na hayo, aliitaka Wizara ya Biashara ya Zanzibar kukaa pamoja na Wizara ya Tanzania bara kuzungumza changamoto zinazoikabili kiwanda hicho ili kuondosha vikwazo na kuona pande zote mbili za muungano ziweze kufanya biashara na maendeleo yaweze kupatikana kwa wananchi wote.
Mapema Waziri wa Biashara na Maendeleo ya Viwanda Zanzibar Omar Said Shaaban alisema sekta ya viwanda ni sekta ya mafanikio na maendeleo ya kiuchumi katika nchi nyingi duniani.
Alisema serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imechukua jitihada za kuhakikisha inakuwa kiviwanda kwa kufaya marekebisho ya sheria mbalimbali ili kuweka kivutio katika sekta ya viwanda na uchumi wa bluu kwa kufufua viwanda hivyo ikiwemo kiwanda cha sukari mahonda, kiwanda cha viatu na kiwanda hicho Juma Hassan Reli, akisoma risala kwa niaba ya muwekezaji wa kiwanda hicho, alisema mradi huo hadi kukamilika kwake unatarajia kugharimu Sh115 bilion ambapo ukikamilika utaweza kuzalisha mita 250,000 za vitambaa vya pamba na polisa vyenye ubora wa kimataifa kwa siku ambayo ni sawa na mita 7.5 milioni kwa mwezi.
Alisema kiwanda hicho kinakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo gharama za usafirishaji wa makaa ya mawe, gharama kubwa ya umeme katika kuendesha kkiwanda hicho na bidhaa zinazozalishwa na kiwanda kutopata soko la uhakika.