Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE), kimeandaa kongamano la maendeleo ya biashara na uchumi ambalo linatarajaiwa kufunguliwa na Rais wa Zanzibar Dk. Hussein Ali Mwinyi mkoani Dodoma.
Hayo yalisemwa jana chuoni hapo na Mkuu wa chuo hicho, Profesa Emmanuel Mjema, wakati akizungumzia kongamano hilo litakalofanyika tarehe 15 na 16 mwezi huu kwenye ukumbi wa mikutano wa Jakaya Kikwete mkoani humo.
Alisema kongamano hilo linakauli mbiu ya ‘Biashara Uwekezaji na Ubunifu kwa Mabadiliko ya Kiuchumi na kwamba kutokana na umuhimu wake viongozi mbalimbali wa Tanzania bara na visiwani watashiriki kongamano hilo.
Profesa Mjema alitaja mada zitakazojadiliwa kwenye kongamano hilo kuwa ni pamoja na Biashara ya ndani na kimataifa, Uwekezaji wa moja kwa moja wa kigeni, Ubunifu na Ujasiriamali, Uwezeshaji wa Biashara na Ushirikiano wa Kiuchumi, uwekezaji na Teknolojia, Uchumi wa Buluu, Zuia mnyororo na Fedha za kidijitali
Profesa Mjema alisema lengo la mdahalo huo wa Kitaaluma ni kujenga uwezo na mitandao miongoni mwa watafiti na wadau wengine barani Afrika na kutoa fursa ya kuleta maendeleo ya kiuchumi kupitia biashara na kwamba kongamano hilo litasaidia kuleta ufahamu mpya katika tasnia mbalimbali.
Pia Profesa Mjema alisema kutakuwa na mahafali ya 57 ya CBE ambapo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Waziri Mkuu Kassim Majaliwa Novemba 12 mwaka huu katika kampasi ya Dar es Salam ambapo kutakuwa na wahitimu wa Shahada ya Uzamili, Stashahada ya Uzamili, Shahada ya Kwanza, Stashahada na Cheti cha Ufundi.
Alisema wiki ya Makongamano kwa Kampasi zote shughuli zitaanza Jumatatu hadi Alhamis ambayo itakuwa ni siku ya kilele na kwamba katika wiki hiyo shughuli mbalimbali kama vile mawasilisho ya machapisho, maonesho ya Idara za Kitaaluma ambayo yawahusisha wahitimu wa zamani yaani CBE Alumni ambao wanakaribishwa kuonesha bidhaa na huduma wanazozifanya.
“Pia semina na warsha kuhusu mambo mbalimbali ya biashara zitawezeshwa bila gharama yoyote na katika mahafali hayo ya 57 katika Kampasi zetu zote takribani Wahitimu 2,000 watatunukiwa stahiki zao katika ngazi tofauti tofauti,” alisema Profesa Mjema