Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Rais Mwinyi awaita Warusi kuwekeza Zanzibar

Wawekezaji Urusiiiii Rais Mwinyi awaita Warusi kuwekeza Zanzibar

Thu, 2 Feb 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Rais wa Zanzibar Dk Hussein Mwinyi, ameiomba Serikali ya Urusi kuisaidia Zanzibar kwenye sekta za Afya, Utalii na Uchumi wa Buluu.

Dk Mwinyi alitoa ombi hilo jana Jumatano Februari Mosi, 2023 Ikulu, Zanzibar wakati akizungumza na Balozi wa Urusi nchini Tanzania, Andrey Avestisyan.

Dk Mwinyi amemueleza Balozi Avestisyan kwamba Serikali ya Zanzibar imeimarisha sekta ya afya kwa kujenga hospitali kubwa za wilaya na mikoa, hivyo akaomba ushirikiano wa kupatiwa madaktari bingwa kwenye hospitali hizo sambamba na fursa ya madaktari wa Zanzibar kwenda Urusi kwa ajili ya kuongeza ujuzi.

“Tumejenga hospitali nyingi za wilaya na mikoa ambazo zinahitaji wataalamu watakaotoa huduma zinazoendana na gharama za miundombinu,”alisema Dk Mwinyi.

Akizungumzia sekta ya utalii, Dk Mwinyi alimueleza balozi huyo kuwa Zanzibar ina fursa nyingi na vivutio adhimu, hivyo alimuomba kuangalia uwezekano kwa kuleta watalii wengi zaidi pande zote mbili zinufaike na fursa hizo.

Amesema Zanzibar imejaliwa visiwa vizuri vyenye mvuto kwa utalii na ardhi kwa ajili ya uwekezaji wa sekta hiyo, pamoja na Mji Mkongwe ambao ni kivutio adhimu kwa wageni, hivyo alimkaribisha Balozi Avestisyan kuitumia fursa hiyo kuwakaribisha Warusi wengi nchini kujionea tunu za Visiwa vya Zanzibar.

Kwa upande wa Sekta ya Uchumi wa Buluu, Rais Mwinyi amesema Zanzibar ina uwanda mpana katika uwekezaji hivyo wanawakaribisha kuwekeza kisiwani humo.

Naye Balozi Andrey Avestisyan, amesema kuna ushirikiano wa muda mrefu baina ya mataifa hayo mawili.

Amesema tayari wameanza mazungumzo na nchi yake kuangalia namna ya kuweka ubalozi mdogo wa nchi hiyo Zanzibar ili iwe rahisi kwa wawekezaji watakaoshawishika kwenda kuwekeza katika kisiwa hicho.

Amesema Warusi wengi wana utaalamu mkubwa wa kusarifu masuala ya uvuvi na matunda ya bahari na kueleza kwamba eneo hilo watalichukulia kwa umuhimu wa pekee katika kuimarisha sekta hiyo kwa uchumi wa Zanzibar na kuboresha diplomasia.

Amesema katika kudumisha ushirikiano uliopo baina ya Urusi na Zanzibar, itapendeza zaidi kuanzisha safari za ndege za moja kwa moja baina ya Urusi na Zanzibar hali aliyoieleza itasaidia Warusi wengi kuja kutalii Zanzibar na kuvutiwa na mandhari mwanana ya upepo wa visiwa.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live