Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

RIPOTI YA BENKI YA DUNIA: Umaskini wapungua kwa kasi ndogo

87583 Pic+umaskini RIPOTI YA BENKI YA DUNIA: Umaskini wapungua kwa kasi ndogo

Sun, 8 Dec 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dodoma. Kwa muongo mmoja uliopita kiwango cha umaskini nchini kimeendelea kupungua ingawa kasi ya upunguaji huo ni ndogo.

Hayo yalibainishwa katika Ripoti ya Tathmini ya Hali ya Umaskini Tanzania Bara iliyotolewa juzi na Benki ya Dunia (WB).

Ripoti hiyo inaonyesha kati ya mwaka 2007 hadi mwaka 2018 kiwango cha umaskini kimepungua kutoka asilimia 34.4 hadi asilimia 26.4.

Ripoti hiyo, ambayo imezinduliwa na Waziri wa Viwanda na Biashara, Innocent Bashungwa pia inaonyesha kuwa kuimarika kwa maisha na vipato vya watu kumechangia kupungua kwa umaskini.

Mkakati wa Serikali katika matumizi ya umeme wa jua umeleta mafanikio ambapo asilimia 33 ya kaya zinazoishi vijijini zinanufaika na nishati hiyo kwa ajili ya kupata mwanga ikilinganishwa na asilimia 14 ya kaya za mijini. “Takwimu zinaonyesha kuongezeka kwa kiwango cha upatikanaji huduma muhimu na kuongezeka kwa pato la watu,” ilisema sehemu ya ripoti hiyo iliyowasilishwa na Mchumi Mwandamizi wa WB, Rob Swinkels.

Licha ya kuwa na mikakati ya na mafanikio ya kupunguza umaskini nchini lakini kupungua huko hakuendani na kasi ya ongezeko idadi ya watu.

Hali hiyo inatajwa katika ripoti hiyo kuchangia ongezeko la watu maskini hadi kufikia milioni 14 kutoka milioni 13 wa mwaka 2007 ambao inadaiwa wanaishi chini ya kiwango cha Taifa cha umaskini cha Sh49,320 kwa mtu mmoja kwa mwezi.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, upunguaji umaskini nchini unatajwa kutoakisi ukuaji wa uchumi.

Ripoti hiyo pia inazungumzia upatikanaji wa ajira ambao unakua kwa kiwango cha chini sambamba na mabadiliko ya kiuchumi huku viwanda na huduma zinakuwa kwa kasi zaidi kuliko kilimo ambako idadi ya Watanzania wanaotegemea ajira kwenye kilimo ikipungua.

Ajira za kwenye kilimo zinatajwa kupungua kutoka asilimia 75 mwaka 2012 hadi asilimia 58 mwaka 2018. “Ajira imehama kutoka katika kilimo kwenda katika huduma na viwanda,” alisema Swinkels.

Ripoti pia inaonyesha kuwa saa za kufanya kazi katika kilimo zimepungua kutoka 58 hadi 46.

Naye Mwakilishi wa WB nchini, Bella Bird alisema anapotembelea maeneo mbalimbali nchini hukutana na vijana wakijishughulisha na kilimo na kuishauri Serikali ili kupunguza kiwango cha umaskini iwekeze katika kilimo biashara kwa kuhakikisha teknolojia na elimu inapatikana kwa vijana.

Akizindua ripoti hiyo, Bashungwa alisema Serikali ya Awamu ya Tano inatekeleza miradi mbalimbali ya kimkakati ambayo lengo lake kuu ni kuondoa umaskini na kukuza uchumi.

“Niwasihi viongozi wenzangu tuendelee kufanya kazi kwa juhudi na maarifa zaidi na tuendelee kuunga mkono juhudi za Rais kwa kutekeleza kwa vitendo na kusimamia kwa dhati miradi mikubwa inayoendelea nchini,” alisema.Alisema ni imani yake kuwa kiwango cha umaskini kitaendelea kupungua zaidi ya asilimia 26.4 ya mwaka 2017/18.

Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu, Dk Albina Chuwa alisema takwimu zinaonyesha chakula cha kalori 2,200 kinachotakiwa kwa mtu mzima kwa siku kinapatikana kwa Sh1,109.53 bila kujali eneo alipo mhusika.

“Ukuaji wa uchumi kwa miongo miwili mfululizo unahusiana na kupungua kwa kiwango cha umaskini nchini,” alisema.

Alisema kilimo kimekuwa kikikuwa kwa zaidi ya asilimia sita nchini.

Chanzo: mwananchi.co.tz