Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Raha ya mwendokasi iliyogeuka shubiri

19997 Pic+mwendokasi TanzaniaWeb

Mon, 1 Oct 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Mradi wa mabasi yaendayo haraka wa jijini Dar es Salaam, Dart ulionekana kuwa mkombozi wa gharama za usafiri kwa wakazi ambao wanaishi maeneo ulikopitia.

Usafiri wa uhakika kuwahi ofisini au katika shughuli nyingine, nauli nafuu, usalama vituoni na ndani ya mabasi na utaratibu mzuri wakati wa kupanda ulisababisha hata wenye magari binafsi, kudiriki kuyaacha majumbani au kwenye maegesho karibu na vituo vya mabasi.

Ahadi kwamba jitihada zilikuwa zikifanyika kuboresha zaidi huduma hiyo, zilituliza wengi na kujenga imani kuwa adha ya usafiri wa umma, sasa inakaribia kupata suluhisho.

Lakini sasa, huduma hiyo imegeuka shubiri. Sasa, wizi uliokuwapo enzi za mabasi ya Uda pekee umerejea, msongamano ndani ya mabasi umerejea, uhakika wa usafiri si mkubwa kama ilivyokuwa awali na hakuna shaka kuwa baadhi ya walioamua kupumzisha magari yao binafsi sasa wameghairi, kwa mujibu wa uchunguzi uliofanywa na Mwananchi.

“Watu hawaoni tofauti ya usafiri wa daladala na mwendokasi,” alisema msemaji wa kampuni ya mabasi yaendayo haraka ya Udart, Deus Bugaywa alipozungumza na Mwananchi kuhusu mabasi 70 yaliyozuiwa kutoka bandarini kusubiri kibali cha Dart.

“Mabasi (yaliyopo) yanaharibika mara kwa mara kwa kuwa yanabeba abiria kupita uwezo wake.”

Kwa mujibu wa Udart, mradi huo ulianza na mabasi 140 na ulikuwa ukihudumia abiria 50,000 lakini ongezeko la watu jijini Dar es Salaam limesababisha abiria kuongezeka hadi kufikia kati ya 150,000 na 200,000 ambao wanahudumiwa na idadi ileile ya mabasi.

Wakati Dart ikisema waendeshaji mradi huo hawajakamilisha taratibu zitakazowezesha kuyatoa mabasi hayo na kuyaingiza barabarani, Udart inasema imeshakamilisha taratibu zote na inachosubiri ni ridhaa ya wamiliki wa mradi na kwa kipindi cha miezi minne sasa, danadana zimekuwa ni hizohizo.

Ni wazi kuwa mabasi hayo kwa sasa hayatoshelezi mahitaji ya watu jijini Dar es Salaam ambao takwimu za mwaka 2012 zinaonyesha walikuwa milioni 4.36 na wanaongezeka kwa kiwango cha asilimia 5.6.

Hivi sasa abiria wanalazimika kutumia nguvu, hasa nyakati za asubuhi na jioni, kuweza kuingia ndani ya mabasi badala ya utaratibu uliokuwapo awali wa kupanga foleni.

Bila kufanya hivyo, abiria anaweza kujikuta anakaa kituoni zaidi ya saa moja akisubiri walau kupata mahali pa kuweka mguu katika usafiri huo ambao ulidhaniwa kuwa mkombozi kwa wakazi wa Dar es Salaam baada ya kuteseka kwa muda mrefu na usafiri wa mabasi binafsi.

Kwa mujibu wa uchunguzi wa Mwananchi, vituo ambavyo abiria hulazimika kukunja misuli ili kupata huduma hiyo muhimu ni Kimara Mwisho, Gerezani, Msimbazi A na B na Kivukoni.

Kwa wale wakazi wa Kimara, Mbezi na maeneo ya jirani hulazimika kuyafuata vituo vya Kibo na Korogwe na kuyapanda hadi Kimara Mwisho na kugeuza nayo.

“Mabasi yanaharibika mara kwa mara kwa kuwa yanabeba abiria wengi kupita uwezo wake,” alisema Bugaywa.

Alisema abiria wanalazimika kusimama kituoni kwa muda mrefu kusubiri usafiri kwa kuwa mara nyingi mabasi hupita yakiwa yameshajaa.

Hali hiyo ya uchache wa mabasi inawafanya wakazi kusubiri mabasi hayo kwa muda mrefu na yakifika hugombea na hivyo kutoa mwanya kwa wahalifu kutumia hali hiyo kuibia abiria.

Katika uchunguzi wake wiki hii, Mwananchi ilishuhudia abiria wakigombea kuingia katika usafiri huo na siku chache zilizopita mwandishi wa gazeti hili aliibiwa akiwa katika moja ya mabasi hayo.

Si wezi pekee wanaoongeza kero katika usafiri huo, wakati mwingine milango ya mabasi hayo hugoma kufungika kutokana na uwingi wa abiria na wakati mwingine abiria hulazimika kujibana zaidi ili kuruhusu mlango kujifunga.

“Hali ya usafiri ni ngumu na ili usichoke sana inabidi upande basi la express (haraka) ambalo husimama vituo vichache na hata kama umesimama huchoki sana,” alisema mkazi wa Kimara aliyejitambulisha kwa jina moja na Jovither.

Mkazi mwingine, Deus Kanze alisema usafiri huo umekuwa kero.

“Ni bora tu wakaleta mabasi mengine au kurejesha daladala kwa wingi maana haya sasa yamekuwa kero. Watu tunakaa zaidi vituoni na yanajaza kupita kiasi. Kwa kweli tunapoteza muda mwingi njiani,” alisema Kanze.

Pia, viti ambavyo vimetengwa kwa ajili ya watu wa makundi maalumu kama wazee, wajawazito na walemavu, kwa sasa havitumiki kama ilivyokusudiwa.

Wengi wanaona sehemu hizo ndizo za kukimbilia kuepuka msongamano na kukanyagana kwenye maeneo ya kusimama. Mwananchi ilishuhudia dereva wa moja ya mabasi hayo akiwanyanyua watu walioketi eneo hilo, ili kuwaruhusu walemavu na mjamzito mmoja kuketi.

Kimbilio la wengi kupata usafiri huo na kukaa kwenye viti ni kituo cha Fire ambako mabasi yanayofanya safari kati ya Kivukoni na Kimara, Kivukoni-Moroco, Moroco-Gerezani, Kimara -Gerezani, au Gerezani Muhimbili lazima yapite.

Anayeenda Kimara hupanda basi kituo hicho na kwenda kugeuza nalo Gerezani au Kivukoni.

Gazeti la Mwananchi limebaini kuwa wanaopata tabu zaidi ya kuzunguka na mabasi ni wanaokwenda Kimara. Wanaotokea maeneo ya Karikoo huyafuata mabasi hayo kituo cha Fire kuzunguka nalo, wakati wanaotokea Kivukoni huyafuata kituo cha ni DIT na kile cha Jiji.

Wizi unavyofanyika

Msongamano huo kwenye mabasi hayo ni fursa kwa wezi.

Alhamisi iliyopita mwandishi wa Mwananchi, aliyekuwa mmoja wa timu iliyokuwa ikifanya uchunguzi wa adha ya usafiri wa Udart, alionja shubiri katika moja ya mabasi hayo baada ya kuibiwa simu yake ya mkononi.

Basi hilo lilikuwa limejaa kupita kiasi, lakini cha kushangaza kila kituo dereva alikuwa akisimama kuchukua abiria na kuzidisha wingi wa watu.

“Nilikosa kiti hivyo nikalazimika kusimama,” alisema mwandishi wetu. “Nilikuwa nimezungukwa na vijana wawili ambao walikuwa wakizungumzaa taarifa za kuzama kwa kivuko cha Mv Nyerere. Mara baada ya kushuka kuna mwanamke mmoja akalalamika kwamba ameibiwa simu na fedha zilizokuwa kwenye mkoba wake ambao ulikatwa kwa ustadi na kitu chenye ncha kali ambacho nahisi ulikuwa wembe.”

Mwandishi wetu alisema mama mmoja alibainisha kuwa walioiba ni wale vijana waliokuwa wanapiga makelele kuzungumzia kivuko kilichozama kwa kuwa hukutana nao kila mara na lazima asikie mtu analalamika kuibiwa.

Alisema staili yao ni hiyohiyo ya kuanzisha gumzo ili kuwazubaisha abiria.

“Nilipofika Posta ya zamani nikajigundua kwamba na mimi nimeshaibiwa simu pamoja na hela zilizokuwa kwenye mfuko wa suruali,” alisema mwandishi wetu.

“Sikutaka kujiuliza maswali nikahisi tu kwamba ni walewale vijana waliokuwa wananipigisha stori za Mv Nyerere.”

Uchache wa mabasi

Ni wazi kuwa kupungua kwa ubora wa huduma hiyo kumesababishwa kwa kiasi kikubwa na kutoongezeka kwa idadi ya mabasi kulingana na kasi kubwa ya ongezeko la watu jijini Dar es Salaam na matumizi ya mabasi hayo.

Mmoja wa wakazi wa Dar es Salaam, Kassim Haji alisema anashangazwa kuona mvutano baina ya Udart na Dart ukiendelea bila mamlaka za juu kuingilia kati.

Haji alisema lazima kuna kitu kinaendelea kati ya Dart na Udart, ila hawataki kukiweka wazi, hivyo ni vyema Rais John Magufuli akaingilia suala hilo ili mabasi hayo yatolewe na abiria wapate ahueni ya usafiri.

“Wakazi wa Kimara tunayatamani sana hayo mabasi kwa kuwa tunapata tabu asubuhi na jioni kujazana kwenye mabasi kama kuku, wakati kuna mabasi 70 yanaozea bandarini. Hii haikubaliki,” alisema. “Rais aseme neno kutuokoa sisi wanyonge tunaotegemea usafiri huu. Kama kuna magumashi basi yaagizwe mengine haraka.”

Mkazi mwingine, Aisha Kaniki alisema wanawake wamekuwa wakipata tabu kugombea magari hayo ikilinganishwa na wanaume na hivyo kujikuta wakikaa muda mrefu vituoni.

“Yaani kwa kweli usafiri huu hauna tofauti na daladala. Tofauti inakuja kwenye muda wa kufika tu kwa kuwa hayakai foleni,” alisema Aisha.

“Kwenye kupanda kwa sisi wanawake ni mateso, labda uwe na nguvu. La sivyo usubiri hadi watu wapungue hususani hapa katika kituo cha Kimara.”

Batuli Amri, mkazi wa Mbezi alisema kwa sasa kuna afadhali kidogo kwa kuwa awali watu walikuwa wakipoteza fahamu na kudondoka kwa kukosa hewa au kubabana ndani ya basi na wakati mwingine vituoni.

Wakati huduma ya usafiri ikionekana kulemewa na idadi ya watumiaji, baadhi ya mabasi huonekana yakiwa yameegeshwa ofisi za Udart badala ya kuingizwa barabarani kusaidia kuondoa msongamano.

Lakini mmoja wa madereva ambaye hakutaka jina lake litajwe gazetini alisema kuegeshwa kwa baadhi ya mabasi wakati a mchana hutokana na ratiba ilivyopangwa na uongozi wa Udart.

“Wanachoona (viongozi) ni kuwa unaweza kuruhusu mabasi mengi kwa wakati mmoja, halafu ukakuta yote yamekwama sehemu moja,” alisema.

Alisema hilo linatokana na ukweli kuwa wanaoruhusu magari maeneo mengi ni trafiki na sio taa na hiyo ndio maana baadhi huegeshwa kwanza.

Wakati hali ikiwa hivyo, watumiaji wa usafiri huo kati ya Gerezani na Kimara na wale wa Morocco wanasema uchache wa mabasi umezidi maeneo yao.

Chanzo: mwananchi.co.tz