Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

RIPOTI MAALUMU: Ahadi ya soko la nje ilivyogeuka kilio kwa wakulima wa muhogo wa mkoani Tanga

35145 PIC+MIHOGO RIPOTI MAALUMU: Ahadi ya soko la nje ilivyogeuka kilio kwa wakulima wa muhogo wa mkoani Tanga

Tue, 8 Jan 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Tanga. Kama kuna watu ambao hawatasahau machungu ya mwaka 2018, basi wakulima mihogo wa Mkoa wa Tanga wamo.

Wameuweka katika kumbukumbu zao kuwa ni mwaka uliowaingiza katika hasara na ‘msiba’ mkubwa wa kukosa soko la mihogo waliyozalisha kwa wingi kuliko wakati mwingine wowote baada ya kuhakikishiwa soko bila mafanikio.

Takribani kila kijiji mkoani Tanga, isipokuwa maeneo ya milima ya Usambara zilipo wilaya za Korogwe, Lushoto na Mkinga, wakulima wamelima mihogo kwa wingi baada ya kuahidiwa soko na bei nzuri.

Hamasisho la kulima mihogo lilianzishwa na viongozi wa serikali na baadhi ya mashirika yasiyo ya kiserikali wakiwaeleza wakulima kwamba kuna soko kubwa kutoka nje ya nchi.

Hamasa hiyo ilisababisha wananchi wengi kujiingiza katika kilimo cha mihogo. Wengine walienda mbali na kuamua kukopa kwenye taasisi za fedha kama benki, vikoba na saccos kwa matarajio ya kuzirejesha baada ya kuuza kwa faida.

Maelezo ya wahamasishaji wa kilimo cha mihogo ni kwamba mkulima ataweza kuuza hadi Sh4 milioni kila ekari moja iliyopandwa vizuri, kukomaa na kuvunwa baada ya miezi sita hadi saba.

Katika baadhi ya mashamba, zao hilo limeharibika kwa kugeuka miti kutokana na kutovunwa kwa wakati kwa sababu wakulima hawana soko.

Mkulima wa mihogo katika Kijiji cha Kirare wilayani Tanga, Jumanne Kivinge hajui la kufanya anaposhuhudia zaidi ya ekari zake 10 za mihogo zinavyoharibika kwa kuchelewa kuvunwa kutokana na kukosa soko.

“Tulihamasishwa tulime na kuahidiwa kila kilo ya muhogo itanunuliwa kwa Sh250. Shambani kwangu nina muhogo aina ya Mpemba niking’oa shina moja tu napata kuanzia kilo 4 hadi tano na kwa miche 1,500 niliyonayo nilikuwa na uhakika wa kupata Sh 6.7 milioni kwa kila ekari,” anasema.

Kivinge aliamini kuwa angepata Sh67 milioni atakapouza ekari zote 10 alizolima lakini sasa anasema amechanganyikiwa kwa kuwa hajitokezi hata wa kununua tenga la mihogo 100 kwa Sh10,000 wakati miaka ya nyuma walikuwa wakiuza kwa bei ya Sh35,000 kwa kila tenga.

“Maana yake hapo muhogo ambao ilikuwa niuze kwa Sh25,000 kwa kila tenga kama ningeuza kwa bei iliyotangazwa ya Sh250 lakini sasa hata Sh10,000 sipati tena,” anasema Kivinge.

Mwalimu mstaafu, Chausiku Ramadhani wa Muheza anasema alipohamasishwa kuhusu faida ya kilimo cha muhogo aliamua kuchukua mkopo wa Sh30 milioni benki kulimia ekari 50 akitarajia kupata Sh225 milioni baada ya mavuno na kuuza kwa bei ya Sh45 milioni kila eka.

“Nimepata muhogo mwingi sana lakini unaozea shambani hakuna soko tuliloahidiwa… sijui nitarejeshaje mkopo.”

Mfanyabiashara Charles Massawe wa Ngamiani, Tanga anasema alikopa Sh7 milioni kwa mjomba wake na kufanikiwa kulima ekari 10 katika Kijiji cha Kirare akitarajia kupata Sh45 milioni baada ya mavuno lakini ameambulia hasara.

Mfanyabiashara Khalid Ali wa Tanga anasema hamasa ya kilimo cha mihogo ilimvutia akaamua kulima ekari 50 wilayani Pangani akitarajia kupata faida ya Sh222 milioni lakini hadi sasa mihogo ipo shambani. Anasema hatarajii kupata hata Sh50 milioni.

Mkulima maarufu wa zao hilo aliyekuwa kuwa mkuu wa mkoa wa Tanga, Mwantumu Mahiza anasema kama kuna jambo linalomsumbua ni kukosekana kwa soko la uhakika la zao hilo kwa wakulima wa kawaida.

Mahiza ambaye pia aliwahi kuwa naibu waziri wa elimu anauza muhogo wake nje ya nchi, lakini anasema kuna haja ya kutafuta mbinu za kuwawezesha wakulima kusindika zao hilo ili wauze unga au makopa yaliyokaushwa kitaalamu.

“Muhogo usipovunwa kwa wakati lazima utaoza au kuwa miti. Tatizo ni kwamba tulielekeza nguvu nyingi kuhamasisha wakulima walime lakini hatukujiongeza kwa kutafuta plan B (mpango mbadala) ya soko la muhogo mbichi,” anasema Mahiza.

Inakadiriwa kuwa wakulima mkoani Tanga walilima wastani wa ekari 645,183 katika msimu wa mwaka 2018 wakitarajia kuvuna takribani tani 2,580,732.

Wilaya ya Handeni ndiyo ambayo ilijiwekea utaratibu mzuri wa kuhamasisha kilimo cha zao hilo kwa viongozi wake kuhamia mashambani kwa wakulima huku wakigawa mbegu.

Akizungumzia changamoto ya soko, Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Godwin Gondwe anasema ofisi yake ilitafuta mbinu za kuokoa muhogo ulioko shambani wakati wakulima wakisubiri kiwanda kikubwa cha Kirare kinachotarajiwa kumaliza kabisa changamoto ya soko la muhogo mbichi.

Anasema wakati kiwanda hicho kinatarajiwa kukamilika mwaka huu, kampuni ya DarCanton Investment Co Ltd kwa kushirikiana na vyama vya ushirika imekuwa ikinunua muhogo mbichi kutoka kwa wakulima.

Hadi sasa jumla ya tani 200 za muhogo uliokaushwa zimeshasafirishwa nje ya nchi na tani nyingine 2,000 zinatarajiwa kusafirishwa mwezi huu. Anasema mwaka huu suala la uhaba wa soko litabaki hadithi.

Anawataka wakulima kuongeza nguvu katika kilimo hicho kwa sababu kiwanda kingine kitakachojengwa Kwedizinga kitakuwa na uwezo wa kununua tani 43,200 kwa mwaka ambazo ni sawa na tani 120 kila siku.

Anasema mihogo ni zao la kimkakati Handeni kwa sababu mbali ya kuuzwa mbichi, itazalisha mbegu bora aina ya Mkuranga na Kiroba hivyo kuifanya kuwa kituo cha mbegu za zao hilo nchini.

“Msimu uliopita tuligawa miche milioni 285 ya mbegu za Mkuranga na Kiroba. Muhogo wake ni mtamu hata kwa kuutafuna, hauozi haraka lakini kubwa zaidi haisumbuliwi na magonjwa,” anasema Gondwe.



Chanzo: mwananchi.co.tz