Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Rais Mwinyi ataka maboresho teknolojia ya nyuklia

Rais Mwinyi Awaka.jpeg Rais Mwinyi ataka maboresho teknolojia ya nyuklia

Fri, 17 Feb 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Hussein Mwinyi amesema sayansi na teknolojia ya nyuklia itainua na kuimarisha uchumi wa Zanzibar kwa kuongeza kasi ya ukuaji wa sekta za kilimo, mifugo, nishati na afya.

Akiweka jiwe la msingi katika mradi wa ujenzi wa ofisi na maabara za Tume ya Nguvu za Atomiki Tanzania iliyofanyika Dunga kisiwani Unguja, Rais Mwinyi amesema matumizi ya teknolojia ya nyuklia yameleta mafanikio makubwa visiwani Zanzibar baada ya kutokomeza wadudu aina ya mbung’o ambao walikuwa wakiathiri sana afya na uzalishaji wa mifugo hususani ng’ombe.

Mbali na hilo, Dk Mwinyi alisema teknolojia ya nyuklia visiwani humo imewezesha upatikanaji wa mbegu bora za mpunga aina ya “SUPA BC”, yenye sifa ya kustahamili ukame na maradhi.

“Matokeo yake kwa sasa mkulima anaweza kupata tani saba badala ya tani nne za awali kwa hekta moja huku muda wa kuvuna toka kupanda ukipungua hadi siku 120 kutoka siku 150 za awali. Kwa hakika haya ni mafanikio makubwa ya kujivunia,” alisema.

Aliongeza kuwa Zanzibar itanufaika pakubwa kutokana na mpango wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kupitia Tume ya Nguvu za Atomiki Tanzania, wa kufadhili vijana wa Kitanzania kwenda kusoma masuala ya sayansi na teknolojia ya nyuklia katika vyuo bora duniani.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live