Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Rais Magufuli anaendelea kuitoa dunia tongotongo

29cbb05dd1764e4db050d6ac937e2d6f.jpeg Rais Magufuli anaendelea kuitoa dunia tongotongo

Wed, 17 Mar 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

TANGU aingie madarakani, Rais John Magufuli amekuwa akifanya mambo mengi kwa utulivu na umahiri mkubwa kiasi cha kuwashangaza wengi.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Hassan Abbas ambaye pia ni Msemaji Mkuu wa Serikali, amepata kusema mara kadhaa kwamba ukitaka kupinga kile aliochoamua kukifanya Rais John Magufuli usikurupuke.

Kwamba unatakiwa kujipanga sana na kuwaza sana na hata kufanya utafiti kwani ukicheza, mwisho wa yote utaumbuka wewe.

Nitoe mfano wa pale Rais alipoamua kuwashughulikia wafanyabiashara ‘wakubwa’ kuhusu sakata la makinikia, wapo waliokurupuka wakisema mengi sana.

Walisema Tanzania itashtakiwa kwenye mahakama za kimataifa, Tanzania itatengwa na wawekezaji, Tanzania itakuwa hivi au vile na mengi mfanoa wa hayo lakini mwanaume alikuwa ametulia akijua anachokifanya na mwisho wa siku wakabaki wameumbuka. Nchi sasa inasonga mbele ikinufaika vilivyo na raslimali zake.

Hata alivyosema serikali yake haitaruhusu wasichana waliopewa mimba kurudi shule za serikali wapo waliopiga makelele hadi kufanya majaribio ya kutaka nchi inyimwe misaada lakini mwisho wa siku ni yeye aliyeibuka mshindi kwa kutoa maono yenye kufaa.

Hata alipokuwa akihimiza watanzaia kuachana na uzazi wa mpango amepingwa sana lakini sasa ni dhahiri kwamba kumbe ni mbinu za mabeberu kuhakikisha waafrika hawaongezeki na kusababisha kuhitaji raslimali nyingi tulizo nazo ambazo Wazungu wanazitegemea pia!

Hebu, katika muktadha huo, tuzungumzie kidogo janga la ugonjwa wa homa kali ya mapafu unaosababishwa na virusi vya corona (Covid-19) na namna misimamo na maneno ya Rais Magufuli yalivyotia fora kwenye janga hili.

Jamani tuache utani, huyu mwanaume kutoka Chato anaendelea kuitoa matongotongo dunia kwa msimamo aliochukua mpaka sasa kwenye hili janga la corona. Yaani kila anachokizungumza kinatokea na kuiamsha dunia.

Alianza kwa kuweka msimamo kwamba hatawafungia watu ndani kama zilivyofanya nchi nyingine wakiwemo majirani zetu, lakini akasema atapambana na ugonjwa huu kisayansi na kumtanguliza Mungu.

Watanzania tulisemwa na kutabiriwa kwamba tutegemee kuokota maiti zilizozagaa barabara lakini wapi! Tukawa nchi ya kwanza kama sikosei katika eneo la hili la Afrika kufunga mawodi kwa kukosa wagonjwa wa corona, lakini wale waliofungiana kila siku taarifa za wagonjwa wapya zikirindima!

Unakumbuka alivyoisihi dunia kuizoea corona na kujifunza kuishi na huu ugonjwa kama watu walivyozoea magonjwa mengine yaliyokuwa tishio huko nyuma kama surua, ukimwi, maleria na mengine?

Wengi walimshangaa lakini muda mfupi baadae Shirika la Afya Duniani (WHO) kupitia kwa mtaalamu wake wa masuala ya dharura, Michael Ryan, akaafiki mawazo ya Rais Magufuli.

Akaitaka dunia nzima kuuzoea ugonjwa wa corona kwamba haukuwa wa kupita na hivyo kujifunza kuishi nao na kuacha kubashiri lini ugonjwa huu utaisha.

Likaja suala la vifaa vya kupima corona. Wakati dunia nzima ikiwa kwenye usingizi mzito wa kuripoti maelfu kwa maelfu ya visa vya corona, Dk Magufuli akaamua kuvifanyia majaribio hivi vipimo vya corona kama kweli vinatoa majibu ya kweli au vina janjajanja ndani yake.

Akachukua sampuli za mapapai, ndege, mbuzi na zingine zisizokuwa binadamu bila wapimaji kujua na kuzipeleka maabara. Cha kushangaza eti mapapai yakatoa majibu chanya (positive) kwamba yana corona, jambo lililoshangaza wengi na kuuamsha ulimwengu mzima kuhusu usahihi wa vifaa vya kupima corona.

Hapo hapo dunia ikaamka kwamba baadhi ya vipimo hivi vya corona vilikuwa vina matatizo sana na inawezekana kabisa vilikuwa havitoi majibu sahihi.

Kwamba inawezekana pia wapimaji walikua na ‘jambo lao’ na pengine walikuwa na mwafaka fulani na mabeberu ambayo kila siku huwa na mbinu nyingi chafu hususani katika nchi zetu hizi za Afrika.

Hii maana yake ni kwamba kuna watu wengi walioambiwa wana corona kumbe inawezekana kabisa hawakuwa na tatizo hilo na inawezekana kabisa watu wengi sana walipoteza maisha yao kwa kihoro na hofu kwamba wamekumbwa na corona kwa sababu tu ya vipimo kutowaambia ukweli.

Kumbuka watalaamu wanasema kuna wakati mwingine hofu inaua haraka kuliko ugonjwa wenyewe.

Baada tu ya Rais Magufuli kuona shida hiyo ya vipimo vya corona, dunia nzima ikaamka na tukaona Nigeria, China, Marekani wakiripoti shida hii ya vifaa vingi ya vya kupima corona kutotoa majibu sahihi.

Ikawa ndio habari ya ulimwengu na dunia nzima, watu wakimjadili huyu Mwafrika aliyegundua kwamba vipimo vya corona vina shida. Akili kubwa sana hii.

Sasa tunasikia kuhusu chanjo ya corona inayopigiwa debe sana na kuanza kusambazwa maeneo mbalimbali ya dunia kwamba pia ni tatizo.

Hii ndiyo chanjo ambayo Rais Magufuli aliitilia shaka toka mwanzo na kuitaka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kuwa makini sana nayo.

Akasema ni vyema kabla ya kuikurupukia tukajiridhisha nayo na ikiwezekana kuachana nayo kabla ya wizara yenyewe ya afya kutoa msimamo wa kutokuwa tayari kupokea chanjo ya corona.

Leo ndani ya wiki chache tangu Dk Magufuli kuitahadharisha nchi na dunia kuhusu chanjo hii ya corona tumeshuhudia ulimwengu mzima ukiitilia shaka.

Baadhi ya nchi zimeamua kusitisha kabisa utoaji wa chanjo ya corona baada ya kudhihirika kwamba tayari katika maeneo mengi duniani imeleta maafa na majanga makubwa kwa kuchukua uhai wa watu.

Tangu kuanza kupigiwa debe chanjo hiyo, tumeshuhudia, chanjo feki zilizotengenezwa na makampuni feki na matapeli pia zikikamatwa na kuanza kusambazwa hasa Afrika.

Chanjo hizo zikiwemo feki zimeondoka na uhai wa watu baada tu ya kuchanjwa na kwingine chanjo hiyo ikisadikika kugandisha damu mwilini.

Tayari mataifa makubwa yamesitisha chanjo hizo za corona ambazo zimeonekana kuwa na matatizo matupu.

Hapa Afrika mataifa ya Afrika Kusini, Congo na mengine hayataki hata kusikia chanjo hiyo.

Yanayotokea kwenye chanjo hii ni yale yale ambayo yalishatolewa tahadhari na Rais Magufuli toka mwanzo wakati chanjo hizi zinaanza kupigiwa debe.

Rais Magufuli pia alielezea kuhusu kuwa makini na barakoa zinazotoka nje. Hazikupita siku nyingi yakakamatwa na marundo na marundo ya barakoa feki nchini Marekani zikitokea China!

Kwa ufupi, katika suala la afya na mengine yanayofanana na hayo, Rais Magufuli ametoa somo kubwa kwa dunia na hususani Afrika kwamba hatutakiwiki kukurupuka na kupokea kikasuku kila wanachotutaka watu wa Magharibi na Marekani.

Kwamba tukifanye kwa kutulia, kuchunguza na ikiwezekana tukifanye kwa kuangalia mazingira yetu. Kama wao uchumi wao unawaruhusu kufungiana ndani, lazima tuangalie kama kwetu kufungiana kuna tija au tunaweza kuwa na mbinu mbadala hata kama ni kuacha wachache miongoni mwetu wapoteze maisha.

Mwandishi wa makala haya ni mchangiaji wa gazeti hili. Mawasiliano yake ni 0657475347

Chanzo: www.habarileo.co.tz